HOTUBA YA MHESHIMIWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AKIFUNGUA MAFUNZO ELEKEZI KWA VIONGOZI NA WATENDAJI WAKUU WA SERIKALI TAREHE 9 MEI, 2011 KATIKA UKUMBI WA ST. GASPAR - DODOMA

Mheshimiwa Waziri Mkuu;

Mheshimiwa Jaji Mkuu;

Wazee Wetu, Mzee na Mzee Pius Msekwa;

Ndugu Mawaziri;

Ndugu Naibu Mawaziri;

Ndugu Makatibu Wakuu;

Ndugu Naibu Makatibu Wakuu;

Wakuu wa Vyombo vya Dola;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana:

Ukaribisho

Nianze kwa kuwakaribisha nyote kwenye Semina Elekezi inayojumuisha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu. Kama lilivyo jina lake, Semina hii ni ya kuelekezana juu ya namna tutakavyotimiza majukumu yetu katika Serikali. Tulikuwa na Semina kama hii mwaka 2006. Imetusaidia kupata mafanikio tuliyoyapata miaka mitano iliyopita. Naamini na Semina hii itatusaidia kupata ufanisi tunaoutarajia na ambao wananchi wanautarajia kutoka kwetu.

Ndugu Viongozi na Watendaji wa Serikali;

Niruhusuni niombe radhi kwa niaba ya Viongozi Wakuu wawili kutokuwa nasi siku ya leo. Wa kwanza ni Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal na wa pili ni Rais wa na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. . Makamu wa Rais yuko Uturuki kuniwakilisha katika LDC Summit. Mwanzoni nilikubali kushiriki kwenye LDC Summit, lakini baada ya tarehe za Semina yetu kubadilika na kuangukia kwenye tarehe za Mkutano huo nikawa sina namna ila kutuma mwakilishi. Kwa uzito wa mkutano wenyewe na matumaini ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na wenyeji wetu kuhusu ushiriki wa Tanzania nikaona Makamu wa Rais atuwakilishe. Makamu wa Rais amefuatana na Mheshimiwa Prof. Anna Tibaijuka, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim. Najua watakosa uhondo, lakini tutawapatia DVD ya Semina wataona na kusikia tuliyozungumza. Mheshimiwa Rais wa Zanzibar amebanwa na vikao vya maandalizi ya bajeti.

Madhumuni ya Semina

Ndugu Viongozi,

Katika Semina hii majukumu ya msingi ya Serikali ya utawala, maendeleo na ulinzi na usalama yatafafanuliwa. Pia itaelezwa jinsi kila mmoja wetu anavyohusika nayo na anavyotegemewa kutimiza wajibu wake. Katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge nilitaja malengo 13 ambayo yamejumuisha mambo makuu tutakayoyapa kipaumbele katika Serikali katika miaka mitano hii. Lakini nilikumbusha kuwa yale mambo 13 ni muhtasari wa maelekezo yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya .

Ndugu Mawaziri;

Mtakumbuka kuwa katika mkutano wangu wa kwanza nanyi niliwasisitizia umuhimu wa Ilani ya Uchaguzi kwa kila mmoja wenu na kwa Serikali yetu kwa jumla. Niliwaambia kuwa Ilani ndiyo mkataba mkuu baina ya Chama cha Mapinduzi na wananchi. Utekelezaji wake ndicho kipimo kikuu cha uwezo wetu wa kuongoza, mwaka 2015. Niliwataka kila mmoja wenu atambue ukweli huo na kutengeneza mkakati wa kutekekeleza Ilani kwa yale mambo yanayohusu Wizara yake. Sina shaka kuwa takriban miezi mitano baadae kila mmoja wetu atakuwa amekamilisha kazi hiyo na kuingiza katika mipango ya kazi ya Wizara itakayotekelezwa kuanzia bajeti itakayowasilishwa Bungeni mwezi ujao.

Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;

Siku ile pia nilisisitiza jambo kwa Mawaziri ambalo napenda kulirudia tena leo kwani linawahusu na Makatibu Wakuu. Ninyi kwa pamoja, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu ndiyo timu moja ya uongozi na utawala katika Wizara. Kama viongozi mnategemewa kuonyesha njia kuhusu nini cha kufanya kutekeleza majukumu ya Wizara nilizowakabidhi kuziongoza.

