Nakala Ya Mtandao (Online Document) 1
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE _____________ MKUTANO WA ISHIRINI Kikao cha Pili – Tarehe 13 Mei, 2015 (Mkutano Ulianza Saa 3.00 Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa tukae. Katibu! MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Waheshimiwa, maswali tunaanza na ofisi ya Waziri Mkuu, anayeuliza swali la kwanza ni Mheshimiwa Josephine J. Genzabuke, kwa niaba yake Mheshimiwa Likokola! Na. 11 Fedha za Mfuko wa JK kwa Wajasiriamali Wadogo MHE. DEVOTHA M. LIKOKOLA (K.n.y. MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE) aliuliza:- Mfuko wa Wajasiriamali wadogowadogo maarufu kama mabilioni ya JK uliwavuta wengi sana lakini masharti ya kupata fedha hizo yamekuwa magumu:- (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya mpango huo uwe endelevu kwa lengo la kuwanufaisha wanyonge? (b) Je, ni wananchi wangapi wa Mkoa wa Kigoma wamenufaika na mpango huo? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI NA UWEZESHAJI alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2006/2007, Serikali ilianzisha mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuongeza ajira kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu. Lengo la mpango huu ni kuwawezesha wananchi mijini na vijijini kupata mikopo ya kuanzisha au kuendeleza shughuli za kiuchumi ili kuongeza ajira na kipato. Masharti ya kupata mikopo hii si magumu sana ikilingalishwa na ile inayotolewa na mabenki, kwa sababu riba inayotozwa kwa mikopo hii ni asilimia 10, ikilinganishwa na riba inayotozwa na mabenki mengine, ambayo ni zaidi ya asilimia 20. Aidha, wananchi wanaopewa 1 Nakala ya Mtandao (Online Document) mikopo kutokana na Mfuko huu, hawahitajiki kuwa na dhamana kama zile zinazotakiwa na mabenki. Mheshimiwa Spika, ili kufanya mpango huu uwe endelevu, Serikali imepanga kufanya tathimini ya kina katika mwaka ujao wa fedha, tathmini inatarajiwa kufanyika katika maeneo yaliyopata mikopo hiyo kwa lengo la kubaini vikundi na wajasiriamali walionufaika, shughuli wanazozifanya, maendeleo ya shughuli hizo na changamoto zilizojitokeza. Mheshimiwa Spika, aidha, matokeo ya tathmini hiyo, yataiwezesha Serikali kuendeleza mpango huu kwa njia bora zaidi ikiwemo kuandaa utaratibu mzuri zaidi wa utoaji wa mikopo hii, utakaosimamiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. (b) Mheshimiwa Spika, kupitia mpango huu, Mkoa wa Kigoma ulipata mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 946.49, ambayo iliwanufaisha wajasiriamali 1,407. Kati ya wajasiriamali hao 553 wanatoka Kigoma Mjini, 827 wanatoka Kasuru, 207 wanatoka Kigoma Vijijini na 20 wanatoka Kibondo. MHE. DEVOTHA M. LIKOKOLA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nashukuru kwa majbu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Serikali haioni kwamba wananchi wengi mpaka sasa hawajawezeshwa kiuchumi, kwa sababu Baraza la Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi halina Kamati kuanzia ngazi ya Taifa mpaka ngazi ya vijiji na kwa maana hiyo kuwakosesha wananchi fursa. Je, Serikali itaweka msukumo katika kuunda Kamati za Kuwezesha Wananchi Kiuchumi, tangu ngazi ya Taifa, Mkoa, Wilaya, Kata, Vijiji na mpaka ngazi ya familia? Swali la pili, kwa nini Serikali haitumii benki ambazo zina matawi mengi mpaka vijijini. Kwa mfano, benki ya Posta na je, Serikali itakuwa tayari sasa hivi kutumia Benki ya Posta kwa ajili ya kuwakopesha wananchi wengi kwa sababu benki hii ni ya Serikali, lakini ina matawi mengi hadi vijijini? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU UWEKEZAJI NA UWEZESHAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza natambua kabisa hoja ya Mheshimiwa Likokola, maana mimi mwenyewe nimefanya ziara katika mikoa na wilaya. Udhaifu niliouona ni huo kwamba, Baraza mahali pengi bado halijajulikana. Kwa maelekezo niliyotoa nilipoingia hapa ofisini ni Baraza kutembea mikoani na wameanza. Nilivyowaeleza katika majibu yangu ni kwamba tunataka sasa kufanya mikopo hii iwe endelevu. Kwa hiyo, Baraza hili tunataka lishuke hadi ngazi ya familia kama anavyosema. Kwa hiyo, tunachotaka kukifanya sasa ni kuhakikisha kwamba mikoa kwanza ina watu wanaitwa focal points na wilaya zina watu wanaitwa focal points kushuka mpaka kwenye familia, ili wale walengwa waweze kujua, vinginevyo inakuwa vigumu mlengwa mwenyewe kama hajui Baraza linafanya kazi gani, akapate mikopo hii. Kwa hiyo, hoja ya Mheshimiwa Likokola ni ya msingi kabisa na ndiyo tunayoifanyia kazi kwa ajili ya kulifanya Baraza hili na mikopo hii iwe endelevu. Mheshimiwa Spika, kuhusu Benki ya Posta ni kwamba, tulipoanza tulichukua mabenki ya NMB, CRDB, tulitumia hata taasisi zingine, kama Pride, Dunduliza, ilikuwa ni mwanzo tu, wengine walifanya vizuri, wengine hawakufanya vizuri. Kwa hiyo, sasa ushauri alioutoa kutumia Benki ya Posta ambayo ina matawi hadi huko kwenye wilaya, huu ni mzuri na ndiyo maana nimesema tunafanya tathmini upya katika mwaka 2 Nakala ya Mtandao (Online Document) huu tuhakikishe kwamba tunatumia mtandao unaowafikia wakulima na wananchi wote ambao wako chini kabisa kuliko kuishia mikoani au makao makuu. MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia fursa hii. Kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema ni kwamba Baraza hili la uwezeshaji halijajulikana na Baraza hili ni la muda mrefu sana na ndiyo sababu kumekuwa na malalamiko makubwa, kwamba hata marejesho hayafiki kwa wakati. Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi, mikopo hii inatolewa kiitikadi. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri atueleze, wana mkakati gani kuhakikisha kwamba walengwa wote bila kujali itikadi za vyama wanapata mikopo hii, kwa sababu tumezunguka vijijini tunakuta matatizo hayo? Naomba Mheshimiwa Waziri atueleze ni kwa nini inafanyika hivyo na je, mna mkakati gani kuhakikisha Watanzania wote wa hali ya chini wanafaidika na Mfuko huu? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI NA UWEZESHAJI: Mheshimiwa Spika, lengo letu sisi ni kuhakikisha kwamba Mifuko hii ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, ambayo kwa kweli ni mingi, kwanza tunahitaji wawe na elimu, iko mingi zaidi ya 10, lakini walio wengi bado hawajaijua na mingine iko kwenye sekta mbalimbali na siwezi kuitaja hapa sasa hivi. Kwanza tunataka wajue ni Mifuko gani na iko wapi na masharti yake yakoje. Sasa kuhusu suala la utoaji, nimesema tutafanya tathmini kujua nani kapata mkopo, yuko wapi, ikiwa ni pamoja na kufanya uhakiki na ukaguzi kuhusu marejesho ya mikopo hii. Maana ukikopa ukarejesha inakuwa endelevu ndiyo na wengine wakope. Mheshimiwa Spika, suala la itikadi sina hakika kabisa kwamba hayo yalikuwa ni masharti, kwa sababu masharti ya kukopa hakuna mahali ambao tumesema yaendane na itikadi ama ya chama cha aina yoyote. Sisi walengwa ni wale, tuseme kwa kifupi tu, walala hoi! Maana ndiyo Mheshimiwa Rais alivyosema, tuwalenge wale wajasiriamali wadogo, whether ni wa chama hiki au kile, bila kujali itikadi. Na. 12 Maendeleo katika Wilaya ya Tarime MHE. NYAMBARI C. M. NYANGWINE aliuliza:- Wilaya ya Tarime imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 – 2015:- (a) Je, ni mambo yapi ya maendeleo yaliyopatikana katika kipindi hiki? (b) Je, kwa nini ujenzi wa daraja la Kyoruba ambalo Serikali iliahidi kulijenga haujafanyika? (c) Je, Serikali inasema nini juu ya ahadi ya Mheshimiwa Rais kuhusu ujenzi wa barabara ya Nyamwanga toka Tarime Mjini hadi Mto Mara kwa kiwango cha lami? 3 Nakala ya Mtandao (Online Document) NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nyambari Chacha Nyangwine, Mbunge wa Tarime, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2010 hadi 2015, Wilaya ya Tarime imepata mafaniko makubwa katika sekta ya barabara, afya, elimu, maji, kilimo, utawala na kadhalika. (b) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ilifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa daraja la Kyoruba uliobaini gharama za ujenzi wa daraja hilo kuwa ni shilingi bilioni 1.5, katika mwaka wa fedha 2014/2015. Katika mwaka huo Wizara ya Fedha ilipelekea Halmashauri shilingi milioni 50 tu na kutokana na ufinyu wa bajeti Halmashauri ilishindwa kutangaza zabuni hiyo. Aidha, Halmashauri ilishauriwa kuweka suala hili kwenye mpango wake wa bajeti. (c) Mheshimiwa Spika, barabara ya Tarime-Nyamwaga hadi Mto Mara hadi Mugumu hadi Natta Mbiso, yenye kilometa 123.97 ipo chini ya Wakala wa Barabara wa Mkoa wa Mara, yaani TANROADS, barabara hii hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2013/2014, ilikuwa na kilometa 5.53 za lami nyepesi zilizojengwa kutoka Tarime hadi Rebu. Katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, zimetengwa shilingi 2,131,300,000/= kwa ajili ya ujenzi wa kilometa mbili na tayari Mkandarasi amekwishapatikana wa kutekeleza kazi hiyo. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2015/2016, imeombewa shilingi bilioni nne kupitia katika bajeti ya maendeleo ili kuendeleza ujenzi wa lami kilometa nne. MHE. NYAMBARI C. M. NYANGWINE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa hili daraja gharama yake ya kulijenga ni shilingi bilioni moja na milioni mia tano na kwa kuwa uwezo wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, kutokana na vyanzo vyake vya ndani ni shilingi milioni 50, ambayo imetengwa kulijenga hili daraja na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri, nilishawahi kumuuliza hili swali akaniambia kwamba tuandike barua ya kuomba TAMISEMI isaidie kujenga hili daraja na hiyo barua niliipeleka kwake mimi mwenyewe. Sasa unawashauri nini