30 APRILI 2019.Pmd
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA KUMI NA TANO Kikao cha Kumi na Nane – Tarehe 30 Aprili, 2019 (Bunge lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Mussa A. Zungu) Alisoma Dua MWENYEKITI: Tukae. Katibu. NDG. RAMADHANI ISSA ABDALLAH – KATIBU MEZANI: HATI ZA KUWASILISHA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA MAJI: Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2019/2020. MWENYEKITI: Ahsante, Katibu. NDG. RAMADHANI ISSA ABDALLAH – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU MWENYEKITI: Maswali, tunaanza Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Anna Richard Lupembe. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Na. 146 Ukarabati wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mpanda MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakarabati Shule ya Sekondari ya Mpanda Girls? MWEYEKITI: Mheshimiwa Waziri. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kufanya ukarabati wa Shule za Sekondari Kongwe nchini kwa awamu kulingana na hali ya upatikanaji wa fedha. Katika Awamu ya kwanza, Serikali imekarabati shule za sekondari 53 kwa gharama ya shilingi bilioni 53.6 ikijumuisha ujenzi wa Shule za Sekondari za Nyakato na Ihungo. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Awamu ya pili Serikali imepanga kukarabati shule 17 kongwe za Sekondari nchini ikiwemo Shule ya Sekondari ya Wasichana Mpanda. Jumla ya shilingi bilioni 16 zimetengwa kukarabati shule hizo. Miongoni mwa fedha hizo shilingi milioni 986 zimetengwa kwa ajili ya Shule ya Wasichana ya Mpanda. Ahsante. MWENYEKITI: Mheshimiwa Lupembe. MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Shule hii ni kongwe halafu iko kwenye eneo ambalo ni hatarishi, kuna bwawa ambalo lina wanyama wakali ambao wanaingia katika eneo la shule kwa sababu 2 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) shule hii haina uzio kabisa; na shule hii ina upungufu mkubwa sana wa madarasa na vilevile ina upungufu wa mabweni; na kwa kuwa Serikali imepanga fedha na imesema hapa kuwa imeji-commit na pesa tayari zipo; sasa naomba commitment, ni lini Serikali itakarabati shule hii kwa sababu wanafunzi wa shule hii wanapata taabu sana? Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, shule hii ina wasichana takribani watoto 888, ni watoto wa kike ambao wanapata shida sana; usiku wakiugua hakuna gari katika shule hii: kwa kuwa hii shule ni kongwe, ni lini Serikali itatuletea gari katika shule hii ya Sekondari ya Mpanda Girls? MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri majibu. Jiandae Mheshimiwa Kapufi. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi ni kwamba zimetengwa fedha shilingi bilioni 16 kwa ajili ya kukarabati shule nyingine mwaka huu wa fedha na commitment ya Serikali ni kwamba ukarabati huu unaanza mara tu tutakapoanza kutekeleza bajeti ya mwaka 2019/ 2020. Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ametoa hoja ya gari na ni kweli kwamba kwa shule hizi kongwe na kutokana na mazingira ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge, naomba tupokee ombi hili tutalifanyia kazi kwa kadri uwezo wa Serikali utapopatikana. MWENYEKITI: Mheshimiwa Kapufi, Mheshimiwa Mwanne, Mheshimiwa Mwakasaka na Mheshimiwa Nape. MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nikirejea hapo katika Shule ya Wasichana ya Mpanda kimechimbwa kisima kirefu, tatizo lililobaki ni ufungaji wa pump na ukizingatia ni shule ambayo ina watoto wa kike peke yake. 3 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Ni lini Serikali itakamilisha suala la ufungaji wa pump kwenye shule hii? (Makofi) MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Waziri kwa kifupi. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tunapokarabati hizi shule kwanza tunaangalia mfumo wa majengo, mabweni, bwalo, madarsa, Ofisi, majengo ya utawala, mfumo pia wa maji na mfumo wa umeme. Kwa hiyo, kama alivyozungumza kwamba kuna kisima ambacho kimechimbwa katika eneo hilo, wakati wa ukarabati litaangaliwa. Tutatenga fedha kwa ajili ya kupata maji katika eneo hilo. Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuwa na wanafunzi wengi katika shule hii kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba ni zaidi ya wanafunzi 800, watoto wa kike, halafu kusiwe na huduma ya maji. Ahsante. MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwanne. MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa matatizo ya ukarabati katika shule za sekondari yanafanana na shule za msingi, Mkoa wa Tabora katika Manispaa ya Tabora, Shule ya Kanyenye iliezuliwa karibuni madarasa manne tangu mwaka 2018 Machi, mpaka leo haijafanyiwa ukarabati, wanafunzi wanapata taabu. Nini kauli ya Serikali kwa leo? MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, kwa kifupi. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nipokee maombi na maelekezo ya Mheshimiwa Mbunge tutayafanyia kazi. Mpaka Bunge lijalo tutakuwa tumepata majibu ya tatizo hili katika eneo la Tabora. Ahsante. 4 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwakasaka. MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Shule ya wasichana ya Tabora (Tabora Girls) ni shule kongwe sana hapa nchini ambayo pia ina vipaji maalumu. Shule hii kwa muda mrefu imetelekezwa kuhusu uzio. Ile shule haina uzio kabisa kwa miaka mingi na tayari juhudi za viongozi mbalimbali nikiwemo mimi mwenyewe tumeshaanza mkakati wa kujenga uzio huo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutusaidia katika kukamilisha uzio huo wa Shule ya Wasichana Tabora? MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri majibu kwa kifupi. Jiandae Mheshimiwa Nape. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namwomba Mheshimiwa Mbunge tuonane tuone. Kama wananchi wameanza kujitolea na wadau mbalimbali akiwepo Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri ya wananchi wake anaowawakilisha hapa Bungeni, basi tuonane tuone ni changamoto gani zilizopo na sehemu gani ya kuweza kusaidia kumalizia uzio huo. MWENYEKITI: Mheshimiwa Nape. MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami naulize swali dogo la nyongeza. Katika jitihada za kuboresha miundombinu ya elimu Mkoani Lindi, kwa misimu miwili, mitatu iliyopita tulikubaliana kukata fedha kutokana na malipo ya korosho ya shilingi 30/= kwa kila kilo ili kukarabati miundombinu na kujenga miundombinu mipya. Sasa iko miundombninu ambayo ilianza kujengwa kwa sababu ya hali ambayo sote tunaijua, miundombinu hiyo sasa imesimama kwa sababu hiyo fedha haikupatikana. 5 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Je, Serikali iko tayari kusaidia kumalizia miundombinu hii katika Mkoa wa Lindi hasa upande wa elimu? (Makofi) MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nia ya Serikali kuendelea kukamilisha miundombinu ya elimu na hasa ile ambayo imeanzishwa na wananchi na ndiyo maana tumepeleka fedha za kiutawala mwezi Januari, tumepeleka fedha za maboma karibu shilingi bilioni 29.9. Kwenye bajeti hii ambayo imepitishwa, zaidi ya shilingi bilioni 90 inaenda kusimamia miundombinu ya elimu. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipokee maombi ya Mheshimiwa Mbunge, tutazingatia maoni yake. Ahsante. MWENYEKITI: Ahsante kwa majibu mazuri, tunaendelea na Wizara ya Nishati, Mheshimiwa Rashid Akbar. Na.147 Matumizi ya Gesi Inayotoka Mtwara na Songosongo MHE. AJALI R. AKBAR aliuliza:- Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa gesi kutoka Mtwara na Songosongo inatumika kwa asilimia sita tu:- (a) Je, kwa nini Kiwanda cha Saruji cha Dangote na Mtwara Cement Mkoani Mtwara havijapatiwa umeme wa gesi asilia hadi leo? (b) Je, kwa nini Wananchi wa Mtwara wasiunganishiwe gesi asilia kwenye nyumba zao? NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Ajali 6 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Akbar, Mbunge wa Newala Vijiji, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kiwanda cha Saruji cha Dangote kimeunganishwa na miundombinu ya gesi asilia ambapo awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa kuwezesha matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme kwa ajili ya kiwanda cha Dongote ilikamilika na kuanza kufanya kazi mwezi Agosti, 2018. Aidha, hadi kufikia Mwezi Aprili, 2019 kiwanda cha Dangote kimeanza kutumia wastani wa futi za ujazo milioni tano kwa siku kwa kuzalisha umeme. Awamu ya pili ya mradi ilikamilika mwezi, Desemba, 2018 na sasa kiwanda cha Dangote kinatumia gesi ya wastani wa futi za ujazo milioni 15 hadi milioni 20 kwa siku kwa ajili ya uzalishaji wa Saruji. Jumla ya gharama za mradi ni shilingi bilioni 8,200. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa TPDC inaendelea na utekelezaji wa mradi kwa kuagiza na kujenga miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia majumbani, viwandani na katika Taasisi mbalimbali kwa Mikoa ya Mtwara, Pwani na Dar es Salaam. Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa kusambaza gesi asilia Mkoani Mtwara imeshaanza ambapo kwa sasa kazi ya ununuzi wa vifaa, mabomba, mita za kupimia gesi pamoja na vifaa vya kupunguza mgandamizo