Majadiliano Ya Bunge ______
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _________________ MAJADILIANO YA BUNGE _____________________ MKUTANO WA KUMI Kikao cha Saba – Tarehe 6 Februari, 2008 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Samuel J. Sitta) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kabla sijamwita Katibu kwa orodha ya shughuli za leo, ninapenda kwanza nimpongeze Corporal Fauster. Napenda niwafahamisheni, ni mara ya kwanza katika historia ya Bunge letu Spika kutanguliwa na Sergeant-At-Arms ambaye ni mwanamke. Tulikwishasema awali Bunge hili litaendeshwa kwa viwango na viwango ni pamoja na kuzingatia jinsia. Hakuna kazi ambazo ni za wanaume tu peke yao. Ahsante sana Corporal Fauster. (Makofi) Waheshimiwa Wabunge, nimerejea, nimesitisha safari ya Marekani. Nalazimika kutoa maelezo kwa sababu ya maneno mengi tu. Safari ile kwenda kule ilipangwa kwa kuzingatia mambo mawili :- Moja, ni umuhimu tu wake. Wenzetu Amerika, wiki ya pili ya Mwezi Februari kila mwaka mihimili yote mitatu ya Dola wanakaa pamoja kwa mlo wa asubuhi, inaitwa National Prayer Breakfast. Pamoja na mambo mengi yatakayofanyika, Rais wao ataongea pale kwenye Prayers Breakfast. Lakini wanawatambua baadhi ya viongozi mashuhuri ambao wana ushirikiano mwema nao. Mimi kama Spika wa Bunge hili, nilialikwa kwa msingi huo. Kwa hiyo, hoja kwamba labda ningeweza kumtuma mtu mwingine, haipo kwa sababu ni mwaliko wa heshima kwa jina. (Makofi) La pili ni kwamba, nikitazama ratiba na Kanuni ya 24 ya Bunge, ilikuwa ni kwamba Miswada inaendelea na kwa hiyo, nilidhani mambo mengine kama vile taarifa za Kamati yangekuja kama ilivyo kawaida katika wiki ya mwisho, na mimi nilikuwa narudi Ijumaa asubuhi. Kwa hiyo, yote yangewezekana. Sasa hilo lilishindikana, niliwaarifu wenyeji wetu kule Marekani na wamesikitika, lakini wamesema kama wanasiasa, wameelewa,kwa sababu niliwaeleza mazingira ambayo yalinifanya nisiende.
[Show full text]