MKUTANO WA 18 TAREHE 5 FEBRUARI, 2015 MREMA 1.Pmd
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
5 FEBRUARI, 2015 BUNGE LA TANZANIA _________________ MAJADILIANO YA BUNGE __________________ MKUTANO WA KUMI NA NANE Kikao cha Tisa – Tarehe 5 Februari, 2015 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua MASWALI KWA WAZIRI MKUU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, leo sijamwona. Kwa hiyo tunaendelea na Maswali kwa Waziri Mkuu na atakayeanza ni Mheshimiwa Murtaza A. Mangungu. MHE. MURTAZA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa vipindi tofauti vya Bunge Mheshimiwa Peter Msigwa, Mheshimiwa Mussa Zungu na hata Mheshimiwa Murtaza A. Mangungu wamekuwa wakiuliza swali kuhusiana na manyanyaso wanayoyapata wafanyabiashara Wadogo Wadogo pamoja na Mamalishe. Kwa kipindi hicho chote umekuwa ukitoa maagizo na maelekezo, inavyoonekana mamlaka zinazosimamia hili jambo haziko tayari kutii amri yako. 1 5 FEBRUARI, 2015 Je, unawaambia nini Watanzania na Bunge hili kwa ujumla? WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa Murtaza Mangungu swali lake kama ifuatavyo:- Suala hili la vijana wetu ambao tunawajua kama Wamachinga, kwanza nataka nikiri kwamba ni suala kubwa na ni tatizo kubwa na si la Jiji la Dar es Salaam tu, bali lipo karibu katika miji mingi. Kwa hiyo, ni jambo ambalo lazima twende nalo kwa kiwango ambacho tutakuwa na uhakika kwamba tunalipatia ufumbuzi wa kudumu. Kwa hiyo, ni kweli kwamba mara kadhaa kuna maelekezo yametolewa yakatekelezwa sehemu na sehemu nyingine hayakutekelezwa kikamilifu kulingana na mazingira ya jambo lenyewe lilivyo. Lakini dhamira ya kutaka kumaliza tatizo hili la Wamachinga bado ipo palepale na kwa bahati nzuri umeuliza wakati mzuri kwa sababu jana tu nimepata taarifa ambayo nimeandikiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI ambayo wanaleta mapendekezo kwangu juu ya utaratibu ambao wanafikiri unaweza ukatatua tatizo hili ambalo lipo sehemu nyingi. Nililoliona katika taarifa yao ni kwamba wao wamependekeza kwamba wataunda kakikosi kazi hivi ka kiofisi, kikosi hicho kitafanya kazi kupitia viongozi wa makundi mbalimbali ya Wamachinga hapa nchini, watakuwa wanakaa nao, wanakubaliana nao juu ya maeneo ambayo wanaona ni vema yakatumika kwa madhumuni hayo. Watakubaliana vilevile juu ya muda muafaka wa kufanya hizo shughuli. Kikubwa nilichokiona katika maeleo yao wametaka sana suala la usafi katika maeneo ambayo shughuli zitaendeshwa lipewe kipaumbele. 2 5 FEBRUARI, 2015 Jambo ambalo mimi nimelikubali na wamamua kwamba wataanza na Jiji la Dar es Salaam watakutana na viongozi, watazungumza nao na uongozi kwa ujumla wakishakubaliana hilo basi wawekeane kabisa maelewano kwamba utaratibu huu sasa ndiyo utatumika na vyombo vyote vifahamu kwamba hayo ndiyo maafikiano. Kwa hiyo, mimi naamini wakifanya kazi hiyo vizuri Mwanza na Arusha wakafanya hivyo inawezekana jambo hili likamalizika vizuri sana. Pengine niseme tu kwamba wengine mnaweza mkafikiri jambo hili ni la Kitanzania tu, hapana. Vijana hawa wapo sehemu nyingi kwa sababu ni mambo yanayotokanana ajira Ugumu wa kupata ajira kwa vijana wetu. Lakini wakati mwingine hata nchi za nje, mimi nimekwenda huko nimekuta kuna kitu wanaita Sunday Markets. Kwa mfano, haina tofauti na hii. Unakuta ni watu wamekusanyika