Katika jukumu lenu la utawala mnategemewa kuwa makini na mahiri katika kutumia rasilimali watu, vifaa na fedha za umma mlizokabidhiwa katika kutekeleza majukumu yenu. Mnategemewa kuwa na mipango na mikakati thabiti ya kutekeleza majukumu hayo.

Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu; Katika Wizara kila kitu huanzia na kuishia kwenu. Hakuna mwingine tena kuliko nyie isipokuwa mamlaka zilizo juu yenu; yaani Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais. Kwa sababu hiyo, ili muweze kutimiza kwa ukamilifu wajibu wenu huo hamna budi kwanza kabisa kutambua vyema majukumu yenu na jinsi ya kuyatekeleza. Semina hii ina shabaha ya kusaidia katika hilo. Lakini, njia kubwa zaidi ni ile niliyowaambia siku ile, yaani ninyi wenyewe kufanya bidii ya kujua kwa kusoma, kuona na kufanya shughuli za Wizara zenu kwa makini.

Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu mnatakiwa kuyajua kwa kina mambo yote yanayohusu Wizara mnazoziongoza. Vinginevyo hamtaongoza vizuri. Mtakuwa wababaishaji. Mtashindwa kutoa malengo maana mtakuwa hamjui nini cha kuekeleza, mtashindwa kusimamia mambo, kwa vile hamjui cha kusimamia, mtakuwa hamuonekani mkifanya chochote cha maana kwa sababu hamna jambo la kufanya zaidi ya mambo ya kawaida – routine issues. Mawaziri na Makatibu Wakuu lazima mtoke. Hiyo ndiyo njia bora zaidi ya kujua mambo yahusuyo Wizara yenu na ndiyo njia bora ya kuongoza: kuona wenyewe na kutenda. Itawafanya mjiamini kuelekeza na pia mnaposimama mbele za watu na kusema. Msiwe mangimeza. Tokeni, tembeeni kuona shughuli zenu. Tembeleeni wananchi muwafahamu, wawafahamu, mjue shida zao muwatatulie.

Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;

Ili mjue mambo ya Wizara zenu vizuri lazima mtengeneze utaratibu mzuri wa kupashana habari kuhusu mambo yanayotokea Wizarani. Utaratibu utakaomwezesha kila mmoja kujua kinachoendelea Wizarani. Msipofanya hivyo kuna hatari ya ninyi wenyewe viongozi wakuu mkawa hamjiamini na hata kuwa na kauli tofauti kwa jambo hilo hilo. Mmoja anasema hivi na mwingine anasema vile. Kuna hatari ya kuzuka kutokuelewana miongoni mwenu.

Hii pia ni muhimu sana hasa kwa sababu barua huandikwa kwa Waziri au Katibu Mkuu. Msipotengeneza utaratibu wa kupashana habari Waziri anaweza asijue anachojua Katibu Mkuu na kinyume chake. Na, baya zaidi Naibu Waziri na Naibu Katibu Mkuu wanaweza kuwa gizani kabisa. Naibu Waziri hushikilia Wizara anaposafiri Waziri na ndiye msemaji wa Wizara katika Bunge asipoyajua vyema yanayotokea au mambo yanayohusu Wizara hatakuwa msemaji mzuri na wa kujiamini wa Wizara. Naibu Katibu Mkuu hushikilia ofisi ya Katibu Mkuu anapokuwa hayupo. Hatafanya kazi kwa kujiamini na atashindwa kuamua mambo kwa sababu hana habari ya mambo yanayohusu Wizara. Mambo yatakawia na mengine kukwama kwa sababu hiyo.

Pamoja na kutoa fursa kwa kila mmoja wenu kuona na kujua kinachotokea Wizarani, jengeni utaratibu wa kukutana mara kwa mara kuzungumzia shughuli za Wizara zenu. Itasaidia sana. Ndiyo maana Jeshini kuna Officers Mess kutoa fursa ya maofisa kufahamiana na kuzungumza masuala yahusuyo shughuli zao. Mnaweza kuwa na vikao vya mara kwa mara au hata kunywa chai pamoja. Hata nyie mnaweza kuwa na utaratibu kama huo.

Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;

Narudia kuwakumbusha kwamba msingi wa utendaji Serikalini ni katiba, sheria, kanuni na taratibu. Ni muhimu kwenu kama viongozi mkajielimisha juu ya Katiba, sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinazoongoza utendaji kazi katika sehemu zenu za kazi. Uhalali wa maamuzi mtakayoyafanya hupimwa na sheria. Ukifanya maamuzi yanayokinzana na sheria utahojiwa wewe binafsi lakini pia utaibebesha Serikali mzigo wa hasara na fedheha itakayotokana na maamuzi hayo.

Lakini pia maamuzi yasiyofuata sheria yanaweza kuwa na madhara kwa wananchi. Heshimuni Katiba na fuateni sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika utekelezaji wa majukumu yenu. Katika semina hii masuala hayo yatafafanuliwa na kuzungumzwa. Kadhalika uhusiano wa Serikali na mihimili mingine ya dola yani Bunge na Mahakama utafafanuliwa.

Uwajibikaji wa Pamoja

Viongozi Wenzangu;

Wakati wote sisi sote tunapaswa kuzingatia kwamba Wizara ni moja, Serikali ni moja, lengo letu ni moja na hivyo wakati wote lazima tuwe na umoja, mshikamano na kauli moja. Serikali au Wizara isiyokuwa na umoja haiwezi kutimiza wajibu wake ipasavyo. Mawaziri na Makatibu Wakuu wasiokuwa na umoja hawatatimiza wajibu wao ipasavyo. Umoja ni kitu cha msingi sana. Unapokosekana kunakuwepo mifarakano na hatimaye huingia udhaifu katika kuamua na kutenda. Hali hiyo itasababisha wananchi kutohudumiwa ipasavyo na maendeleo yao kuathirika.

Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;

Hakikisheni kuwa katika Wizara zenu kuna umoja. Umoja huo uanzie kwenu nyinyi viongozi wakuu. Aghalabu ninyi mkiwa na umoja Wizara huwa na umoja, ninyi mkifarakana wafanyakazi nao hugawanyika. Kwa upande wa Serikali nako hali kadhalika, lazima Mawaziri wawe na umoja. Iwapo Mawaziri wana umoja, Serikali huwa na mshikamano na nguvu katika kuamua na kutenda. Wakati wote tuhakikishe kuwa tuna umoja na mshikamano miongini mwetu. Tuepuke kauli na matendo yatakayofarakanisha Mawaziri na hivyo kuleta mgawanyiko katika Serikali.

Lazima tukumbuke na kuzingatia dhana ya uwajibikaji wa pamoja. Lazima idhihirike katika ngazi ya Wizara na Serikali kwa jumla. Mawaziri, ninyi ndiyo viongozi wakuu katika Wizara zenu na Makatibu Wakuu ndiyo watendaji wakuu wa Wizara. Nyote mnawajibika katika nafasi zenu kwa maamuzi mnayoyafanya ya kisera na kiutendaji. Hamna budi kushirikiana, kushauriana na kuwekeana staha. Viongozi na watendaji wakuu wa Wizara hamna budi kujenga mahusiano mazuri na uwajibikaji wa pamoja. Haifurahishi kuona Waziri na Katibu Mkuu, au Waziri na Naibu Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu au Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu hawaelewani. Wanasemana na hata wakipingana hadharani, yaani mbele za wafanyakazi. Na baya zaidi pale wanapingana katika vyombo vya habari kuhusu maamuzi au utendaji wa Wizara au Serikali kwa ujumla. Hayo si maadili mema katika taasisi yoyote.

Uzoefu unaonesha kuwa jambo hili hutokea pale ambapo kunakuwa na kuingiliana katika majukumu au kwa kutozingatiwa kwa taratibu na maadili ya uongozi. Lazima ieleweke kuwa tukishaamua jambo kwa pamoja Wizarani au katika Baraza la Mawaziri ni uamuzi wetu sote hata kama wewe ulikuwa na mawazo tofauti. Wote tunao wajibu wa kuunga mkono na kuutetea. Kamwe hatutegemewi kuendelea kuupinga baada ya hapo. Kufanya hivyo ni kukiuka maadili ya uongozi na uwajibikaji wa pamoja. Kama unaona vigumu sana kuuafiki ni bora kutoka. Hairuhusiwi kupinga taasisi ambayo wewe umo ndani kama mmoja wa viongozi wake. Ni vyema hili likaeleweka vyema. Msitupe tabu ya kuulizana maswali na kuwasemea.

