Check Against Delivery HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA
Check Against Delivery HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA EDWARD LOWASSA, (MB), WAKATI WA KUTOA HOJA YA KUAHIRISHA MKUTANO WA SITA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA, TAREHE 9 FEBRUARI, 2007 Mheshimiwa Spika, Mkutano wa sita wa Bunge lako Tukufu umehitimisha shughuli zote zilizokuwa zimepangwa. Mkutano huu ni wa kwanza baada ya Serikali ya Awamu ya Nne kutimiza mwaka mmoja madarakani. Taarifa za mafanikio na changamoto zilizojitokeza zimewasilishwa kupitia mikutano mbalimbali ya Chama Tawala, Serikali na vyombo mbalimbali vya habari. Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa, nachukua nafasi hii tena kwa niaba ya Serikali na wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kutoa rambirambi kwako wewe Mheshimiwa Spika, kwa Waheshimiwa Wabunge wote, kwa familia, jamaa na marafiki kwa msiba uliotokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tunduru, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Bunge na Uratibu) Marehemu Juma Jamaldin Akukweti. Wote tulimfahamu Marehemu Akukweti kwa umakini na umahiri wake hapa Bungeni. Marehemu Akukweti alifariki kutokana na ajali ya ndege iliyokuwa inamrejesha Dar es Salaam baada ya kumaliza kazi ya kukagua soko la Mwanjelwa lililoteketea kwa moto mkoani Mbeya. Katika ajali hiyo Watumishi wa Serikali walipoteza maisha. Watumishi hao ni Bibi Theresia Nyantori, Mwandishi wa Habari wa Idara ya Habari; Bwana Nathaniel Katinila, Mratibu wa Mradi wa Masoko; na Bwana George Bendera, Afisa Habari Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu. Majeruhi katika ajali hiyo ambao bado wanapata matibabu lakini wametoka hosptali ni Bw. Nisetas Kanje, Katibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Bunge na Uratibu); na rubani wa ndege hiyo Bw. Martin Sumari. Tunamwomba Mwenyezi Mungu awasaidie majeruhi wote waweze kupona haraka na kurudia katika afya zao.
[Show full text]