Majadiliano Ya Bunge Mkutano Wa Kumi Na Mbili
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ______________ MAJADILIANO YA BUNGE ______________ MKUTANO WA KUMI NA MBILI Kikao cha Kumi na Tano – Tarehe 1 Julai, 2008 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Samuel J. Sitta) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU Na. 132 Kuimarisha Ulinzi na Usalama Jiji Dar es Salaam MHE. CHARLES N. KEENJA : Kwa kuwa, Serikali ya Awamu ya Nne imechukua hatua madhubuti za kuimarisha Ulinzi na Usalama kwenye Jiji la Dar es Salaam kwa kuligawa Jiji kwenye Mikoa na Wilaya za Ki-ulinzi ; na kwa kuwa, hatua hiyo haikwenda sanjari na ile ya kuigawa Mikoa ya Kiutawala:- (a) Je, ni lini Serikali itachukua hatua za kuligawa eneo la Jiji la Dar es Salaam kwenye Mkoa/Wilaya zinazokwenda sanjari na zile za Ulinzi na Usalama ? (b) Je, Serikali haioni kwamba Viongozi kwenye eneo lenye hadhi zinazotofautiana kunaleta matatizo ya ushirikiano na mawasiliano hatimaye kukwamisha utendaji kazi ? (c) Kwa kuwa, zaidi ya 10% ya wananchi wa Tanzania wanaishi Dar es Salaam. Je, Serikali haioni kwamba sasa ni wakati muafaka wa kuweka utaratibu mzuri zaidi wa Uongozi kwenye Jiji hilo ? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- 1 Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles Keenja, Mbunge wa Ubungo, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa katika hatua za kuimarisha Ulinzi na Usalama kwenye Jiji la Dar es Salaam Serikali iliamua kuligawa eneo katika ngazi ya Mikoa ambapo Wilaya zote tatu za Kinondoni, Temeke na Ilala ni Mikoa ya Kiulinzi na ngazi ya Mkoa kupewa hadhi ya Kanda Maalum ya Ulinzi na Usalama. Hatua za kuligawa eneo la Mkoa wa Dar Es Salaam katika hadhi sawa na zile za Kiutawala bado halijaamuliwa. Hivi sasa Serikali imeunda Kamati Kupitia Muundo wa Uongozi wa Halmashauri ya Jiji na Mkoa wa Dar es Salaam na kutoa mapendekezo Serikalini. (b) Mheshimiwa Spika, pamoja na kutofautiana kwa hadhi kwa Viongozi kwenye eneo moja, hakujaathiri kabisa utendaji, Ushirikiano na Mawasiliano kwa kuwa Mgawanyiko huo unaendana na mtiririko mzima wa Uongozi katika Idara hizi muhimu za Ulinzi ambazo zinaongozwa na Kanuni na Sheria zake. Hivyo, mgawanyo huu ni katika hatua ya kutekeleza majukumu tu. (c) Mheshimiwa Spika, kama ilivyoelezwa hapo juu utaratibu mzuri wa uongozi katika Jiji la Dar es Salaam utafikiriwa kutokana na matokeo ya Kamati iliyondwa na Serikali kupitia Muundo wa Jiji la Dar es Salaam ambayo kwa sasa inaendelea na kazi hiyo. MHE. CHARLES N. KEENJA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na hasa kuundwa kwa Kamati hiyo. Lakini kutokana na jibu lake kwa sehemu ya B ya swali langu ningependa kujua ni wapi kwingine ambako kuna mpango kama huu ambao Afisa mwenye hadhi kubwa anaripoti kwa Afisa mwenye hadhi ya chini zaidi na Afisa mwenye hadhi ya chini anaweza kumpa maagizo Afisa mwenye hadhi ya juu maana kama hakuna mgongano basi uko njiani waja. Mheshimiwa Spika, la pili ni kwamba tuna Kata kubwa sana Kimara, Mbezi Louise, Goba na Kibamba. Je, Serikali haioni kwamba huu ni wakati muafaka wa kugawa Kata hizi kabla ya uchaguzi wa mwakani? Mheshimiwa Spika, nakushuru sana. (Makofi) NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Charles Keenja kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapa nakubaliana na yeye anachosema hapa ni kwamba unaye RPC, RPC ambaye anafanya kazi kwa kupokea maelekezo kutoka kwa DC na yeye kwa maana hiyo anaona kwamba huu ni mgongano. 