Majadiliano Ya Bunge ______
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA ISHIRINI Kikao cha Thelathini na Mbili – Tarehe 19 Juni, 2015 (Kikao Kilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tunaanza maswali na Ofisi ya Waziri Mkuu, swali la kwanza linaulizwa na Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, kwa niaba yake Mheshimiwa Dkt. Limbu. Na. 224 Mradi wa Kupandishwa Hadhi Barabara kuwa za Mkoa MHE. DKT. FESTUS B. LIMBU (K.n.y. MHE. DEO K. SANGA) aliuliza:- Tuliomba barabara ya kutoka Mtwango kupitia Kichiwa hadi Ikuna Nyombo, pia barabara ya kutoka Makambako-Mlowa-Manga-Usetuke- Kifumbe-Ibatu-Itandililo kuunganishwa na barabara ya Mgololo:- (a) Je, ni lini barabara hizo zitapandishwa hadhi kuwa za Mkoa? (b) Je, ni lini zitaanza kutengenezwa? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Njombe Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:- 1 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) (a) Mheshimiwa Spika, kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Njombe kilichofanyika tarehe 04 Juni, 2012, kilipendekeza barabara za kupandishwa hadhi kama ifuatavyo:- (i) Mtwanga-Kichiwa-Ikuna hadi Nyombo yenye kilomita 28.6; (ii) Makambako – Mlowa – Manga – Kifumba - Kichiwa hadi Kitandulilo yenye kilomita 35; (iii) Mfiliga – Ikangasi - Itambo hadi Idete yenye kilomita 65; na (iv) Makambako - Usetule hadi Kitandililo yenye kilomita 34. Mheshimiwa Spika, hapo tarehe 30 Julai, 2013, Mkuu wa Mkoa wa Njombe alimwandikia Waziri wa Ujenzi barua yenye Kumb.
[Show full text]