Nakala Ya Mtandao (Online Document) 1 BUNGE LA TANZANIA
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ________________ MAJADILIANO YA BUNGE ________________________ MKUTANO WA KUMI NA TANO Kikao cha Kumi na Tisa – Tarehe 27 Mei, 2014 (Mkutano Ulianza Saa tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA: Taarifa ya Mwaka na Hesabu za Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha kwa Mwaka 2012/2013 (The Annual Report and Accounts of Arusha International Conference Centre for the Year 2012/2013). Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MHE. BETTY E. MACHANGU (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA): Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 na Maoni ya Kamati 1 Nakala ya Mtandao (Online Document) Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MHE. ABDULKARIM E.H. SHAH (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA ARDHI, MALIASILI NA MAZINGIRA): Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MHE. HAROUB MUHAMMED SHAMIS (K.n.y. MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI WA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA): Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MHE. PAULINE P. GEKUL (K.n.y. MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI WA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI): Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MASWALI NA MAJIBU Na. 130 Mbunge/Diwani Kutekeleza Ahadi Zake Wakati wa Uchaguzi Mdogo MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:- Je, kwa mujibu wa Sheria wakati wa Uchaguzi Mdogo kwenye kijiji, mtaa au Kata, Mbunge au Diwani anaruhusiwa kutekeleza ahadi aliyotoa siku za nyuma wakati Kampeni zikiendelea? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE alijibu:- 2 Nakala ya Mtandao (Online Document) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi wakati wa Uchaguzi Mkuu wagombea wa Ubunge au Diwani wanaruhusiwa kufanya kampeni kwa madhumuni ya kuwashawishi Wapiga Kura wawachague. Katika kuwashawishi wapiga kura wagombea wanaweza kutoa ahadi ambazo watatakiwa wazitekeleze. Inawezekana wakati wagombea waliochaguliwa Wabunge au Madiwani wanatekeleza ahadi zao katika Jimbo/Kata pakatokea uchaguzi mdogo. Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria za uchaguzi hazikatazi Wabunge na Madiwani kutekeleza ahadi zao wakati wa uchaguzi mdogo pamoja na kwamba Sheria za Uchaguzi hazikatazi, Wabunge na Madiwani kutekeleza ahadi wakati wa Uchaguzi Mdogo. Inashauriwa kwamba hekima na busara zitumike katika utekelezaji wa ahadi hizo ili isitafsiriwe kuwa mgombea au chama husika kinatoa rushwa kwa Wapiga Kura. MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Waziri nakushukuru kwa majibu yako. Lakini najiuliza ni kwa nini umepotosha na unadanganya Bunge wakati Sheria ya Gharama za Uchaguzi Namba 16 ya Mwaka 2010. Ninayo hapa hiyo Sheria, Section ya 21 Sehemu ya 5 inasema vitendo vinavyokatazwa. Naomba ni-quote section ndogo Mheshimiwa Waziri inasema hivi:- “Miradi ya kijamii au ahadi mbalimbali katika Jimbo yanaweza yakafanyika kabla ya mchakato wa Uchaguzi na kampeni kuanza. Section Namba 21 Section ndogo ya tatu, inakataza wapiga kura kusombwa kupelekwa kwenye vituo vya kupiga kura. Inakataza ahadi hizo za Wabunge na Madiwani kutekelezwa wakati kampeni zimeanza”. Mheshimiwa Waziri, kwa nini unasema hekima itumike wakati unajua ni Sheria na imekataza? (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa chaguzi tulizo nazo sasa katika nchi yetu, kuna chaguzi za Serikali za Mitaa, na Uchaguzi Mkuu ambako ni Madiwani, Wabunge na Rais. Chaguzi hizi zinaongozwa na Sheria mbili tofauti. Katika Chaguzi za Serikali za Mitaa vitambulisho vya kupiga kura au vya mpiga kura havitumiki. Mheshimiwa Waziri huoni kwamba sasa ni wakati muafaka kuleta hizo Sheria mbili zirekebishwe ili hata katika chaguzi za Serikali za Mitaa vitambulisho vya mpiga kura vitumike? (Makofi) 3 Nakala ya Mtandao (Online Document) WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafikiri wewe ndiyo umechanganya. Mimi sijadanganya. Kwa sababu aidha kwanza kuna chaguzi za aina mbili. Chaguzi ya kwanza ni ile inayoitishwa ya miaka mitano na Tume ya Uchaguzi. Wakati ule tunafanya uchaguzi ule