Tarehe 22 Juni, 2017
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________ MKUTANO WA SABA Kikao cha Hamsini na Tatu – Tarehe 22 Juni, 2017 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Dkt. Tulia Ackson) Alisoma Dua NAIBU SPIKA: Tukae. Katibu. NDG. THEONEST RUHILABAKE – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tutaanza na Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, sasa aulize swali lake. Kwa niaba yake, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile. Na. 437 Sheria ya Kuwalinda wafanyakazi wa Mahotelini na Majumbani MHE. FAUSTINE E. NDUGULILE (K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI) aliuliza:- Sheria ya kuwalinda wafanyakazi wa mahotelini na majumbani imekwama kutungwa Zanzibar na Tanzania Bara kutokana na Azimio lililofikiwa na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) kutoridhiwa na Bunge tangu Mkataba kusainiwa mwaka 2011, mkataba ambao unataka kila nchi 1 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) mwanachama kuwa na Sheria ya kulinda haki za wafanyakazi hao:- (a) Je, ni sababu zipi zinazosababisha azimio hilo kutowasilishwa Bungeni tangu Tanzania iliposaini Azimio la ILO wakati nchi nyingine zimeanza utekelezaji wake zikiwemo za Afrika Mashariki? (b) Kwa kuwa Zanzibar haiwezi kutunga Sheria zake za kulinda haki za wafanyakazi wa mahotelini na majumbani mpaka azimio hilo lipelekwe na Ofisi yako Bungeni na kuridhiwa ndiyo kila upande utunge Sheria zake kutokana na mambo ya kazi kuwa sio ya Muungano: Je, ni lini Bunge litapokea azimio hilo la kulinda haki za wafanyakazi hao? (c) Je, Serikali inawaeleza nini Vyama vya Wafanyakazi wa Mahotelini na Majumbani ambao walianza kufanya matayarisho ya utekelezaji wa azimio hilo, lakini wamekwama kutokana na mkataba huo kutoridhiwa na Bunge tangu kuafikiwa? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa mwaka 2011, nchi wanachama wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ikiwemo Tanzania, zilipitisha Mkataba wa Kimataifa kuhusu kazi za staha kwa wafanyakazi wa majumbani (Convention No.189 on Decent Work for Domestic Workers). Hadi sasa nchi zilizoridhia mkataba huu ni 23 kati ya nchi wanachama 189. Kwa upande wa Afrika ni nchi mbili tu zilizoridhia ambazo ni Afrika Kusini na Mauritius. Serikali inaendelea kupitia kwa makini sana maudhui ya mkataba huo ili kufanya maandalizi ya kuuridhia. 2 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya kazi na ajira siyo ya Muungano. Tanzania ina Sheria za Kazi, hali kadhalika na Zanzibar pia wana Sheria za Kazi ambazo zinawahusu wafanyakazi wote wakiwemo wafanyakazi wa mahotelini na majumbani. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nchi yetu inazo sheria mbalimbali zinazotambua na kusimamia maslahi ya wafanyakazi nchini, wakiwemo wafanyakazi wa majumbani, wafanyakazi na vyama vyao waendelee kutambua juhudi za Serikali na kulinda na kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi kupitia sheria, kanuni na taratibu tulizonazo. Serikali itaendelea kuelimisha jamii na wadau mbalimbali kuhusu mifumo, maudhui na taratibu za uridhiaji wa mikataba ili kufanya maandalizi stahiki kabla ya uridhiaji wa mikataba hiyo. NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, swali la nyongeza. MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nimesikiliza kwa makini sana majibu ya Mheshimiwa Naibu Wazir; swali langu la kwanza: Je, ni lini sasa Serikali italeta azimio hilo Bungeni kuweza kupitishwa? Maana amesema kwamba ni nchi mbili tu ambazo zimepitisha. Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; sisi Tanzania tuna Sheria ya Kazi nadhani ya mwaka 2004. Je, ni lini sasa kulingana na mazingira ya sasa mtaileta tena ili iweze kufanyiwa mapitio? NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, majibu. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza ameuliza, ni lini? Katika majibu yangu ya msingi, nimesema Serikali bado tunaendelea kupitia maudhui ya 3 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) mkataba huu ili baadaye baada ya kujiridhisha tuweze kuuleta kwa ajili ya kuwa ratified. Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Convention hii namba 189; katika utaratibu wa hizi Conventions huwa pia wanatoa vitu vinaitwa recommendation. Katika Convention hii kuna recommendation namba 201 ambayo inatoa mazingira ya nchi zile wanachama kuona namna bora ya kuweza kuandaa baadhi ya mechanism ili mikataba hii iweze kuridhiwa. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mambo mengi ambayo yapo katika mkataba huu tayari yapo ndani ya sheria zetu. Ukiangalia katika article ya kuanzia 13 mpaka 18 imezungumza kuhusu masuala ya Freedom of Association, masuala ya mikataba ambayo kwa mujibu wa sheria zetu, tayari yako covered. Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda katika nchi kama Kenya, ziko baadhi ya Conventions ambazo hawajazi-ratify kwa sababu wanaona sheria yao ni nzuri zaidi kuliko ile mikataba. Kwa hiyo, nasi bado tunaona kabisa kwamba yako maeneo mengi sana ambayo sheria yetu ime-cover. Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni mapitio ya sheria. Kwa mujibu wa utaratibu wa masuala ya kazi, sisi tunafanya kazi katika mfumo ambao tunaita ni tripartism kwamba ni Serikali, Waajiri na Wafanyakazi. Inapotokea kwamba kuna jambo lolote ambalo linahitaji marekebisho au mapitio ya sheria, wadau huwa wanafanya taratibu hizo. Nasi kama Serikali mara zote tumekuwa flexible kuhakikisha kwamba sheria zetu za Kazi zinakuwa intact ili ziwe msimamizi mzuri katika masuala ya kazi katika nchi yetu. NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Roman Selasini. MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na kusubiri mapitio ya huo mkataba, lakini hapa nchini pana vikundi mbalimbali vya watu vinawakusanya watoto wetu wa nchi hii kwa minajili 4 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) ya kuwatafutia kazi za ndani nchi za nje. Habari tulizonazo ni kwamba baadhi ya hawa watoto wamekuwa wakinyanyasika, wakiteswa na hata kuuawa. Je, ni hatua zipi za wazi ambazo Serikali inazichukua kwa ajili ya kudhibiti vikundi hivi? NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, majibu. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge hapa alikuwa anazungumzia wale mawakala wa ajira ambao kwa namna moja ama nyingine, yamekuwepo malalamiko mengi sana ya kuwapeleka mabinti zetu katika nchi hasa za Uarabuni kwenda kufanya kazi za ndani. Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu alishatoa agizo na tangazo la kwamba wale wote ambao wanakwenda kufanya kazi nje ya nchi wapitie mfumo ambao upo katika Wizara yetu kupitia Wakala wa Ajira wa Serikali ambaye ni TAESA. Sasa tukibaini kwamba wako watu ambao wanafanya kazi hii kinyume na taratibu, sheria zetu ziko wazi, huwa tunawafutia usajili. Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tumekuwa tukiwachukulia hatua kuhakikisha kwamba hawapati tena registration ili tuhakikishe kwamba nguvu kazi yetu hii wakienda kufanya kazi nje ya nchi tuwe tumewalinda kwa maana ya haki zao za kimsingi, tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo wako baadhi ya Watanzania ambao hawapitii katika Ofisi yetu na wakienda nje ya nchi wakipata manyanyaso tunakuwa hatuna taarifa. Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hata Balozi zetu zimeweka utaratibu mzuri; ile mikataba inayotolewa pale, mwajiri yeyote wa nje ya nchi ambaye anamtaka mfanyakazi wa Tanzania lazima apitie katika Ubalozi na Ubalozi unawasiliana nasi kwa ajili ya kuandaa mikataba ili tumlinde na tulinde haki za mfanyakazi wa Kitanzania. 5 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, sasa aulize swali lake. Na. 438 Kuboresha Maslahi ya Walimu Nchini MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:- Serikali imekuwa na dhamira ya dhati ya kuboresha maslahi ya Watumishi hususan Walimu kwa kutoa nyaraka mbalimbali ikiwemo Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa tarehe 20/10/2014 unaohusu mishahara na Posho ya Madaraka kwa Viongozi wa elimu (Responsibility Allowance):- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kutekeleza waraka huo? (b) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa Posho ya Kufundishia (Teaching Allowance) ili kuleta ufanisi wa kazi? NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Serikali ilianza kutekeleza Waraka Na. 3 wa mwaka 2014 tangu tarehe 1 Julai, 2016 kuhusu Posho ya Madaraka kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu wa Elimu Kata. Walimu Wakuu wanalipwa sh.200,000/= kila mwezi na Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata wanalipwa sh.250,000/= kila mwezi. Kwa mwezi mmoja, Serikali inatumia takriban shilingi bilioni 5.01 kwa ajili ya kulipa Posho za Madaraka kwa viongozi hao kwa ajili ya kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimu. 6 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) (b) Mheshimiwa Naibu Spika, posho ya kufundishia ilijumuishwa katika Mshahara wa Walimu ili kuboresha maslahi ya Walimu wanapostaafu. Hata hivyo, Serikali hivi sasa kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora inafanya mapitio ya kazi kwa watumishi wote nchini ili kuboresha maslahi kwa kuzingatia uzito wa kazi. NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mussa Sima, swali