1 Bunge La Tanzania
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA TISA Kikao cha Tatu – Tarehe 1 Novemba, 2007 (Mkutano Ulianza Saa 3.00 Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU Na. 28 Majibu ya Maswali Bungeni MHE. JUMA HASSAN KILLIMBAH aliuliza:- Kwa kuwa baadhi ya majibu ya Serikali kwa maswali ya Waheshimiwa Bungeni, mara nyingi yamekuwa hayamridhishi muuliza swali na hata wananchi anaowawakilisha Bungeni hasa pale Serikali ilipotoa majibu kama Mheshimiwa Mbunge avute subira, Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Halmashauri yake na au hali ya Serikali itakapokuwa nzuri na kadhalika. (a) Je, Serikali inaweza kutueleza ni taratibu gani zinazostahili kuchukuliwa hasa pale ambapo majibu ya maswali yamepitiliza muda wa utekelezaji na vile vile kutofanikiwa kwa juhudi na nyingine za kupata ufumbuzi kutoka kwenye Halmashauri? (b) Je, kwa nini Serikali isitoe majibu yenye ukomo ili muuliza swali awe na majibu ya kuwapa wapiga kura wake badala ya kuambiwa avute subira isiyo na mwisho? (c) Je, Serikali iko tayari kuwa na utaratibu wa kufuatilia majibu ya Mawaziri na kuhimiza utekelezaji wa ahadi za Serikali? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, MAAFA NA KAMPENI DHIDI YA UKIMWI (MHE. DR. LUCAS SIYAME) alijibu:- 1 Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Hassan Killlimbah, Mbunge wa Iramba Magharibi, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Naibu Spika, maswali ya Waheshimiwa Wabunge, yanapatiwa majibu kamilifu kutoka Serikali kwa mujibu wa Kanuni za Bunge hili Tukufu. Majibu ya Serikali kwa kuzingatia Kanuni ya 37 A (1), (2) na (3) yamekuwa yakionyesha hatua zilizochukuliwa, zinazochukuliwa au zitakazochukuliwa na Serikali katika utekelezaji wa jambo lenyewe.
[Show full text]