Kuwajibika Bungeni

Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;

Dhana hii ya uwajibikaji wa pamoja nayo inahusu pia shughuli za Serikali Bungeni. Miswada ya Serikali ni ya Mawaziri wote mmoja mmoja na kwa umoja wao. Mswada wa Sheria ukiletwa na Waziri mmoja, kila Waziri anao wajibu wa kuunga mkono na kuutetea. Haitegemewi na ni kinyume cha maadili cha hali juu kwa Waziri kupinga mswada wa Waziri mwenzake. Kwa kweli, tabia hii haivumiliki na anayetenda hayo amejitenga mwenyewe na Serikali.

Jambo lingine muhimu kwa Mawaziri ni kutambua kuwa kuhudhuria vikao vya Bunge ni jambo la lazima kama ilivyo kwa vikao vya Baraza la Mawaziri. Si jambo la hiari. Ni lazima Waziri ahudhuria vikao vya Bunge bila ya kukosa labda awe na sababu kubwa inayoelezeka na kukubalika. Kutembelea jimbo lako la uchaguzi ni jambo la lazima lakini siyo sababu ya kukufanya ukose vikao vya Bunge au Baraza la Mawaziri.

Uwajibikaji Kikazi na Kimaadili

Ndugu Viongozi;

Tulipokutana mara ya kwanza kule Dar es Salaam baada ya kuunda Serikali, nilizungumzia uadilifu. Napenda, leo tena kusisitiza jambo hili kwa sababu ya umuhimu wake. Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu ni viongozi wakubwa sana Wizarani, Serikalini na katika jamii. Kiongozi anatakiwa kuwa mfano mwema (role model) kwa watu anaowaongoza. Watu watamani kuwa kama yeye au kuishi kama yeye. Watu watamani kumuiga kwa uchapakazi wake, kwa tabia njema na matendo mema. Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Mkuu wasinyooshewe kidole kwa uvivu, uzembe, wizi, ubadhirifu wa mali ya umma, vitendo vya utovu wa uadilifu kama vile wizi, ulevi wa kupindukia, uzinzi, majigambo, ubabe na uonevu na dhuluma. Kuwa hivyo ni kupungukiwa sifa za msingi za uongozi. Huwakatisha tamaa wananchi na kuwafanya wapoteze imani na Serikali yao.

Uwajibikaji kwa Wananchi

Ndugu Viongozi;

Lazima tukumbuke kwamba Serikali yetu imewekwa madarakani na wananchi kwa ajili yao na siyo kwa ajili ya viongozi tuliopo madarakani. Serikali ipo kwa ajili ya kuwahudumia na kutatua matatizo yanayowakabili wananchi na kuwaletea maendeleo. Wananchi wanapenda kuona Serikali yao ina viongozi na watumishi waadilifu, wachapakazi hodari, wanaowasikiliza, wanaojali shida zao na wepesi wa kushughulikia na kutekeleza maamuzi mbalimbali ya Serikali. Ni wajibu wetu kama viongozi wakuu na watendaji wakuu kutimiza matarajio hayo ya wananchi.

Kuisemea Serikali

Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;

Moja ya mada ya semina hii inahusu mawasiliano ya Serikali. Kwa maneno mengine kuisemea Serikali. Hili ni jambo ambalo tuna udhaifu mkubwa. Sijui kwanini hatuwi wepesi kuyasemea mafanikio mengi tuliyoyapata tukaacha wasiotutakia heri wanaosema hatukufanya kitu wasikike mpaka waonekane wanasema kweli. Mwanazuoni mmoja bingwa wa habari aliwahi kusema kuwa “kufanya kitu bila kuufahamisha umma ni sawa kama kitu hicho hakijafanyika.” Mwingine anasema kuwa uongo ukisemwa mara nyingi hugeuka kuwa ukweli.

