Majadiliano Ya Bunge ______
NAKALA YA MTANDAO (ON LINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ___________ MAJADILIANO YA BUNGE ______________ BUNGE LA KUMI NA MOJA ___________ MKUTANO WA KWANZA Kikao cha Kwanza - Tarehe 17 Novemba, 2015 (Bunge lilianza Saa Tatu Asubuhi) DKT. THOMAS D. KASHILILAH - KATIBU WA BUNGE: Naomba tukae. TANGAZO LA RAIS LA KUITISHA MKUTANO WA BUNGE DKT. THOMAS D. KASHILILAH - KATIBU WA BUNGE: Waheshimiwa Wabunge, kwa mujibu wa masharti ya Katiba, Mkutano huu wa Kwanza unaanza kwa Rais kuuitisha. Naomba kuchukua nafasi hii kusoma Tangazo la Rais kama ambavyo tumelipokea. Tangazo la Serikali Na. 513 la tarehe 6 Novemba, 2015. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Sura ya Pili, hati iliyotolewa kwa mujibu wa Ibara ya 90(1). Hati ya Kuitisha Mkutano wa Bunge Jipya. KWA KUWA, Uchaguzi Mkuu ulifanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; NA KWA KUWA, masharti ya Ibara ndogo ya kwanza ya Ibara ya 90 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, yanamtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuitisha Mkutano wa Bunge Jipya kabla ya kupita siku saba tangu Tume ya Uchaguzi kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu; NA KWA KUWA, matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 yalitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi tarehe 29 Oktoba, 2015; HIVYO BASI, mimi John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mamlaka niliyonayo chini ya Ibara ya 90(1) ya 1 NAKALA YA MTANDAO (ON LINE DOCUMENT) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, naitisha Mkutano wa Bunge Jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ufanyike katika ukumbi wa Bunge uliopo Mjini Dodoma tarehe 17 Novemba, 2015 kuanzia saa tatu asubuhi.
[Show full text]