wanafanya biashara lakini kwa kipindi maalum na wakishamaliza wanaondoka. Kwa hiyo, mimi nadhani nimekubaliana nao. Hivyo naamini Mheshimiwa Mangungu pengine jambo hili tunaweza sasa tukalipa sura tofauti kuliko huko tulikotoka. MHE. MURTAZA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa majibu mazuri. Kwa kipindi hiki cha mpito wakati hayo yakiendelea, je, uko tayari kutoa kauli ili unyanyasaji ambao unafanyika dhidi ya wafanyabiashara hao wadogowadogo pamoja na waendesha Pikipiki isimamishwe mara moja kwa maana kwamba sasa hivi wanyang’anywa mali zao, wanapelekwa Mahakamani, wanapigwa faini lakini zile mali zinataifishwa na hatujui kama mali hizo zinaingia katika mfuko wa Serikali au zinaingia katika mfuko wa nani. WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika,wazo ni zuri lakini mimi nafikiri wazo hili ambalo limetoka TAMISEMI mimi nadhani ni jema zaidi. 3 5 FEBRUARI, 2015 Ninachoweza kushauri ni kwamba madam Bunge linamalizika ndani ya siku mbili zijazo, zoezi hili lianze wiki ijayo yaani kukutana huku wafanye wiki inayokuja ili waweze kuanza utaratibu huu mapema kadri itakavyowezekana. MHE. HIGHNESS S. KIWIA:Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuanza kumwuliza swali Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu, leo ni mara ya nne ninasimama katika Bunge hili Tukufu, nikikuuliza swali lile lile linalohusiana na kufukuzwa Madiwani wangu watatu wa Manispaa ya Ilemela wa CHADEMA na sasa ni miaka miwili imepita na mara zote umekuwa ukinipa majibu yenye matumaini yasiyo kuwa na ukamilifu. Hoja ya msingi ni uhalali wa kufukuzwa kwao kwa sababu moja tu kwamba hawakuhudhuria vikao vitatu vya kawaida. Mara ya mwisho kauli yako ulisema kwamba umeagiza jopo la Wanasheria ili waweze kuangalia uhalali na ukweli wa suala hili. Mheshimiwa Waziri Mkuu, suala hili limechukua muda mrefu sana na miaka miwili ni mingi sana. Kwa niaba ya wananchi wa Ilemela, leo unawaambia nini kuhusiana na mustakabali wa Kata tatu hizi ambazo zimekosa uwakilishi kwa muda wa miaka miwili sasa? WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Kiwia nakubaliana na wewe kabisa, naomba radhi kama unaona tumechelewa sana. Lakini limetokana na tatizo lenyewe kwani lilikuwa ni la kisheria zaidi kuliko tulivyokuwa tumefikiria. Ilibidi katika hatua za mwisho hapa tukakubaliana tukaunda jopo la Wanasheria ili kutupa tafsiri ya baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa yanaleta utata. Bahati nzuri ile timu imemaliza kazi yake, wameleta kwangu na juzi nimesaini barua kwenda TAMISEMI nikitoa uamuzi wa mwisho juu ya jambo hili. 4 5 FEBRUARI, 2015 Kwa hiyo, mimi nafikiri sasa limemalizika baada ya ushauri tulioupata kutoka kwa wanasheria. MHE. HIGHNESS S. KIWIA: Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na maelezo haya ambayo hayafanani na maelezo ya huko nyuma wakati tulipoandika barua ya kwanza na matokeo yake ikaishia kwa Mkuu wa Mkoa na haikufika kwa wahusika. Naomba uwahakikishie wananchi wa Ilemela hususani wa Kata hizi tatu za Kirumba, Nyamanoro pamoja na Ilemela, ni lini maamuzi ambayo yamefikiwa yatawafikia ili tuweze kupata mustakabali na mazingira ya amani katika Jimbo letu la Ilemela. Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, hiyo barua nimeisaini juzi wakati nipo Dar es Salaam, inakwenda kwa Waziri wa Nchi TAMISEMI kama ilivyo kawaida. Kwa hiyo, ninachoweza kukuaminisha tu ni kwamba halitachukua muda mrefu kutoka TAMISEMI kwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ili yeye sasa aweze kutoa taarifa kwa kwenye mamlaka inayohusika na wahusika waweze kujulishwa. MHE. ENG. MOHAMED HABIB JUMA MNYAA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika kukuza democracy, Tanzania imesifika na imefanya jambo zuri sana la kupigiwa mfano. Mwaka jana, Serikali imesifiwa sana kupitia Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, iliporuhusu wajumbe wa Bunge hilo kupiga kura wakiwa nje ya nchi. Kwa kuwa, mwaka huu tuna Uchaguzi wa Rais na Wabunge, na kwa kuwa jambo hili linakwenda vizuri sana na principles za kidunia za Human Rights, za African Charter on Human Rights and Peoples Rights za United Nations ambazo Tanzania imesaini. 5 5 FEBRUARI, 2015 Je, utaratibu gani au maandalizi gani yameshafanywa katika uchaguzi wa mwaka huu wa Rais na Wabunge kwamba Watanzania waliopo nje ya nchi ambao wamejiandikisha katika daftari la kupiga kura wataruhusiwa kupiga kura na mipango gani imetengenezwa? SPIKA: Ahsante kwa kuuliza kwa kifupi, Mheshimiwa Waziri Mkuu! WAZIRI MKUU:Mheshimiwa Spika, swali zuri lakini sina hakika kama Mnyaa wale jamaa wakipiga kura kule kama utawakubalia maana naona mna tatizo nao sana. Lakini jambo hili tumelipeleka kwenye Tume ya Uchaguzi ili wao waone ni utaratibu gani ambao utatumika ili kuwezesha ndugu zetu ambao wako nje sehemu mbalimbali kama Uarabuni, Ulaya, China na kadhalika ili naowaweze kushiriki katika Uchaguzi Mkuu ujao. Sasa tulisha-attempt huko siku za nyuma ilionekana kama kuna matatizo kidogo ya kitaalamu taalamu hivi na hasa unapokuwa sasa na utaratibu mpya ambao tutakwenda nao katika Kuandikisha Wapiga Kura ndiyo maana tumesema bora tuwaachie wao ili waone ni namna gani hili jambo wanaweza wakalisimamia. MHE. ENG. MOHAMED HABIB JUMA MNYAA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Uchaguzi wa Rais ni wa Jamhuri nzima ya Tanzania kwa hiyo kuachia upande mmoja si suala zuri kwa sababu Tanzania ni nchi moja. Na kwa kuwa, muda mchache uliobakia wa Mabunge. Je, jambo hili tutalifanya kisheria ambayo italetwa hapa Bungeni ili tufanikishe jambo hili? WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, sheria ya Uchaguzi ipo na imeweka utaratibu wa namna watu watakavyoshiriki katika Upigaji wa Kura. 6 5 FEBRUARI, 2015 Suala hapa ni pale anapokuwa na Mpiga Kura hayupo nchini unamwekea utaratibu gani utakaomwezesha na yeye kushiriki katika Uchaguzi huu. Ndiyo maana nasema ni suala kimsingi linalopaswa kusimamiwa na Tume hizi mbili, ya Zanzibar na Tume ya Taifa ya Bara ili kuweka utaratibu. Itakuwa ni utaratibu wa kawaida tu ambao utawawezesha watu hawa kushiriki. Suala ni namna tu watakavyofanya kwa sababu wakati wa Bunge la Katiba tuliweza kufanya hivyo ingawa kulikuwa na matatizo ya hapa na pale lakini iliwezekana. Kwa hiyo, mimi naamini Tume inaweza kabisa ikaona ni utaratibu gani ambao hautaleta kikwazo, tunaweza tukautumia na tukawawezesha wananchi kushiriki. MHE. DKT. ANTONY G. MBASSA: Mheshimiwa Spika,nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kumwuliza Waziri Mkuu swali. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kumekuwa na tatizo la muda