1458123221-Hs-15-26
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA __________ MAJADILIANO YA BUNGE __________ MKUTANO WA KUMI NA TANO Kikao cha Ishirini na Sita – Tarehe 4 Juni, 2014 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE: MWIGULU L. M. MCHEMBA): Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MHE. ESTHER L. M. MIDIMU (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA UCHUMI, VIWANDA NA BIASHARA): Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MHE.CHRISTINA M. LISSU (K.n.y. MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KWA WIZARA YA FEDHA): Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, kwa Wizara ya Fedha Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MASWALI NA MAJIBU NAIBU SPIKA: Swali letu la kwanza kama ilivyo ada linaelekezwa Ofisi ya Waziri Mkuu na linaulizwa na Mheshimiwa Agripina Zaituni Buyogera, Mbunge wa Kasulu Vijijini. Kwa niaba yake Mheshimiwa Rajab Mbarouk Mohammed. Na. 182 Uwekezaji Kwenye Pori la Makere Kusini MHE. RAJAB MBAROUK MOHAMMED (K.n.y. MHE. AGRIPINA Z. BUYOGERA) aliuliza:- 1 Nakala ya Mtandao (Online Document) Licha ya kwamba kuna uwekezaji unaoendelea kwenye Pori la Makere Kusini (Kagera Nkanda) katika Jimbo la Kasulu Vijijini; bado kuna mambo ya kuhoji:- (a) Ushirikishwaji wa wananchi na wawakishi wao ukoje, hasa ikizingatiwa kuwa hata Mbunge wao hana taarifa sahihi juu ya uwekezaji huo? (b) Je, Halmashauri na Wananchi wanaozunguka eneo hilo la uwekezaji wananufaika vipi na eneo hilo? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ELIMU) alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agripina Zaituni Buyogera, Mbunge wa Kasulu Vijijini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna uwekezaji unaoendelea katika Pori la Makere Kusini. Wananchi wanashirikishwa kutoka mwanzo na mazungumzo kati ya mwekezaji (Mawalla Trust Ltd.) na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa njia ya vikao vya Kijiji, Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira na kwa kupitia Baraza la Madiwani. Kupitia vikao hivyo Serikali ya Kijiji na Wananchi waliridhia kutoa eneo hilo kwa Halmashauri ya Wilaya ili litumike kwa uwekezaji kwenye Mkutano Mkuu wa Kijiji cha Kagerankanda uliofanyika tarehe 25 Julai, 2011. Mkataba kati ya Mwekezaji, Mawala Trust Ltd. na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ulisainiwa mbele ye Baraza la Madiwani tarehe 5 Juni, 2012. (b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia mkataba uliowekwa kati ya Halmashauri ya Wilaya na Mwekezaji, Halmashauri na Wananchi wanaozunguka eneo hilo watanufaika kwa kupata mapato ya shilingi milioni 440 kwa mwaka kama kodi ya pango la ardhi kwa matumizi ya uhifadhi wa maliasili na kuendesha shughuli za utalii. Aidha, wananchi kupitia Serikali zao za vijiji watanufaika kwa kulipwa asilimia 25 ya kiasi kilicholipwa na Mwekezaji kwa Halmashauri ya Wilaya kila mwaka. Mheshimiwa Naibu Spika, Mwekezaji amewezesha wananchi kwa kuwapa mafunzo ya ufugaji bora wa Nyuki na kuwapatia zana bora za ufugaji nyuki kwa ajili ya kuyatunza mazingira na kuwaongezea kipato. Aidha, Mwekezaji alitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 32 kwa ajili ya upimaji wa Vijiji na kuandaa matumizi bora ya ardhi kwa vijiji viwili vya Kagerankanda na Mvinza ambavyo vinapakana na eneo la uwekezaji na wananchi wamepata ajira kwa kushirikishwa katika ngazi za doria na kulinda kambi za Watalii.(Makofi) MHE. RAJAB MBAROUK MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Wizara kwa maana ya Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) ina jukumu la kuzilea na kuzilinda Halmashauri zetu. Sasa ninataka kufahamu maoni ya Wizara kuhusiana na mkataba huu ambao Halmashauri hii imeingia na huyu Mwekezaji. Je, wao kama Wizara waliridhia? 2 Nakala ya Mtandao (Online Document) NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ELIMU): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rajab Mbarouk Mohammed, kama ifuatavyo:- Ni kweli kwamba tunapokuwa na shughuli za Uwekezaji popote katika ngazi zetu za vijiji kwa kupitia maeneo yaliyopo, hatua ya kwanza ni kuwashirikisha wananchi wenyewe, lakini mbili ni lazima Kamati zinazohusika ikiwemo Ward DC - Kamati ya Maendeleo ya Kata ambayo inamiliki kimoja kati ya vijiji hivyo. Pia Baraza la Madiwani likiisharidhia sasa Wizara tunakuwa tumeridhika kwa sababu hatua za msingi za kushirikisha wananchi zinakuwa zimepitiwa. Kwa hiyo, kwa hatua waliyoifikia na kwa kuwa pia tumeona kampuni inayowekeza imetoa tija kwa wananchi wa maeneo yale kwa kuwapeleka mafunzoni. Lakini pia kuwapa vifaa bora vya ufugaji unaopelekea pia kulinda msitu wetu. Mheshimiwa Naibu Spika, si hilo tu, mwekezaji yule ametoa mchango mkubwa sana; amejenga madarasa mawili pamoja na jengo la utawala kwenye Shule ya Sekondari ya Kiminya. Pia amejenga bweni la Wasichana katika shule ya Sekondari ya Makere, jambo ambalo kwa kweli na sisi tunaona kwamba, wanananchi wanapata tija. Kwa hiyo, sisi Wizara tumeridhia kwa uendeshaji huo, unless Wananchi sasa wanaleta malalamiko kwenye maeneo ambayo hayajakamilika. MHE. MOSES J. MACHALI:- Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa nimwulize Waziri swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu iliingia mkataba na Kampuni ya Mawalla Trust Ltd., lakini bahati mbaya aliyekuwa Mkurugenzi au Mmiliki wa Kampuni hii alifariki dunia na hatunaye. Ikatokea taarifa kwamba, mkataba waliokuwa wameingia Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu pamoja na Kampuni hii, ni kwamba kampuni ile ilipaswa kuwa inalipa zaidi ya shilingi milioni 440. Halmashauri ilipata kueleza kwamba, fedha hizo hazitalipwa kwa sababu mmiliki wa Kampuni hayupo. Nilikuwa naomba kupata kauli ya Serikali. Je, itakuwa tayari kufuatilia ili kubaini kama fedha hizi zililipwa au hazijalipwa kwa sababu kuna utata au misingi ya kifisadi ambayo imekuwa inafanywa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu? Je, Naibu Waziri yuko tayari kuweza kufuatilia na hatimaye aweze kutupa jibu ambalo pengine ni sahihi juu ya fedha hizi ziko wapi? NAIBU SPIKA: Majibu ya ombi hilo Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitsaa (TAMISEMI). NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ELIMU): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Moses Machali, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge ameeleza jambo ambalo linaendelea na sasa jambo hili kwetu ni jipya na kwa kuwa ameomba kufuatilia, ninataka nimuahidi kwamba, tutafuatilia na tutampatia taarifa Mheshimiwa Mbunge ili aweze pia kuwa na ufuatiliaji wa karibu katika jambo hili. Ahsante sana. (Makofi) NAIBU SPIKA: Swali la mwisho Mheshimiwa Keissy nilikuona. 3 Nakala ya Mtandao (Online Document) MHE. ALLY KEISSY MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Naibu Spika, ni mashamba mengi ya Wawekezaji ambao hawalipi kodi ya ardhi kwenye Vijiji husika au Halmashauri. Je, Serikali ina mpango gani kufuatilia wawekezaji ambao inawapa vibali wasilipe kodi ya ardhi kuzifidia Halmashauri zetu badala ya hao Wawekezaji ambao Serikali inawalea kisiasa? Mfano katika Wilaya ya Nkasi? (Makofi) NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ELIMU): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Keissy kama ifuatavyo:- Suala lolote la uwekezaji mahali popote kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu la msingi ni jambo ambalo kwanza ni lazima liridhiwe na eneo hilo. Lakini katika kuridhia kunakuwa na makubaliano, yale makubaliano ndiyo msingi wa uwepo wake. Kama jamii husika haikubaliani kati ya mambo ambayo wanataka yafanyike,hakuna nafasi ya Mwekezaji kuendelea kwenye eneo hilo, na sisi Serikali kazi yetu ni kulinda makubaliano yaliyowekwa kati ya Mwekezaji na Wananchi. Pale ambapo inaonekana wananchi hawajaridhia Serikali hatuwezi kuruhusu kuendelea tu kama Wananchi wa eneo hilo hawajaridhia. Tumeendelea kuhakikisha kwamba, maeneo yote ya uwekezaji yanatoa tija kwa wananchi wetu. (Makofi) NAIBU SPIKA: Nakushukuru sana. Sasa tuhamie swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini. Na. 183 Kujenga Upya Shule ya Msingi Kabungu MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:- Shule ya Msingi Kabungu ni ya muda mrefu toka enzi za mkoloni; shule hii ambayo ni chakavu sana iko pembeni sana na maeneo wanayoishi wananchi wa kijiji cha Kabungu. Je, Serikali iko tayari kujenga shule hii ili iendane na mazingira ya sasa? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ELIMU): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, Shule ya Msingi Kabungu ilijengwa tangu enzi za mkoloni mwaka 1949 katika eneo ambalo mwanzoni lilikuwa Makao Makuu ya Wilaya ya Mpanda. Aidha, baadhi ya wakazi walihama kutoka katika makazi yao ya asili kwenda katika makazi mapya ambayo ni mbali na shule hiyo. Halmashauri imeshauriwa kusimamia sheria inayodhibiti uanzishaji wa makazi holela ili kuondoa tatizo la watu kuishi mbali na miundombinu ya jamii