2 Kwa kawaida Ma-RPC wako chini ya Mkuu wa Mkoa lakini kwa sababu ya matatizo ambayo yameonekana yapo katika Mkoa wa Dar es Salaam ilionekana kwamba ni vizuri Mkoa wa Dar es Salaam ukapewa umuhimu wake kwa maana ya kugawanya eneo hilo katika utaratibu wa kiulinzi huu ambao anauzungumzia hapa. Kwa maneno mengine ni kwamba wanapokutana Kamati ya Ulinzi na Usalama pale Temeke au pale Kinondoni au pale Ilala wanakutana pale DC ndiye anakuwa Mwenyekiti wa ile Kamati na mle ndani kwa maana ya mfumo huu unaozungumzwa hapa maana yake RPC anakuwapo hapo ndani na ndiyo mgongano ambao uanonekana kama unakuwapo pale. Kwa maneno mengine ni kwamba RPC anafika mahali anajiona kwamba hawezi kupokea maelekezo kutoka kwa DC. Mheshimiwa Spika, lakini kama nilivyojibu hapa, hatupata tatizo lolote katika kufanya kazi hiyo na kama nilivyoeleza hapa Kamati imeundwa ili iangalie vizuri kwamba ni kwa namna gani tunaweza tukaboresha utaratibu huu. Sasa ameuliza hapa ni eneo gani lingine ambalo limewahi kufanya hivyo, sinalo mimi eneo ninalolifahamu lakini najua kwa mantiki yake ndiyo hiyo. Amezungumzia habari ya Kata hapa kwamba yeye haoni kuna umuhimu wa kuzigawanya kata zile. Suala la kata hatuna tatizo nalo kabisa sisi tunasema kwamba Kata zitasaidia kwa ajili ya kuimarisha mfumo huu na kama tulivyojibu hapa tunaomb maombi yale yaletwe yote ili tuweze kuyashughulikia yote kwa pamoja na hivyohivyo tumefanya hivyo kwa upande wa ulinzi kwamba kuna Kata zake na Wilaya zake. (Makofi) MHE. GODFREY W. ZAMBI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, Dar es Salaam ni Jiji ambalo linakua sana inaonekana hata halmashauri za Jiji ambazo zipo pengine zinashindwa hata kufanya kazi sawasawa kulifanya Jiji la Dar es Salaam likaonekana ni Jiji zuri machoni pa watu wengi. Je, sasa Serikali haioni kwamba wakati pengine umefika kuliundia Jiji la Dar es Salaam Wizara maalum kama nchi nyingine zinavyofanya ili iweze kufanya kazi vizuri zaidi kwa kuwa na Bajeti ambayo Waziri Maalum atalisimamia? 3 NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Godfrey Zambi, kama ifuatavyo; Mheshimiwa Spika, huu utaratibu ambao Mheshimiwa Zambi anauzungumzia ni utaratibu ambao mimi nimewasikia wenzetu wa Nairobi wanauzungumzia na wala si kitu cha ajabu sana kwa maana ya kwamba wao wanaona ili waufanye mji ule uweze kufanya kazi kwa ufanisi lile Jiji la Nairobi wameligeuza wakalifanya sasa linakuwa na Wizara yake. Mheshimiwa Spika, hivi nilivyozungumza hapa Wizara na Serikali kwa ujumla tumekubaliana kwamba tuunde Kamati ambayo itaangalia mfumo mzima wa kiutawala wapo watu ambao wamebobea pale Mzee Mmari ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI, wako watu kama Mzee Nsakaisi watu ambao wana utaalamu mkubwa. Mimi nina hakika kwamba tutachukua wazo hili na tutalipeleka kwao kwamba yapo mawazo ya kufikiria kwamba Dar es Salaam iwe ni Wizara ili kuweza kuleta ufanisi zaidi na kama itakubalika basi kwa maana hili ni suala la Sheria ya Serikali basi litakuwa limefanyiwa kazi kwa msingi huo. Na. 133 MHE. MOHAMED RAJAB SOUD aliuliza:- Kwa kuwa, Serikali iliamua kwa makusudi matumizi ya njia tatu (3) kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari Jijini Dar es Salaam na kwa kuwa, lengo hilo zuri sasa limegeuka kuwa chanzo kipya cha vifo kwa wananchi wetu:- Je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kuboresha utaratibu huo ili kupunguza au kuondoa kabisa vifo kwa waenda kwa miguu? NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohammed Rajab Soud, Mbunge wa Jang’ombe, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, uamuzi wa Serikali wa kuanzisha utaratibu wa njia tatu katika Jiji la Dar es Salaam ulilenga kupunguza msongamano wa magari hususan nyakati za asubuhi na jioni. Utaratibu huu umeweza kusaidia kupunguza msongamano wa magari na wananchi kuweza kuwahi shughuli zao saa za asubuhi na kuwahi kurudi majumbani wao muda wa jioni.Takwimu za ajali zilizotokea katika barabara za Morogoro na Ali Khasan Mwinyi kuanzia tarehe 21 Mei, 2007 hadi Mei, 2008 4 zinaonyesha kupungua kwa kiasi kikubwa. Kupungua kwa ajali hizo kumetokana na juhusi za Serikali kufanya yafuatayo:- (i) Kuendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara juu ya utaratibu huo wa njia tatu. (ii) Kuweka alama za barabarani (Road Signs) kwa watumiaji wa barabara. (iii) Kuongeza idadi ya Askari wa Usalama Barabarani hasa katika maeneo ambayo njia tatu huanza kutumika na kumalizikia na kwenye vivuko rasmi vya waenda kwa miguu? (iv)Kuzifanyia matengenezo barabara ndogo ndogo kwa nia ya kupunguza msongamano katika barabara Kuu za Jijini. Barabara zinazohusika na mpango huu ni:- - Kigogo – Mburahati – Ubongo Maziwa; - Twiga – Jangwani – Kigogo – Tabata Dampo; - Vingunguti – Segerea; - Africana – Njia panda ya Kawe; na - Jet Club – Davis Corner – Mtongani. Mheshimiwa Spika, ni vizuri ikaeleweka kwamba mpango wa njia tatu siyo suluhisho la kudumu la tatizo la msongamano katika Jiji la Dar es Salaam. Mikakati ya baadaye ya kudumu ni pamoja na:- (i) Kujenga barabara za pete (ring roads); (ii) Kujenga miji modogo yenye huduma zinazotakiwa nje ya Jiji (Satellite Towns); (iii) Kupanua vituo vya daladala; na (iv) Kuanzisha mradi wa mabasi yaendayo kasi. Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba nichukue fursa hii kuwaomba watumiaji wote wa barabara kufuata na kuzingatia maelekezo ya matumizi ya njia tatu ili kupunguza msongamano na ajali ambazo pia husababisha vifo kwa watumiaji wa barabara. MHE. MOHAMED RAJAB SOUD: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa, anakiri daladala ndiyo chanzo kikubwa kwa ajali za njia tatu. Je, Serikali inachukua hatua gani zaidi kuhusu wanaosababisha ajali hizo? La pili, kwa kuwa Bima mpaka hivi sasa hawatambui hizi njia tatu na ajal haina miadi. Je wanaopata