Majadiliano Ya Bunge
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________ MKUTANO WA KUMI NA MOJA Kikao cha Sitini na Moja – Tarehe 29 Juni, 2018 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Najma Murtaza Giga) Alisoma Dua MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Tunaanza Kikao chetu cha Sitini na Moja, Katibu. NDG. NENELWA WANKANGA – KATIBU MEZANI: HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Taarifa ya Mwaka ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (Workers Compensation Fund) kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2016. Taarifa ya Mwaka ya Utekelezaji wa Shughuli za Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2016. MWENYEKITI: Ahsante sana, Katibu. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) NDG. NENELWA WANKANGA – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tunaanza na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, swali la Mheshimiwa Mulugo, Mbunge wa Songwe. Na. 510 Hospitali ya Kanisa Katoliki – Mbeya (Songwe) MHE. PHILIPO A. MULUGO aliuliza:- Je, Serikali haioni haja ya kuipandisha hadhi Hospitali Teule ambayo inamilikiwa na Kanisa Katoliki Dayosisi ya Mbeya iwe Hospitali Teule ya Wilaya ili wananchi wa Songwe waweze kupata huduma stahili? MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu ya swali hilo. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Philipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 2 Januari, 2018, Halmashauri ya Wilaya ya Songwe ilisaini mkataba na Kanisa Katoliki, Jimbo la Mbeya uliopandisha hadhi ya Hospitali ya Mwambani kuwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Songwe.
[Show full text]