Nakala Ya Mtandao (Online Document) 1
Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE _____________ MKUTANO WA ISHIRINI Kikao cha Pili – Tarehe 13 Mei, 2015 (Mkutano Ulianza Saa 3.00 Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa tukae. Katibu! MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Waheshimiwa, maswali tunaanza na ofisi ya Waziri Mkuu, anayeuliza swali la kwanza ni Mheshimiwa Josephine J. Genzabuke, kwa niaba yake Mheshimiwa Likokola! Na. 11 Fedha za Mfuko wa JK kwa Wajasiriamali Wadogo MHE. DEVOTHA M. LIKOKOLA (K.n.y. MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE) aliuliza:- Mfuko wa Wajasiriamali wadogowadogo maarufu kama mabilioni ya JK uliwavuta wengi sana lakini masharti ya kupata fedha hizo yamekuwa magumu:- (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya mpango huo uwe endelevu kwa lengo la kuwanufaisha wanyonge? (b) Je, ni wananchi wangapi wa Mkoa wa Kigoma wamenufaika na mpango huo? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI NA UWEZESHAJI alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2006/2007, Serikali ilianzisha mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuongeza ajira kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu. Lengo la mpango huu ni kuwawezesha wananchi mijini na vijijini kupata mikopo ya kuanzisha au kuendeleza shughuli za kiuchumi ili kuongeza ajira na kipato. Masharti ya kupata mikopo hii si magumu sana ikilingalishwa na ile inayotolewa na mabenki, kwa sababu riba inayotozwa kwa mikopo hii ni asilimia 10, ikilinganishwa na riba inayotozwa na mabenki mengine, ambayo ni zaidi ya asilimia 20.
[Show full text]