MKUTANO WA TATU Kikao Cha Kumi – Tarehe 15 Aprili, 2021
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA TATU Kikao cha Kumi – Tarehe 15 Aprili, 2021 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Dkt. Tulia Ackson) Alisoma Dua NAIBU SPIKA: Waheshimiwa, tukae. Katibu. NDG. NEEMA MSANGI – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU NAIBU SPIKA: Maswali Waheshimiwa Wabunge, tutaanza na Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini sasa aulize swali lake. Na. 79 Kuongeza Vituo vya Afya Jimbo la Nkasi Kusini MHE. VICENT P. MBOGO aliuliza:- Jimbo la Nkasi Kusini lina Kata 11 na Kituo cha Afya kimoja pekee:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Vituo vya Afya hasa katika Tarafa ya Chala, Kate, Myula, Sintali na Ninde? 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Dkt. Dugange, majibu. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: - Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, ambapo katika mwaka wa fedha 2017/2018 hadi mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imejenga na kukarabati Vituo vya Afya vya Nkomolo na Kirando kwa gharama ya shilingi milioni 900. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi. Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi tatu na shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
[Show full text]