MKUTANO WA NNE Kikao Cha Tatu – Tarehe 8 Septemba, 2016
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ___________ MAJADILIANO YA BUNGE __________ MKUTANO WA NNE Kikao cha Tatu – Tarehe 8 Septemba, 2016 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Waheshimiwa Wabunge, naomba niwakaribishe kwenye kikao chetu cha tatu cha Mkutano wa Nne leo tarehe 8 Septemba. Katibu! NDG. ASIA MINJA – KATIBU MEZANI: MASWALI KWA WAZIRI MKUU SPIKA: Maswali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri Mkuu karibu. (Makofi) Kama ilivyo ada endapo kiongozi wa upinzani ana swali tunampa kipaumbele cha kwanza. Mheshimiwa Freeman Mbowe. MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kumuuliza Waziri Mkuu swali. Mheshimiwa Spika, kwa hali ilivyo nchini sasa hivi kiuchumi, kuna mdororo mkubwa wa uchumi, na katika mdororo huu wa uchumi ambao tuna imani kabisa katika hatua za baadaye utaathiri bajeti ya Serikali, wawekezaji wengi wanasita kuwekeza katika nchi kwa sababu ya kutokuwa na uhakika kuwa Tanzania ya kesho itakuwaje. Kuna kuporomoka sana kwa deposits ama amana zinazowekwa katika benki zetu za biashara, mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, mizigo katika Bandari ya Tanga, mizigo katika border posts za Namanga, Sirari, Horohoro na Tunduma imepungua kwa zaidi ya asilimia 60. 1 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Waziri Mkuu, baadhi ya makampuni ya usafirishaji kwa zaidi ya asilimia 40 yamefunga kazi zao au vyombo vyao vya usafirishaji, kwa maana ya malori makubwa yamesitisha safari na makampuni mengine yamehamia nchi nyingine za jirani kwa sababu ya kutokuwa na uhakika wa hali ya ndani. Je, hali hiyo kama Serikali mnaijua? Na kama mnaijua mnachukua hatua gani za makusudi za kurekebisha hasa ikizingatiwa kwamba uchumi unapoporomoka, kama ilivyo Tanzania leo mazao ya wakulima kama mbaazi, nafaka, mpunga nao unaanguka bei na tayari umeshaanguka bei kwa kiwango kikubwa? Mheshimiwa Waziri Mkuu, mna mkakati gani wa makusudi wa kurekebisha hali hii? (Makofi) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nianze leo kwa kujibu swali la Mheshimiwa Mbowe, Mbunge na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kwa swali lake muhimu kwa sababu linagusa hali ya uchumi ndani ya nchi. Mheshimiwa Spika, tunapozungumia hali ya uchumi tunazingatia mambo mengi na nikiri kwamba maeneo yote uliyoyatamka ni sehemu kubwa ya mchango wa hali ya uchumi nchini. Na kwa kutambua kwamba uchumi unashuka, inabidi tufanye tathmini ya kutosha, ingawa maeneo uliyoyatamka kwamba yamepungua sana nayo pia kuna haja ya kujiridhisha na kupata takwimu sahihi za miaka iliyopita na hali tuliyonayo sasa ili tujue kama je, kiwango cha kushuka kimesababishwa na nini? (Makofi) Mheshimiwa Spika, Serikali haitaweza kulala, malengo ya Serikali wakati wote ni kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi unaongezeka. Moja ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kwamba uchumi unakua kupitia nyanja zote pamoja na maeneo uliyoyatamka. (Makofi) Kwa hiyo, kupungua kwa mizigo bandarini kumekuwa kunazungumzwa na watu wengi na juzi juzi Kamati yetu ya Bunge ya Viwanda na Biashara ilikuwa bandarani kupitia hayo na wamekaa na wadau. Lakini wadau peke yao hawatoshi, ni lazima tupate pia taarifa kutoka ndani ya Serikali na mwenendo wa uendeshaji wa bandari, mipaka yetu, lakini pia mazao yetu ndani ya nchi na mwenendo wake mzima. (Makofi) Kwa hiyo, niseme kwa sasa kukupa takwimu halisi za kuporomoka au kutoporomoka si rahisi sana, lakini nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kwamba Serikali itafanya jitihada wakati wote kuhakikisha kwamba uchumi wake unapanda. Serikali itakubali kukutana na wadau kuzungumzia hatma ya uchumi nchini, Serikali itapokea ushauri kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge kwa namna ambavyo wanaona kwamba kuna 2 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) udhaifu mahali ili tuweze kuhakikisha kwamba uchumi unaongezeka na pia bajeti ya mwakani inapata mafanikio makubwa ukilinganisha na bajeti ambayo tunaitekeleza sasa. (Makofi) Mheshimiwa Spika, kwa hiyo basi bado nirudie kukuhakikishia kwamba Serikali haitalala katika hili kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi unapanda na kwa hiyo, kama changamoto ya maeneo ambayo umeyatamka tutafanya mawasiliano na Wizara ya Fedha lakini pia na Benki Kuu ili tuweze kupata takwimu halisi za hali ya uchumi nchini na tutakuja kulijulisha Bunge letu ili Wabunge wajue na wapate nafasi ya kutushauri. Kamati yetu ya Kudumu ya Biashara na Viwanda ipo, bado ina nafasi nzuri ya kuweza kutushauri kama Serikali. Ahsante sana. (Makofi) SPIKA: Swali la nyongeza Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe. MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, haihitaji utafiti wa ziada kujua uchumi umeshuka. (Makofi) Mheshimiwa Spika, lakini tunatambua