Hii Ni Nakala Ya Mtandao (Online Document)
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ______________ MAJADILIANO YA BUNGE _______________ MKUTANO WA NNE Kikao cha Hamsini na Tano – Tarehe 25 Agosti, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, napenda kutoa taarifa kwamba, ujumbe uliokwenda kushiriki maziko kwa ndugu yetu mpendwa sana, Mheshimiwa Silima, tulikwenda kwa usalama na mwenzetu amelazwa vizuri, kwa amani na upendo mkubwa sana. Watu wa kule wamefurahi kwamba, tumeweza kushirikiana nao vizuri. Kwa hiyo, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge, kwa kufanya maombolezo kwa ajili ya ndugu yetu. Roho yake ipumzike mahala pema peponi; Amin. HATI ZILIWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. GREGORY G. TEU): Taarifa ya Mwaka na Hesabu za The National Board of Accountants and Auditors – Tanzania kwa Mwaka wa Fedha 2009/2010 (The Annual Report and Accounts of the National Board of Accountants and Auditors – Tanzania for the Financial year 2009/2010). Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MWENYEKITI WA KAMATI YA FEDHA NA UCHUMI: Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Fedha kwa Mwaka 2010/2011 pamoja na Maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MHE. CHRISTINA L. MUGHWAI (K.n.y. MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KWA WIZARA YA FEDHA): Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani juu ya Wizara ya Fedha kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MASWALI KWA WAZIRI MKUU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, leo ni Siku ya Maswali kwa Waziri Mkuu; naomba maswali yawe yale ya kisera na siyo maswali ambayo yanakuwa siyo eneo lake hasa Waziri Mkuu. Kwa kuwa tunaye Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, yeye siku zote anaanza. Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Mbowe. MHE. FREEMAN A. MBOWE – KIONGOZI WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa sababu kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi kuhusiana na sakata la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini limeleta utata mkubwa katika Taifa; na kwa sababu Bunge lako jana liliridhia umuhimu wa kuunda Kamati ambayo itachunguza undani wa jambo hili; na kwa sababu Katibu Mkuu Kiongozi alimrudisha ofisini Ndugu Jairo; je, Serikali 1 haioni kuna umuhimu wa Bwana Jairo aendelee na likizo wakati Kamati Teule ya Bunge inafanya kazi yake? (Makofi) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, hatua hiyo tayari imeshachukuliwa na Rais. Ninachoweza kuliahidi Bunge lako ni kwamba, kwa sababu jambo hili limeundwa kwa mujibu wa utaratibu, Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha ili tuweze kubaini mazingira na mambo yote yanayoendana na yaliyojitokeza. (Makofi) MHE. FREEMAN A. MBOWE – KIONGOZI WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI: Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na majibu mazuri sana ambayo nakupongeza kwa kauli hiyo, ningependa tu kukumbusha kwamba, wakati Katibu Mkuu Kiongozi anatoa kauli ile, alizungumza jambo lingine ambalo nalo vilevile ni zito na lenye utata mkubwa; aliposema kwamba ni utamaduni wa kawaida wa Serikali kufanya hivyo; na wakati huo huo, kwa faida ya Bunge na Watanzania kwa ujumla, Wizara ya Waziri Mkuu ambayo ilikuwa na bajeti kubwa ambayo ilijadiliwa kwa siku tano, ilitumia jumla ya shilingi 174,545,000 kuwezesha bajeti kupita, wakati Wizara ya Nishati na Madini ilitumia shilingi 578,000,000; je, pamoja na kwamba Bunge litachunguza; Serikali itakuwa tayari kuwachukulia hatua za kinidhamu wale wote watakaokuwa wamehusika na ubadhirifu wa fedha za umma? Je, itatangazwa rasmi kwamba siyo Sera ya Serikali au tuchukue kauli ya Katibu Mkuu Kiongozi kwamba hiyo ni Sera na utaratibu wa kawaida wa Serikali? (Makofi) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, mimi nafikiri Mheshimiwa Mbowe, mengine haya tuiachie Kamati Teule, kwa sababu naamini kabisa katika eneo hili, wataweza pengine kugundua mambo mengine mengi ambayo yote yanaweza kuwa ni kwa maslahi ya nchi. Kwamba, ule ndiyo utaratibu, well, anaweza kuwa alikuwa ni sahihi kwa upande mmoja, lakini inawezekana vilevile siyo sahihi sana, inategemea zile fedha mmezitumia kwa ajili ya jambo gani. Kwa hiyo, kama zipo sababu ambazo zinaweza kuhalalishwa kwa maana kwamba, zimetumika kwa jambo ambalo wote tunaweza tukaona ni sawa, hakuna tatizo. Hofu hapa ni kwamba, inawezekana fedha hizo hazitumiki kwa nia njema, ndiyo maana kidogo linaleta hisia ambazo ni lazima kwa kweli wote turidhiane. MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa kuwa biashara ya dawa za kulevya ni biashara ambayo inaliathiri Taifa letu sana; na kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameliona hilo na akaunda Kikosi Kazi ambacho nafikiri Wabunge wote tunakubali kwamba kimefanya kazi nzuri sana; je, Mheshimiwa Waziri Mkuu, haoni kwamba kuna umuhimu sasa wa kuchukua hatua ya dharura ya kuwatafutia Kikosi Kazi kile jengo la kuhifadhi zile dawa za kulevya wanazokamata kuliko ambavyo sasa zimerundikana ofisini kwao na wakati mwingine zinapotea na wao kukosa ushahidi? WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza, nakubaliana na Mheshimiwa Anne Kilango kwamba, ile Task Force inafanya kazi nzuri sana. Hiyo ni dhahiri kabisa na Serikali inaridhika na kazi wanayoifanya. Vilevile ni kwamba, kikundi hiki kinakabiliwa na changamoto nyingi tu za kiutendaji ambazo ni dhahiri kabisa kwamba, kama Serikali lazima tukubali kutafuta suluhu ya matatizo yao. Kwa hiyo, hilo ulilolisema Mheshimiwa Mama Anne Kilango ni eneo moja kwa maana ya kuona ni namna gani tunaweza tukawasaidia kuwa na jengo la uhakika, hasa kwa sababu ya hifadhi ya zile exhibits ambazo wakati mwingine zinaleta utata kutokana na mlundikano uliopo pale. Mheshimiwa Spika, sisi tumekwishaanza kuliangalia na kimsingi ni kwa sababu lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa hiyo, kazi hiyo tumeshaanza kuifanya na Katibu Mkuu, kuona namna ya kuwasaidia katika eneo hilo. MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninashukuru kwamba, changamoto mmeshaziona. Changamoto kubwa ni kwamba; Kikosi Kazi kile kinafanya kazi eneo kubwa ambalo ni Tanzania nzima, lakini kina magari mawili tu na hakina mgawo maalum, hakina bajeti; je, Ofisi yako Mheshimiwa Waziri Mkuu haiwezi kutoa gari moja kutoka kwenye pool pamoja na Ofisi ya Rais ikatoa gari moja, wakaongezewa japo magari mawili ili wafanye kazi kwa urahisi zaidi? 2 WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, Kikosi Kazi kile ni kikundi kidogo sana, lakini makini sana. Kwa hiyo, Serikali tunajitahidi sana kukiwezesha kiweze kufanya kazi zake vizuri; ni Kikosi Kazi lakini kipo chini ya Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya. Kama nilivyosema, Rais alipoamua jambo hili ni kwa sababu alitaka sasa tuwe na kikundi ambacho kitajikita zaidi katika eneo hili ili tuweze kupambana vizuri zaidi, badala ya kuliacha liwe jambo la jumla. Kwa hiyo, nakubaliana kabisa na rai yako na ushauri wako; sisi tutafanya kila litakalowezekana kuhakikisha Kikosi Kazi hiki kinatimiza majukumu yake vizuri, ikiwa ni pamoja na kukipatia nyenzo hizo. Nadhani katika hili, hata Waheshimiwa Wabunge, hawatagombana na mimi na viposhoposho vya kuhakikisha wanafanya kazi yao vizuri. (Makofi) MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Wakulima wa Tanzania na mimi nikiwa mmojawapo, ninaomba kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Serikali imepiga marufuku kuuza mazao nje ya nchi; na wakulima kwa sasa hivi wanateseka kwa sababu wameshindwa kuuza mazao yao kwa vile wanunuzi wameacha kununua mazao na wale wanaonunua wananunua kwa bei ya chini sana kwa mfano; mbaazi, choroko, dengu, ngwala; ni mazao ambayo yote sasa hivi hayanunuliwi; sasa tunaomba Serikali itoe tamko kwamba inakuwaje kuhusu hayo mazao? Kama hairuhusiwi kuuzwa nje, je, Serikali ipo tayari kununua hayo mazao ili hao wakulima waweze kujiandaa kwa msimu ujao ambao umekwishafika? (Makofi) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, Tangazo la Serikali ambalo ndilo lilipiga marufuku uuzaji wa mazao nje ya nchi, halihusiani hata kidogo na mbaazi wala jamii ya mikunde ya namna yoyote. Ili kuondoa utata huu na sijui umetokana na nini, nadhani ni kwa sababu tu labda lile tangazo wengi hawajui linasema nini; tutaiagiza ofisi yetu, lile tangazo litoke kwenye gazeti ili watu wajue. Tulichokuwa tunalenga zaidi pale ilikuwa ni Zao la Mahindi. Kama inabidi tuongeze orodha zaidi, ni lazima lile tangazo tulirekebishe ili tuweze kuongeza mazao mengine. Vinginevyo, hauwezi ukakataza zao nje ya yale ambayo yamewekwa kwenye Tangazo la Serikali. (Makofi) MHE. SALUM K. BARWANY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali kwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa udini na ukabila ni vitu hatari sana katika jamii kwa wakati huu ambavyo kwa namna moja au nyingine vinaweza kutuharibia umoja wetu, mshikamano wetu na amani na utulivu uliokuwepo katika Taifa hili. Kwa muda mrefu sasa jamii ya watu wenye imani ya Uislam wanatoa kauli zao hadharani katika vyombo vya habari na katika machapisho mbalimbali kwamba ndani ya Mfumo wa Utawala kwa sasa kuna udini dhidi yao; je, Serikali inasema nini juu ya hoja hiyo? WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza, nataka nikubaliane kabisa na Mheshimiwa Barwany kwamba, sisi kama Taifa, Katiba inatuasa kama Wananchi wa Tanzania tusiwe na tabia au mwelekeo wowote ule wa kubaguana ama kwa misingi ya dini au makabila yetu au rangi zetu au jinsia au namna nyingine yoyote. Hivyo ndivyo Katiba inavyosema. Kwa hiyo, kwa mtu yeyote ambaye anafanya jambo lolote