Uzoefu wa miaka mitano umeonyesha kwamba tumefanya mambo mengi lakini wananchi hawakuelezwa ipasavyo. Pia, tumeacha upotoshaji kufanywa bila ya kusahihishwa au kuchelewa sana kusahihishwa. Hivyo basi, wananchi wamekuwa wakijikuta wakiamini uongo na kulaumu au hata kuichukia Serikali kwa mambo ambayo ni potofu. Wangeambiwa ukweli mapema hawangefikia hapo. Lazima upungufu huo tuondokane nao. Lazima tuwe makini na hodari kuelezea shughuli zinazofanywa na Serikali, mafanikio yanayopatikana na changamoto zilizopo.

Aidha, tuwe wapesi kusahihisha upotoshaji wowote unaofanywa dhidi ya Serikali. Kutokufanya hivyo kumetugharimu sana. Hatuwezi kuendelea hivi wakati ninyi viongozi mpo, watu Mawizarani wapo, rasilimali zipo na vyombo vya habari vipo vinasubiri kupewa habari.

Ukuzaji Uchumi na Maendeleo

Ndugu Viongozi; Nilieleza awali kuwa mojawapo ya majukumu ya msingi ya Serikali ni kuleta maendeleo ya nchi na watu wake. Hususan Serikali inalo jukumu la kukuza uchumi na kuwapatia wananchi huduma za msingi za kiuchumi na kijamii kwa lengo la kuongeza mapato na kuboresha hali ya maisha ya Watanzania. Hii ni kazi ya msingi sana kwa Serikali kufanya na lazima kufanikiwa. Kazi hiyo ndiyo moja ya sababu na shabaha pana ya Serikali kuwepo na sisi wote kuwapo. Kwangu mimi na ninyi wenzangu kuleta maendeleo na kukidhi matumaini ya Watanzania ni changamoto na mtihani wetu mkubwa sana.

Katika Semina hii masuala ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo yamepewa nafasi ya kuzungumzwa kwa upana. Pamoja na watoa mada wa ndani, tunawashukuru marafiki zetu wa Benki ya Dunia kwa kutuletea mabingwa wa uchumi na maendeleo kuja kuzungumza nasi. Naamini uzoefu na mifano ya nchi mbalimbali kuhusu kufanya mageuzi ya kiuchumi na kujiletea maendeleo kutatusaidia kuimarisha na kuboresha hatua tunazochukua nchini.

Ndugu Viongozi;

Hakika tumefanya mengi na mafanikio yanaonekana, lakini tunayo kazi kubwa sana mbele yetu ya kufanya. Tanzania ni miongoni mwa nchi 49 maskini sana duniani. Shabaha yetu kubwa ni kutoka hapa tulipo sasa na kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Yaani, tutoke kwenye pato la wastani la USD600 la sasa hadi pato la USD1,500 mpakaUSD3,000 mwaka huo.

Niliamua na kuelekeza kuwa yafanyike mapitio ya Vision 2025 na tuigawe miaka 15 iliyosalia katika mafungu matatu ya miaka mitano mitano. Tuwe na mipango ya maendeleo ya miaka mitatu tukianzia na huu unaowiana na kipindi chetu cha uongozi. Hii itatuongoza vizuri zaidi kuelekea na kufikia lengo. Kazi ya mapitio inaendelea kama ilivyo ile ya matayarisho ya mpango wa kwanza wa maendeleo. Katika Semina hii tutapata maelezo ya awali ya kazi inayoendelea.

Ndugu Viongozi na Ndugu Washiriki;

Tunao pia Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) ambao tumekuwa tunautekeleza tangu mwaka 2005. Tumekamilisha MKUKUTA I na hivi sasa tupo kwenye utekelezaji wa MKUKUTA II ambao utakamilika mwaka 2015. MKUKUTA umetusaidia sana katika kuainisha maeneo ya kipaumbele katika bajeti. Kwa ajili hiyo, imesaidia katika jitihada za Serikali za kupunguza umaskini na kuinua hali ya maisha ya Watanzania. Bila ya shaka tutapata nafasi ya kuelezwa maudhui ya MKUKUTA II ili tuelewe namna ya kuwianisha shabaha zake na shughuli tunazozifanya katika Wizara zetu.