kwamba Benki Kuu ndiyo taasisi muhimu katika Taifa ambayo mara kwa mara kila baada miezi mitatu ina- release data fulani fulani kuonesha hali ya uchumi katika Taifa, na tayari hali ya uchumi katika Taifa imeshaelezwa kwenye Ripoti ya Benki Kuu ambayo inatoka quarterly, kila baada ya miezi mitatu kwamba kuna kushuka kwa hali ya juu katika importation, kuna kushuka katika exportation, kuna kushuka katika construction industry, kuna kushuka katika circulation ya fedha. (Makofi) Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu hivi majuzi tulimsikia Mheshimiwa Rais akisema kwamba watu wanaweka fedha nyumbani, wanahifadhi fedha na ndiyo sababu mzunguko wa fedha umepungua katika circulation, kitu ambacho mimi binafsi naamini si kweli, na sijui vyanzo vya Mheshimiwa Rais ni nini kama Serikali ilikuwa haijafanya utafiti wa kina kujua kweli hali hiyo ipo. Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kamati ya Bunge ya Biashara na Uwekezaji ilikwenda Bandarini na ilitoa ripoti ambayo ni dhahiri, ni Kamati ya Bunge imedhihirisha hilo. Hao wadau mnaosema mtawashirikisha tayari wanalalamika. TATOA wanalalamika kuhusu mizigo yao, mahoteli yanafungwa, makampuni yanafungwa, watalii wamepungua, utafiti gani bado mnahitaji mjue kwamba uchumi umeanguka? (Makofi) Mheshimiwa Spika, nilitegemea leo Waziri Mkuu ujue kabisa waziwazi kwamba uchumi unaanguka na uchumi umeanguka na utueleze measures ambazo mnachukua kurekebisha hali hii. Lakini it seems like the government 3 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) haina uhakika ni nini kinaendelea. Waziri Mkuu unaonaje katika mazingira hayo, mka-declare kwamba mmeshindwa kuendesha Serikali hii? (Makofi) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbowe, Mbunge na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa kuanza kusema kwamba Serikali hiihaijashindwa kuongoza nchi hii. (Makofi) Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote, tutaongoza nchi hii kwa mafanikio makubwa sana kwenye sekta zote. Kazi hiyo imeanza kwa kufanya marekebisho makubwa ya maeneo ambayo tunadhani yatafanya Taifa hili liweze kupata mafanikio makubwa vilevile. (Makofi) Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani umeeleza hasa juu ya bandari. Kwanza nieleze kwamba Serikali imekuwa ikifanya mawasiliano na mataifa mengine yanayoendesha shughuli za bandari. Mwezi mmoja uliopita nilipokea timu ya wafanyabiashara maarufu duniani kutoka Singapore akiwemo mfanyabiashara anayefanya biashara za meli duniani. Alinieleza kwamba suala la mdororo wa usafirishaji wa mizigo kwa njia ya meli imeshuka duniani kote. Mheshimiwa Spika, suala la kupungua kwa mizigo maeneo yote ni kwa sababu ya hali ya kiuchumi duniani iliyotokana na kuporomoka kwa bei ya gesi na mafuta duniani. (Makofi) Mheshimiwa Spika, ukanda huu wa kwetu wa Afrika Mashariki ambako bandari yetu inatumika sana, nataka nikuhakikishie, Tanzania kupitia bandari zetu tunategemea sana mizigo kutoka Congo, Rwanda, Burundi kidogo lakini pia na Zambia; na wote mnajua kwamba Congo na Zambia ni nchi ambazo zilikuwa zinaelekea kwenye uchaguzi na kulikuwa na migongano mingi ndani ya nchi na wafanyabiashara wengi walisimama kidogo kufanya biashara zao; na hiyo ikasababisha kupungua hata kwa kiasi cha mizigo. Sio tu kwa Bandari ya Dar es Salaam pia hata usafirishaji kwenda kwenye bandari nyingine kutoka kwenye nchi hizo ambazo nimezitaja. (Makofi) Mheshimiwa Spika, lakini nataka nikupe faraja kwamba wiki moja iliyopita tumepata barua kutoka kwa timu ya wafanyabiashara wa Congo. Kutokana na hali iliyokuwepo awali na stabilization iliyopo sasa wametuhakikishia kwamba sasa usafirishaji wa mizigo yao yote utafanyika kupitia Bandari ya Dar es Salaam. (Makofi) Mheshimiwa Spika, Rwanda wametuandikia barua kutuhakikishia kwamba kutokana na mdororo uliokuwepo awali wafanyabiashara wengine kuamua kupeleka maeneo mengine kwa sababu ya hali ya kiuchumi lakini sasa 4 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) wameamua mizigo yote itapitia Bandari ya Dar es Salaam, hasa kwa mkakati wetu wa pamoja wa ujenzi wa reli ya standard gauge inayotoka Dar es Salaam - Tabora mpaka Bandari kavu ya Isaka, lakini tunaunganisha pia na reli hiyo standard gauge kwenda nchini Rwanda na kwa hiyo jitihada za kusafirisha mizigo sasa zitaimarishwa ili kuleta motisha ya ujenzi wa reli hiyo ili iendelee kusafirisha mizigo hiyo. (Makofi) Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nataka nikuhakikishie, ni kwamba haya yote uliyoyaeleza kama kuna jambo ambalo tunahitaji kukaa pamoja ni jambo la uchumi na hili ni jambo endelevu na nataka nikuhakikishie kwamba tutalifanyia kazi kwa kiasi kikubwa ili sasa tujiridhishe kila eneo na yale ambayo yanatakiwa na kama kufanya kampeni zaidi ya kupata wafanyabiashara zaidi, Serikali itafanya hilo kwa lengo lile lile la kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi