MKUTANO WA TANO Kikao Cha Kwanza – Tarehe 1 Novemba, 2016
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA __________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA TANO Kikao cha Kwanza – Tarehe 1 Novemba, 2016 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) WIMBO WA TAIFA (Hapa Wimbo wa Taifa Uliimbwa) D U A Mwenyekiti (Mhe. Najma Murtaza Giga) Alisoma Dua MWENYEKITI: Katibu. DKT. THOMAS D. KASHILILAH - KATIBU WA BUNGE: TAARIFA YA SPIKA MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, katika Mkutano wa Nne wa Bunge, Bunge lilipitisha Miswada ya Sheria ifuatayo:- (i) Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa wa mwaka 2016(The Access to Information Bill 2016); (ii) Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa mwaka 2016 (The Valuation and Valuers Registration Bill, 2016); (iii) Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa mwaka 2016 (The Government Chemist Laboratory Authority Bill, 2016); (iv) Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa mwaka 2016, (The Chemist Professionals Bill, 2016); (v) Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania wa mwaka 2016 (The Agricultural Research Institute Bill, 2016); na 1 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) (vi) Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Uvuvi wa Tanzania wa mwaka 2016 (The Fisheries Research Institute Bill, 2016). Kwa taarifa hii, napenda kuliarifu Bunge hili Tukufu kwamba, tayari Miswada hiyo imekwishapata kibali cha Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Sheria za nchi ambazo sasa zinaitwa:- (i) Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa Na. 6 ya mwaka 2016 (The Access to Information Act. No.6, 2016); (ii) Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini, Na. 7 ya mwaka 2016 (The Valuation and Valuers Registration Act, No.7, 2016); (iii) Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na. 8 ya mwaka 2016 (The Government Chemist Laboratory Authority Act, No.8, 2016); (iv) Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia Na. 9 ya mwaka 2016, (The Chemist Professionals Act, No.9, 2016); (v) Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania, Na.10 ya mwaka 2016 (The Agricultural Research Institute Act, No.10, 2016); na (vi) Sheria ya Taasisi ya Uvuvi, Tanzania, Na.11 ya mwaka 2016 (The Fisheries Research Institute Act, No.11, 2016). Waheshimiwa Wabunge, imetolewa leo hii na Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Job Ndugai, leo tarehe 1, Novemba 2016. Katibu! DKT. THOMAS D. KASHILILAH – KATIBU WA BUNGE: Hati za kuwasilisha mezani. HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Taarifa za Matoleo ya Gazeti la Serikali pamoja na Nyongeza zake yaliyochapishwa tangu Mkutano wa Bunge uliopita kama ifuatavyo:- (i) Toleo Na. 16 la Tarehe 15/4/2016; (ii) Toleo Na. 17 la Tarehe 22/4/2016; 2 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) (iii) Toleo Na. 21 la Tarehe 20/5/2016; (iv) Toleo Na. 36 la Tarehe 26/8/2016; (v) Toleo Na. 37 la Tarehe 02/9/2016; (vi) Toleo Na. 38 la Tarehe 09/9/2016; (vii) Toleo Na. 39 la Tarehe 16/9/2016; (viii) Toleo Na. 40 la Tarehe 23/9/2016; (ix) Toleo Na. 41 la Tarehe 30/9/2016; (x) Toleo Na. 42 la Tarehe 07/10/2016; na (xi) Toleo Na. 43 la Tarehe 14/10/2016. MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa Waziri wa Ncho Ofisi ya Waziri Mkuu, sasa namuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Mwongozo wa kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018. MWENYEKITI: Ahsante sana Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Sasa namuomba Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti. MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA BAJETI: Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti juu ya Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018. MWENYEKITI: Ahsante, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti. Sasa namkaribisha Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Fedha na Mipango. MHE. DAVID E. SILINDE - NAIBU MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI WA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO: Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Fedha na Mipango juu ya Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018. MWENYEKITI: Ahsante, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani. Katibu, tuendelee. 3 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) DKT. THOMAS D. KASHILILAH - KATIBU WA BUNGE: MASWALI NA MAJIBU MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tunaanza na Ofisi ya Waziri Mkuu na swali la kwanza litaulizwa na Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Viti Maalum. Na. 1 Makazi Maalum kwa Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:- Kumekuwa na mauaji ya Watanzania wenye ulemavu wa ngozi kwa muda mrefu sasa ambapo hali hiyo imesababisha wananchi wasamaria wema kuanzisha makazi maalum kwa ajili ya kuwahifadhi. Je, Serikali inashiriki vipi katika kutoa huduma muhimu ikiwemo kuhakikisha wanapata elimu, matibabu pamoja na lotion? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha takriban miaka kumi, kumekuwa na matukio ya vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino ambavyo vimesababisha baadhi ya wasamaria wema kuanzisha makazi maalum ya kuwahifadhi watu wenye ualbino. Licha ya matukio hayo kupungua, bado kuna makazi yanayotumika kuwatunza watu wenye ualbino kwa sababu mbalimbali zikiwemo sababu za unyanyapaa na taarifa za baadhi ya matukio ya mashambulio japo si mara kwa mara kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita. Makazi hayo yanajumuisha yale yaliyoanzishwa na Serikali na yale yaliyoanzishwa na wasamaria wema. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika makazi haya, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inawajibika kuhakikisha kuwa watoto wenye ualbino wanapata elimu katika mazingira salama na kadri inavyowezekana kwa kuzingatia hali halisi Serikali itahakikisha watoto hawa wanapata elimu katika mazingira shirikishi. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa matibabu na mafuta maalum ya ngozi, Serikali kwa kushirikiana na Taasisi za Tiba za Ocean Road, KCMC, 4 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) Bugando na wadau wengine imekuwa ikitoa matibabu na mafuta maalum ya kuzuia athari za mionzi ya jua katika ngozi, yaani sun screen lotion, kwa watu wenye ualbino. Aidha, Serikali kupitia Bohari Kuu ya Madawa (MSD) imeandaa mkakati wa kusambaza mafuta maalum katika hospitali zote za Wilaya ili kuwasaidia watu wenye ualbino ambapo mafuta hayo yameingizwa katika kundi la dawa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji. Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali ikishirikiana na wadau wengine imeandaa utaratibu wa kuwapima macho na ngozi watu wenye ualbino na kuwapatia tiba pamoja na ushauri ili wasiathirike. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaamini kuwa suluhisho la kudumu la kuondoa vitendo vya ukatili na unyanyapaa dhidi ya watu wenye ualbino nchini ni kutoa elimu ili kubadili fikra potofu kwa jamiii kuliko kunzisha makazi na vituo. Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanikisha azma hii, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana mamlaka ya Serikali za Mitaa na wadau wengine imeanzisha kampeni ya kupinga unyanyapaa na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino kwa lengo la kutoa uelewa na kutokomeza imani potofu iliyojengeka miongoni mwa jamii kuhusu watu wenye ualbino. MWENYEKITI: Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, swali la nyongeza. MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba niulize maswali ya nyongeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa makazi haya ya watu wenye ulemavu yako ndani ya Halmashauri, je, Serikali sasa haioni haja Halmashauri ikatenga bajeti ndogo ili iweze kusaidia upatikanaji wa chakula ili wananchi hao wawe na uhakika wa kupata chakula badala ya kusubiri msaada kutoka kwa mwananchi mmoja mmoja? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na jitihada za Serikali za kupambana na mauaji haya. Je, sasa naomba Serikali inihakikishie ina mkakati gani wa haraka kuhakikisha watu hawa wanahudumiwa na vitendo hivi vinakoma ili wananchi hawa waweze kuungana na ndugu zao na jamii ili waweze kushirikiana katika shughuli mbalimbali? MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Halmashauri, ni kweli, kwa mujibu wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu labda nifafanue kwanza; jukumu la kwanza la kumlinda 5 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) mtu mwenye ulemavu linaanzia kwenye familia baadaye taasisi, Serikali kwa upande wa Halmashauri ni sehemu ya mwisho kwenye makazi kwa sababu msisitizo uko katika kuishi katika hali ya kuchangamana na wengine na kweli Halmashauri zinaagizwa kuhakikisha kwamba zinatenga bajeti kwa ajili ya kutoa misaada maalum hasa ya makazi na chakula kwa wale wanaohitaji. Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni jambo ambalo liko wazi kisheria, na tayari Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikitoa maagizo hayo na kwa kutumia fursa hii niwakumbushe wote wanaohusika na Wabunge pia kwa sababu ni Wajumbe katika Mabaraza ya Madiwani ambayo yanahusika kupanga bajeti ya Halmashauri mbalimbali kuhakikisha kwamba wanasimamia bajeti katika Halmashauri zao ili kuhakikisha kwa mba watu wenye ulemavu wanapewa kipaumbele katika masuala mbalimbali si tu ya makazi. Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu jitihada maalum, niseme tayari kumekuwa kuna jitihada mbalimbali na hata juzi tu nafikiri, siku ya Ijumaa kwa wale