Ndugu Mawazirina Ndugu Makatibu Wakuu;

Kuinua hali ya maisha ya Watanzania kuna sura mbili: upande mmoja kuna kuongeza kipato chao. Yaani wasiokuwa na shughuli wapate shughuli za kufanya (kukuza ajira) na wale wenye shughuli zikue na kuimarika ili mapato yao yaongezeke. Mazungumzo yahusuyo kukuza uchumi yatatoa fursa ya kuyajadili mambo haya. Upande wa pili unahusu upatikanaji wa huduma za kiuchumi na huduma za kijamii zilizo bora na zinazotosheleza mahitaji. Wananchi wanataka kuona miundombinu hasa ya barabara zinajengwa na kuimarishwa, umeme wa uhakika pamoja na huduma za maji, afya na elimu zinapatikana kwa kiwango kinachokidhi mahitaji na ubora unaostahili.

Tumejitahidi kwa kiasi kikubwa kuongeza upatikanaji wa huduma hizo katika miaka mitano hii. Lakini, kazi iliyo mbele yetu bado ni kubwa. Upande mmoja bado tunayo kazi ya kuwafikia wale ambao huduma hizo hazijawafikia. Na, upande mwingine tunayo kazi ya kuhakikisha ubora na uendelevu wa huduma pale inapopatikana. Kuyafanya hayo ni wajibu wa msingi wa Serikali, kinachotakiwa ni kujipanga vyema kwa mipango na rasilimali watu, vifaa na fedha ili kutimiza wajibu huo.

Mapato na Matumizi ya Serikali

Ndugu Viongozi;

Uwezo wa Serikali kutekeleza majukumu yake unategemea sana kuwepo kwa rasilimali fedha na jinsi fedha hizo zinavyotumika. Upatikanaji wa rasilimali fedha unategemea ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Serikali inapata mapato yake kupitia kodi na tozo mbalimbali. Kodi ndicho chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali na chombo kikubwa cha ukusanyaji wa mapato hayo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Katika miaka mitano hii mafanikio makubwa yamepatikana na mapato yameongezeka karibu mara tatu kutoka shilingi 177 bilioni kwa mwezi hadi shilingi 430 bilioni kwa mwezi hivi sasa.

Pamoja na nyongeza hiyo bado tunao uwezo wa kuongeza zaidi. Kuna watu wengi ambao bado hawajafikiwa na wigo wa kodi. Laiti wangefikiwa mapato ya Serikali yangekuwa makubwa zaidi ya ilivyo sasa. Tutafanyaje tufanikishe hilo ni changamoto yetu sote Serikalini. Tufanye nini ili tuzibe mianya inayovujisha mapato ya Serikali ni swali ambalo sote katika Serikali hatuna budi kutoa jibu muafaka. Kwa upande wa tozo mbalimbali karibu kila Wizara inazo tozo za namna hiyo. Wengi wenu hamjafikia hata theluthi moja ya malengo. Tutafanyaje ili tufikie malengo na kuyavuka ni swali ambalo kila mmoja wetu anatakiwa kujiuliza na kutoa majibu sahihi.

Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;

Sote tunajua kuwa licha ya tozo na kodi, chanzo kingine cha mapato ya Serikali ni mikopo na misaada kutoka Mabenki, Mataifa Rafiki, na Mashirika ya Fedha ya Kimataifa. Tumepata misaada na mikopo mingi ya kutoka nje katika kipindi kilichopita na muelekeo ni kuwa tutaendelea kupata zaidi katika miaka mitano ijayo. Tunatambua haja na hoja ya kupunguza utegemezi wa misaada na mikopo kutoka nje kwa kuongeza mapato yetu ya ndani. Katika miaka mitano hii tumeendelea kupunguza utegemezi lakini nia yetu sote iwe kupunguza zaidi. Naamini tutafika kwenye shabaha hiyo iwapo tutaongeza mapato ya ndani. Naomba tuzungumzie namna ya kufikia shabaha hiyo.

Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;

Usimamizi wa matumizi ya fedha tunazokusanya kama mapato ni jukumu jingine kubwa kwetu sote. Tuna wajibu wa kuhakikisha kuwa fedha za walipa kodi zinatumika ipasavyo kuwaletea maendeleo wananchi. Katika kudhibiti matumizi ni muhimu kuelewa na kusimamia sheria, taratibu na kanuni za fedha na manunuzi ya umma kwa ufanisi wa hali ya juu. Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zinaonyesha kuongezeka kwa ubora lakini bado tunayo kazi ya kufanya kufikia kiwango cha kusema sasa tunapumua. Bado kuna makosa mengi katika kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za mapato na matumizi ya fedha za umma. Nataka tuzungumze kwa dhati tutafikaje kwenye ufanisi wa hali ya juu kwenye eneo hilo. Hali hii hatuwezi kuiacha iendelee kuboreka kwa kasi ndogo iliyopo sasa.

