MKUTANO WA KUMI NA MOJA Kikao Cha Sitini – Tarehe 28 Juni, 2
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________ MKUTANO WA KUMI NA MOJA Kikao cha Sitini – Tarehe 28 Juni, 2018 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Andrew J. Chenge) Alisoma Dua MWENYEKITI: Waheshimiwa tukae. Tunaanza Kikao chetu cha Sitini. Katibu. NDG. BAKARI KISHOMA – KATIBU MEZANI: HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Hati ya Uhamishaji Fedha Na. 1 ya Mwaka 2017/2018 (Statement of Reallocation Warrant No. 1 of 2017/2018). Hati ya Uhamishaji Fedha Na. 2 ya Mwaka 2017/2018 (Statement of Reallocation Warrant No. 2 of 2017/2018). MWENYEKITI: Ahsante. Katibu. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) NDG. BAKARI KISHOMA – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU MWENYEKITI: Maswali. Swali letu la kwanza kwa leo linaulizwa na Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini. Na. 505 Mgao wa Fedha za Barabara MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:- Hali ya barabara zinazosimamiwa na halmashauri ni mbaya sana kutokana na fedha zinazotolewa na Mfuko wa Barabara kukaa kwa muda mrefu na hali ya kuongezeka kwa magari binafsi na yale ya biashara ambapo kila tarafa ina zaidi ya magari 20 na hivyo, kufanya barabara hizo kuharibika na kuwa vigumu kupitika nyakati za masika:- (a) Je, Serikali haioni haja ya kuleta mapendekezo mapya ya mgao wa fedha za barabara? (b) Barabara nyingi za Halmashauri ya Mji wa Mbulu zimejifunga katika Tarafa za Nambis na Daudi. Je, kwa nini wataalam kutoka Wizarani wasifike kuzikagua na kutoa ushauri stahili? (c) Je, kwa nini BQ za tenda za barabara ngazi ya mkoa zisiwekwe kwenye kitabu cha RRB, ili Waheshimiwa Wabunge na wananchi wafahamu shughuli zitakazofanywa na makandarasi waliopewa kazi? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, naomba kujibu swali la 2 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye Sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kufanya tathmini ya mtandao wa barabara nchi nzima ili hatimaye utumike kuangalia kwa kina utaratibu mzuri zaidi wa mgawo wa fedha za barabara kati ya TANROADS inayoshughulikia barabara kuu na barabara za mikoa na TARURA inayoshughulikia barabara za Mamlaka za Serikali za Mitaa. (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2017/2018 Barabara za Mji wa Mbulu zilitengewa shilingi milioni 814.56. Kati ya hizo shilingi milioni 262.12 zilitengwa kwa ajili ya barabara kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum (Periodic Maintenance) Barabara za Ayamaame – Kainam – Hhasama – Mbulu – Endagikot – Tlawi, Tango FDC, Waama – Masieda, Ayayumba – Hhayloto zenye urefu wa kilometa 35.7 katika Tarafa za Daudi na Nambisi na kuweka changarawe katika Barabara za Ayamaami – Kainam – Hhasama, Mbulu – Kuta na Ayayumba - Hhayloto zenye urefu wa kilometa 8.13 Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuchonga barabara ya Uhama – Masieda – Hayayumba – Hailoto zenye urefu wa kilometa 31.5 na ujenzi wa kalavati za njia mbili zenye kipenyo cha milimita 900 katika Tarafa ya Daudi. Barabara zilizokuwa zimejifunga kwa kuharibika na mvua sasa zinapitika ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 95 na kazi inaendelea. Katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 Barabara za tarafa za Nambis na Daudi zimetengewa shilingi milioni 438.8 kwa ajili ya matengenezo. (c) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haki ya wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa na wananchi kupata taarifa za jumla za barabara zilizopangwa kujengwa katika mkoa, ikiwemo gharama za kazi ambazo wajumbe wanaweza kuzipata katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa. 3 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Issaay. MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa sababu swali hili lilikuwa la mwezi wa Pili mwaka huu. Hivi sasa ni kweli, barabara hizo nilizozitaja zimefanyiwa matengenezo, lakini kwa kuwa, sasa fedha zinazotengwa kwa wenzetu wa TARURA kutengeneza hizi barabara za vijijini ni kidogo sana je, Serikali haioni umuhimu mkubwa wa kutafuta vyanzo vingine na kuhakikisha kuwa, barabara zote zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini, anaweza kupatiwa fedha za kutosha? Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sisi wote Wabunge humu ndani ni mashahidi, maeneo mengi yanayopata makorongo makubwa katika halmashauri zetu na majimbo yetu yanahitaji mdaraja makubwa. Fedha zinazotolewa kwa wenzetu wa TARURA ni kidogo sana kiasi kwamba, hata kama wangepewa fedha makorongo hayo hayapo katika jiografia au mtandao wa barabara wanazohudumia wenzetu wa TARURA. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, Serikali haioni ni wakati wa kuja na mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayohitaji madaraja makubwa ambayo ni kikwazo kwa huduma za kijamii zikiwemo kliniki za akinamama, huduma za afya na elimu zinapatiwa mpango mkakati wa kujengewa madaraja hata ya chuma? Kwa kuwa, eneo hilo ni tete na… MWENYEKITI: Ahsante. Majibu kwa maswali hayo Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Hapana, Mheshimiwa Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi, Mheshimiwa Kwandikwa. NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli, fedha ambazo tunazipata kwa ajili ya matengenezo ya barabara nchi nzima, 4 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) ikiwemo pesa za TANROADS na TARURA ni kidogo. Sasa hivi uwezo wa fedha tunazopata ni asilimia 57 ya mahitaji. Hata hivyo niseme tu kwamba, kati ya fedha tunazozipata asilimia 90 zinakwenda kufanya matengenezo ya barabara, kwa hiyo, utaona kwamba ni asilimia 10 tu ndiyo inayokwenda kujenga barabara mpya. Kwa hiyo iko haja ya kuongeza fedha kwenye matengenezo ya barabara zetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, lile zoezi la kutambua network ya barabara kwa upande wa wenzetu wa TARURA, limefanyika, lakini kulikuwa na changamoto ya data ambazo zilipatikana; ikalazimika TARURA waende maeneo husika ili tuweze kuzitambua barabara zote ili sasa mgawo wa fedha na mahitaji ya fedha tuweze kuyaona kwa uhakika zaidi. Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo ambavyo vinatumika ni pamoja na urefu wa mtandao wa barabara, tunatumia vigezo pia vya aina ya barabara, kama ni barabara ya lami, barabara ya changarawe, barabara ya udongo na hali ya barabara ilivyo na idadi ya magari yanayopita katika maeneo. Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga na TARURA wanafanya kazi nzuri na ni kesho tu tunategemea taarifa itawasilishwa TAMISEMI, itawasilishwa kwenye Mfuko wa Barabara na upande wa kwetu kwenye Wizara, ili tuangalie mahitaji yetu halisi na tuweze kuomba fedha zaidi kukamilisha maeneo ambayo ni korofi. Kwa hiyo, kazi inaendelea ya kuhakikisha barabara zetu tunaziboresha. MWENYEKITI: Mheshimiwa Flatei. MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, Mheshimiwa Waziri amesema fedha za TARURA ni kidogo na yeye amepita barabara za Mbulu, hasa Tumati kwenda Martado ni mbaya sana. Je, 5 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) atatusaidiaje kwenye kipindi hiki ili barabara zile ziweze kutengenezwa na wananchi wakaondoa ile adha ya kupita kwenye barabara ambayo haipitiki kwa sasa? MWENYEKITI: Majibu kwa swali hilo, Mheshimiwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Kakunda. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyoeleza katika jibu la msingi na kama ambavyo amejibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa muuliza swali la msingi, Mheshimiwa Kwandikwa Naibu Waziri wa Ujenzi; taarifa ya tathmini ile ya kina ambayo tutaipata kuanzia kesho, hiyo ndiyo itakayotupatia taarifa sahihi ya barabara zote ikiwemo barabara ile ya kwenda Tumati ambayo tulipita na Mheshimiwa Mbunge kuanzia Yaeda Chini mpaka Tumati kule barabara si nzuri sana. Kwa hiyo, tutaiwekea utaratibu mzuri sana wa kipaumbele baada ya kuwa tumekubaliana vizuri zaidi na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi. MWENYEKITI: Mheshimiwa Haonga. MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tatizo la barabara katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu linafanana kabisa na tatizo la barabara katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlowo katika Jimbo la Mbozi. Naomba kuuliza, ni lini sasa Serikali itatengeneza barabara ambazo zipo katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlowo, Jimbo la Mbozi, ambazo wakati wa mvua mara nyingi zimekuwa hazipitiki? MWENYEKITI: Ahsante. Jibu kwa swali hilo Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Kakunda. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli. Tatizo alilolisema Mheshimiwa Mbunge katika eneo lake ni tatizo ambalo limekuwa likiikabili nchi 6 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) nzima wakati wa masika wakati mvua kubwa zikinyesha, hasa barabara zetu ambazo huwa zinaathirika sana ni barabara za udongo na barabara za changarawe, ukiacha barabara za lami ambazo maeneo machache, hasa ya madaraja ndio huwa yanaathirika zaidi. Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimpe ndugu yangu comfort kwamba, suala hilo linatambulika Serikalini. Katika tathmini ambayo tunaifanya tumezingatia hilo ili tuwe na backup ya kutosha wakati wa mvua kuweza kukabiliana na changamoto ambazo huwa zinajitokeza wakati wa masika. MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Kiula. MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru