Online Document)
Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ___________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________ MKUTANO WA KUMI NA TANO Kikao cha Ishirini na Nane – Tarehe 6 Juni, 2014 (Kikao Kilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, maswali, tunaanza na Ofisi ya Waziri Mkuu, atakayeuliza swali la kwanza ni Mheshimiwa Felix Mkosamali. Na. 197 Huduma za Zahanati – Muhambwe MHE. FELIX FRANCIS MKOSAMALI aliuliza:- Vijiji vya Magarama, Kigina na Nyarulanga katika Jimbo la Muhambwe havina Zahanati:- Je, Serikali imefikia wapi katika kuvipatia vijiji hivyo huduma ya zahanati? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felix Francis Mkosamali, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, ni kweli Vijiji vya Kigina, Magarama na Nyarulanga, vilivyopo katika Jimbo la Muhambwe, havina Zahanati. Ujenzi wa Zahanati nchini unafanyika kupitia Mpango wa Fursa na Vikwazo Katika Maendeleo, ambapo Wananchi wenyewe huibua Miradi ambayo inazingatia changamoto zilizopo. Halmashauri huchangia gharama kidogo za utekelezaji wa Miradi hiyo kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa pamoja na usimamizi. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Zahanati katika Kijiji cha Kigina umekamilika kwa Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 na ujenzi wa nyumba ya Mganga uko katika hatua ya mwisho, ambapo Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2013/2014, ilitenga jumla ya shilingi milioni 20. Aidha, ujenzi wa jengo la wagonjwa (OPD) wa nje katika Kijiji cha Magarama upo hatua ya mwisho kukamilika. Serikali imetenga shilingi milioni 23 katika bajeti yake ya mwaka 2014/2015 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba za watumishi.
[Show full text]