Viongozi na watendaji wakuu wa Serikali, mnatakiwa kuwa mfano kwa wafanyakazi mnaowaongoza kwa kuzingatia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma. Hakikisheni bajeti hazikiukwi, fedha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na sheria na kanuni za fedha zinaheshimiwa. Niliagiza Kamati za Fedha ziundwe katika kila Wizara na Idara za Serikali zinayojitegemea. Je zimeundwa? Je zinafanya kazi? Hakikisheni zipo hai na zinatimiza wajibu wake. Zitasaidia sana kwa upande wa kuongeza mapato na kudhibiti matumizi katika Wizara.

Ulinzi na Usalama

Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;

Katika semina hii tutapata nafasi ya kuzungumzia masuala ya ulinzi na usalama. Tutawasikiliza Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhusu usalama wa nchi. Pia tutamsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na Kamishna wa Tume ya Maadili ya Viongozi kuhusu uadilifu wa viongozi.

Maandalizi ya Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru

Ndugu Viongozi;

Kama mnavyofahamumwaka huu tunaadhimisha miaka hamsini ya Uhuru wa Tanzania Bara. Tumeazimia kusherehekea siku hii kwa uzito unaostahili. Niliagiza tufanye mambo kadhaa muhimu ambayo ni pamoja na kufanya tathmini ya kina ya mafanikio tuliyoyapata, katika juhudi zetu za kujiletea maendeleo. Aidha, niliagiza Wizara, idara na taasisi za Serikali na hata sekta binafsi zifanye tathmini ya shughuli zao na kuandika vitabu ili kuhifadhi kumbukumbu hizo muhimu kwetu na kwa vizazi vijavyo. Vile vile niliagiza yafanyike maonesho maalum katika Uwanja wa Maonyesho wa Julius Nyerere hapa Dar es Salaam na kote mikoani kwenye viwanja vya maonesho, kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali katika miaka 50 tangu Uhuru wa Tanzania Bara. Kwa kuwa tunakaribia nusu ya mwaka huu, ni vema sasa kukumbushana kuendelea na maandalizi ya sherehe hizo. Ni matumaini yangu kwamba kila Wizara inakaribia kukamilisha tathmini hiyo. Walio nyuma sana waongeze kasi. Tuliazimia pia kuwa tuanzishe mchakato wa kuipitia Katiba yetu. Tumeanza, lakini kuna upotoshaji mkubwa, lakini wajibu wetu sote tuliopo hapa kukabili hila na njama hizo chafu. Naamini tutafika salama. Kinachotakiwa ni mshikamano na umoja miongini mwetu.

Hitimisho

Ndugu Viongozi Wenzangu,

Ni matumaini yangu kwamba maneno haya ya utangulizi niliyosema, yatatupatia msingi wa tafakuri katika mijadala na mafunzo tutakayopatiwa katika siku nne zijazo hasa katika maeneo makuu ya semina ambayo ni pamoja na mfumo wa utawala na utendaji; uchumi na maendeleo; utawala bora; ulinzi na usalama; muungano; na masuala mtambuka.

Nimeambiwa kwamba semina hii itaendeshwa kwa utaratibu wa mihadhara kwa ajili ya kuwasilisha mada pamoja na majadiliano ya pamoja. Pia nimearifiwa kuwa kutakuwepo majadiliano katika vikundi ili kuchambua kwa undani zaidi mada zilizowasilishwa. Hivyo, rai yangu kwenu nyote muwe tayari kushiriki kwa ukamilifu katika majadiliano kwenye mihadhara kwa ukweli na uwazi bila kujali tofauti ya nyadhifa zenu. Wote muwe huru kutoa maoni yenu. Ndiyo maana tuko hapa.

Ndugu Viongozi,

Nawashukuru watoa mada waliokubali kuchangia ujuzi na uzoefu wao nasi. Baada ya kusema hayo sasa napenda kutamka kwamba Semina Elekezi kwa Viongozi na Watendaji Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefunguliwa rasmi.