katika kipindi cha Uchaguzi Ukuu kunakuwa na referee, Kanuni zinatolewa na Tume ya Uchaguzi inasimamia wote tunajua. (Makofi) Mambo gani yanatakiwa na mambo gani hayatakiwi. Kwa hiyo, huo uchaguzi wakati huo hakuna Mbunge katika Jimbo. Hakuna Diwani kwenye Kata. Wote tunasimamiwa na Tume ya Uchaguzi. Chaguzi ya pili mtu kafa, mtu kafukuzwa, Mwenyekiti wa Kijiji kafukuzwa. Mimi Mbunge wa Jimbo la Isimani, Mwenyekiti kafukuzwa, ninakatazwa nini kwenda kutekeleza ahadi kwenye Jimbo langu, kwani mimi ndiyo nachaguliwa? (Makofi) Diwani kafa, kafukuzwa, mimi Mbunge nitasimama kufanya shughuli zangu katika eneo pana kwa sababu Diwani kafukuzwa haiwezekani. Juzi hapa Igunga mlishitaki kesi kwamba Serikali imefanya hivi imegawa mahindi. Mbona kesi imeamuliwa tumeshinda. Tumetoa mahindi wakati kuna njaa na Mahakama ya Rufaa imesema Serikali haiwezi kusimama kutekeleza jukumu lake. (Makofi) Kwa hiyo, mimi nafikiri Mheshimiwa Gekul unachanganya mambo mawili. Haiwezekani kuna uchaguzi mdogo katika Kata, Diwani kafa, halafu hatekelezi ahadi zake, inawezekana wapi? Nani huyo atakaetekeleza ahadi zake wakati tunafanya uchaguzi mdogo kwa mtu aliyekufa. Haiwezekani, kwa hiyo kwa hiyo ni chaguzi umechanganya. Kwenye uchaguzi mkuu haiwezekani, kwa saabu unasimamiwa na Tume ya Uchaguzi na wote tunakuwa hatuna vyeo hivyo. Lakini kwenye chaguzi ndogo inategemea, kwa sababu kama ni uchaguzi wa Kijiji lazima yule Mwenyekiti wa Kijiji au kafa au kafukuzwa. Kwa hiyo hawezi kufufuka kutekeleza ahadi zake. Lakini mwenye eneo kubwa anaweza kufanya hizo kazi zake za ahadi alizofanya. Kwa hiyo Mheshimiwa Gekul nilifikiri hiyo nikuelimishe namna hiyo. (Makofi) Lakini la pili hili la Sheria za Uchaguzi kati ya Serikali, Sheria inayosimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi wa Madiwani na Wabunge. Zoezi tunalokwenda nalo sasa marekebisho ya Katiba itakuwa ndiyo wakati muafaka wa kurekebisha jambo hili. Kwa sababu jambo hili linazungumzwa sana na mmekuwa mnazungumza sana kuanzia kwenye Katiba. Kwa hiyo, mimi ushauri wangu ni kwamba tuanze kwenye Katiba. Tushirikiane wote turudi tutengeneze Katiba nzuri halafu tushirikiane baada ya hapo turekebishe Sheria ya Uchaguzi ili nia yako njema iweze kutimia. (Makofi) 4 Nakala ya Mtandao (Online Document) NAIBU SPIKA: Mmesikia mrudi kwenye Kikao hapa. Tunaendelea na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi. Swali la Mheshimiwa Catherine Valentino Magige. Kwa niaba yake Mheshimiwa Jafo. Na. 131 Utaratibu wa Kulipa Kodi ya Nyumba Kwa Mwaka Mzima MHE. SELEMANI S. JAFO (K.n.y. MHE. CATHERINE V. MAGIGE) aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuzuia utaratibu wa wenye nyumba kulazimisha wapangaji kulipa kodi ya pango la mwaka mzima hali ambayo huwaumiza sana wananchi wengi wanaohitaji nyumba za kupanga? NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentino Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1984 Serikali baada ya kutambua kero wanazopata wapangaji hususani wale wa nyumba wamiliki binafsi ikiwemo kudaiwa kodi kubwa sana na kutakiwa kulipa mwaka mzima, ilitunga sheria ya udhibiti na upangaji na kodi za nyumba yaani The Land Restriction Act No.17 mwaka 1984. Mwaka 2005 Sheria hiyo ilifutwa kupitia marekebisho ya Sheria Na. 2 ya mwaka 2005 yaani The Written Laws Miscellaneous Amendment Na. 2 Act of 2005.Sheria hiyo iliweka utaratibu utakaofuatwa na wenye nyumba kumtoza mpangaji kodi ya pango. Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mambo yaliyolalamikiwa ni kuwa Sheria hii iliwapendelea sana wapangaji kuliko wenye nyumba. Aidha, kutokana na hali hiyo, soko la nyumba limeshuka na kusababisha upungufu wa nyumba nchini na hivyo kufanya wahitaji kukubali masharti yoyote watakayopewa na wamiliki ikiwa ni pamoja na kulipa kodi kubwa kwa mwaka au zaidi. Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa ipo haja ya kuweka utaratibu wa ulipaji wa kodi ya nyumba ili wananchi wengi wenye kipato cha chini wasiumie. Naomba kulijulisha Bunge lako Tukufu sasa Wizara yangu iko katika hatua ya kuandaa Sheria ya Nyumba itakayosimamia 5 Nakala ya Mtandao (Online Document) utekelezaji wa nyumba ikiwa ni pamoja na kusimamia masuala ya upangaji na kodi ya pango. Namwomba Mheshimiwa