HOTUBA YA MHESHIMIWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AKIFUNGUA MAFUNZO ELEKEZI KWA VIONGOZI NA WATENDAJI WAKUU WA SERIKALI TAREHE 9 MEI, 2011 KATIKA UKUMBI WA ST. GASPAR - DODOMA Mheshimiwa Waziri Mkuu; Mheshimiwa Jaji Mkuu; Wazee Wetu, Mzee Cleopa Msuya na Mzee Pius Msekwa; Ndugu Mawaziri; Ndugu Naibu Mawaziri; Ndugu Makatibu Wakuu; Ndugu Naibu Makatibu Wakuu; Wakuu wa Vyombo vya Dola; Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana: Ukaribisho Nianze kwa kuwakaribisha nyote kwenye Semina Elekezi inayojumuisha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu. Kama lilivyo jina lake, Semina hii ni ya kuelekezana juu ya namna tutakavyotimiza majukumu yetu katika Serikali. Tulikuwa na Semina kama hii mwaka 2006. Imetusaidia kupata mafanikio tuliyoyapata miaka mitano iliyopita. Naamini na Semina hii itatusaidia kupata ufanisi tunaoutarajia na ambao wananchi wanautarajia kutoka kwetu. Ndugu Viongozi na Watendaji wa Serikali; Niruhusuni niombe radhi kwa niaba ya Viongozi Wakuu wawili kutokuwa nasi siku ya leo. Wa kwanza ni Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal na wa pili ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein. Makamu wa Rais yuko Uturuki kuniwakilisha katika LDC Summit. Mwanzoni nilikubali kushiriki kwenye LDC Summit, lakini baada ya tarehe za Semina yetu kubadilika na kuangukia kwenye tarehe za Mkutano huo nikawa sina namna ila kutuma mwakilishi. Kwa uzito wa mkutano wenyewe na matumaini ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na wenyeji wetu kuhusu ushiriki wa Tanzania nikaona Makamu wa Rais atuwakilishe. Makamu wa Rais amefuatana na Mheshimiwa Prof. Anna Tibaijuka, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim. Najua watakosa uhondo, lakini tutawapatia DVD ya Semina wataona na kusikia tuliyozungumza. Mheshimiwa Rais wa Zanzibar amebanwa na vikao vya maandalizi ya bajeti. Madhumuni ya Semina Ndugu Viongozi, Katika Semina hii majukumu ya msingi ya Serikali ya utawala, maendeleo na ulinzi na usalama yatafafanuliwa. Pia itaelezwa jinsi kila mmoja wetu anavyohusika nayo na anavyotegemewa kutimiza wajibu wake. Katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge nilitaja malengo 13 ambayo yamejumuisha mambo makuu tutakayoyapa kipaumbele katika Serikali katika miaka mitano hii. Lakini nilikumbusha kuwa yale mambo 13 ni muhtasari wa maelekezo yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Ndugu Mawaziri; Mtakumbuka kuwa katika mkutano wangu wa kwanza nanyi niliwasisitizia umuhimu wa Ilani ya Uchaguzi kwa kila mmoja wenu na kwa Serikali yetu kwa jumla. Niliwaambia kuwa Ilani ndiyo mkataba mkuu baina ya Chama cha Mapinduzi na wananchi. Utekelezaji wake ndicho kipimo kikuu cha uwezo wetu wa kuongoza, mwaka 2015. Niliwataka kila mmoja wenu atambue ukweli huo na kutengeneza mkakati wa kutekekeleza Ilani kwa yale mambo yanayohusu Wizara yake. Sina shaka kuwa takriban miezi mitano baadae kila mmoja wetu atakuwa amekamilisha kazi hiyo na kuingiza katika mipango ya kazi ya Wizara itakayotekelezwa kuanzia bajeti itakayowasilishwa Bungeni mwezi ujao. Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu; Siku ile pia nilisisitiza jambo kwa Mawaziri ambalo napenda kulirudia tena leo kwani linawahusu na Makatibu Wakuu. Ninyi kwa pamoja, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu ndiyo timu moja ya uongozi na utawala katika Wizara. Kama viongozi mnategemewa kuonyesha njia kuhusu nini cha kufanya kutekeleza majukumu ya Wizara nilizowakabidhi kuziongoza. Katika jukumu lenu la utawala mnategemewa kuwa makini na mahiri katika kutumia rasilimali watu, vifaa na fedha za umma mlizokabidhiwa katika kutekeleza majukumu yenu. Mnategemewa kuwa na mipango na mikakati thabiti ya kutekeleza majukumu hayo. Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu; Katika Wizara kila kitu huanzia na kuishia kwenu. Hakuna mwingine tena kuliko nyie isipokuwa mamlaka zilizo juu yenu; yaani Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais. Kwa sababu hiyo, ili muweze kutimiza kwa ukamilifu wajibu wenu huo hamna budi kwanza kabisa kutambua vyema majukumu yenu na jinsi ya kuyatekeleza. Semina hii ina shabaha ya kusaidia katika hilo. Lakini, njia kubwa zaidi ni ile niliyowaambia siku ile, yaani ninyi wenyewe kufanya bidii ya kujua kwa kusoma, kuona na kufanya shughuli za Wizara zenu kwa makini. Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu mnatakiwa kuyajua kwa kina mambo yote yanayohusu Wizara mnazoziongoza. Vinginevyo hamtaongoza vizuri. Mtakuwa wababaishaji. Mtashindwa kutoa malengo maana mtakuwa hamjui nini cha kuekeleza, mtashindwa kusimamia mambo, kwa vile hamjui cha kusimamia, mtakuwa hamuonekani mkifanya chochote cha maana kwa sababu hamna jambo la kufanya zaidi ya mambo ya kawaida – routine issues. Mawaziri na Makatibu Wakuu lazima mtoke. Hiyo ndiyo njia bora zaidi ya kujua mambo yahusuyo Wizara yenu na ndiyo njia bora ya kuongoza: kuona wenyewe na kutenda. Itawafanya mjiamini kuelekeza na pia mnaposimama mbele za watu na kusema. Msiwe mangimeza. Tokeni, tembeeni kuona shughuli zenu. Tembeleeni wananchi muwafahamu, wawafahamu, mjue shida zao muwatatulie. Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu; Ili mjue mambo ya Wizara zenu vizuri lazima mtengeneze utaratibu mzuri wa kupashana habari kuhusu mambo yanayotokea Wizarani. Utaratibu utakaomwezesha kila mmoja kujua kinachoendelea Wizarani. Msipofanya hivyo kuna hatari ya ninyi wenyewe viongozi wakuu mkawa hamjiamini na hata kuwa na kauli tofauti kwa jambo hilo hilo. Mmoja anasema hivi na mwingine anasema vile. Kuna hatari ya kuzuka kutokuelewana miongoni mwenu. Hii pia ni muhimu sana hasa kwa sababu barua huandikwa kwa Waziri au Katibu Mkuu. Msipotengeneza utaratibu wa kupashana habari Waziri anaweza asijue anachojua Katibu Mkuu na kinyume chake. Na, baya zaidi Naibu Waziri na Naibu Katibu Mkuu wanaweza kuwa gizani kabisa. Naibu Waziri hushikilia Wizara anaposafiri Waziri na ndiye msemaji wa Wizara katika Bunge asipoyajua vyema yanayotokea au mambo yanayohusu Wizara hatakuwa msemaji mzuri na wa kujiamini wa Wizara. Naibu Katibu Mkuu hushikilia ofisi ya Katibu Mkuu anapokuwa hayupo. Hatafanya kazi kwa kujiamini na atashindwa kuamua mambo kwa sababu hana habari ya mambo yanayohusu Wizara. Mambo yatakawia na mengine kukwama kwa sababu hiyo. Pamoja na kutoa fursa kwa kila mmoja wenu kuona na kujua kinachotokea Wizarani, jengeni utaratibu wa kukutana mara kwa mara kuzungumzia shughuli za Wizara zenu. Itasaidia sana. Ndiyo maana Jeshini kuna Officers Mess kutoa fursa ya maofisa kufahamiana na kuzungumza masuala yahusuyo shughuli zao. Mnaweza kuwa na vikao vya mara kwa mara au hata kunywa chai pamoja. Hata nyie mnaweza kuwa na utaratibu kama huo. Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu; Narudia kuwakumbusha kwamba msingi wa utendaji Serikalini ni katiba, sheria, kanuni na taratibu. Ni muhimu kwenu kama viongozi mkajielimisha juu ya Katiba, sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinazoongoza utendaji kazi katika sehemu zenu za kazi. Uhalali wa maamuzi mtakayoyafanya hupimwa na sheria. Ukifanya maamuzi yanayokinzana na sheria utahojiwa wewe binafsi lakini pia utaibebesha Serikali mzigo wa hasara na fedheha itakayotokana na maamuzi hayo. Lakini pia maamuzi yasiyofuata sheria yanaweza kuwa na madhara kwa wananchi. Heshimuni Katiba na fuateni sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika utekelezaji wa majukumu yenu. Katika semina hii masuala hayo yatafafanuliwa na kuzungumzwa. Kadhalika uhusiano wa Serikali na mihimili mingine ya dola yani Bunge na Mahakama utafafanuliwa. Uwajibikaji wa Pamoja Viongozi Wenzangu; Wakati wote sisi sote tunapaswa kuzingatia kwamba Wizara ni moja, Serikali ni moja, lengo letu ni moja na hivyo wakati wote lazima tuwe na umoja, mshikamano na kauli moja. Serikali au Wizara isiyokuwa na umoja haiwezi kutimiza wajibu wake ipasavyo. Mawaziri na Makatibu Wakuu wasiokuwa na umoja hawatatimiza wajibu wao ipasavyo. Umoja ni kitu cha msingi sana. Unapokosekana kunakuwepo mifarakano na hatimaye huingia udhaifu katika kuamua na kutenda. Hali hiyo itasababisha wananchi kutohudumiwa ipasavyo na maendeleo yao kuathirika. Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu; Hakikisheni kuwa katika Wizara zenu kuna umoja. Umoja huo uanzie kwenu nyinyi viongozi wakuu. Aghalabu ninyi mkiwa na umoja Wizara huwa na umoja, ninyi mkifarakana wafanyakazi nao hugawanyika. Kwa upande wa Serikali nako hali kadhalika, lazima Mawaziri wawe na umoja. Iwapo Mawaziri wana umoja, Serikali huwa na mshikamano na nguvu katika kuamua na kutenda. Wakati wote tuhakikishe kuwa tuna umoja na mshikamano miongini mwetu. Tuepuke kauli na matendo yatakayofarakanisha Mawaziri na hivyo kuleta mgawanyiko katika Serikali. Lazima tukumbuke na kuzingatia dhana ya uwajibikaji wa pamoja. Lazima idhihirike katika ngazi ya Wizara na Serikali kwa jumla. Mawaziri, ninyi ndiyo viongozi wakuu katika Wizara zenu na Makatibu Wakuu ndiyo watendaji wakuu wa Wizara. Nyote mnawajibika katika nafasi zenu kwa maamuzi mnayoyafanya ya kisera na kiutendaji. Hamna budi kushirikiana, kushauriana na kuwekeana staha. Viongozi na watendaji wakuu wa Wizara hamna budi kujenga mahusiano mazuri na uwajibikaji wa pamoja. Haifurahishi kuona Waziri na Katibu Mkuu, au Waziri na Naibu Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu au Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu hawaelewani. Wanasemana na hata wakipingana hadharani, yaani mbele za wafanyakazi. Na baya zaidi pale wanapingana katika vyombo vya habari kuhusu maamuzi au utendaji wa Wizara au Serikali kwa ujumla. Hayo si maadili mema katika taasisi yoyote. Uzoefu unaonesha kuwa jambo hili hutokea pale ambapo kunakuwa na kuingiliana katika majukumu au
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages10 Page
-
File Size-