Nakala Ya Mtandao (Online Document) 1 BUNGE LA TANZANIA
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ___________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA KUMI NA TANO Kikao cha Ishirini na Tano - Tarehe 3 Juni, 2014 (Mkutano Ulianza Saa 3.00 Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Mussa A. Zungu) Alisoma Dua MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge tukae. Katibu tuendelee! HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI: Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na :- NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. MWIGULU L. M. NCHEMBA): Randama za Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MWENYEKITI WA KAMATI YA HUDUMA ZA JAMII: Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, ya Huduma za Jamii Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 Pamoja na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MHE. RAJAB MBAROUK MOHAMMED (K.n.y. MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI WA WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MASWALI NA MAJIBU Na. 172 Tatizo la Maji Mkoa wa Kigoma. MHE. MOSES J. MACHALI K.n.y. MHE. DAVID Z. KAFULILA aliuliza:- 1 Nakala ya Mtandao (Online Document) Licha ya Mkoa wa Kigoma kuwa na kiasi kikubwa cha maji kuliko Mkoa wowote nchini bado Mkoa umekuwa miongoni mwa Mikoa ya mwisho kabisa kwa huduma duni ya maji nchini:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inafuta aibu hiii Mkoani Kigoma hususani katika Kata ya Kandaga ambapo mwezi Mei, 2012 wananchi walimzuia Mheshimiwa Rais kwa mabango na yeye kuahidi kulishughulikia tatizo hilo? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ELIMU) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa David Zacharia Kafulila, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma unakadiriwa kuwa asilimia 61 ya wakazi wake wanapata huduma ya maji safi na salama toka kwenye Visima vifupi 406, Visima virefu vyenye pampu za mikono 261 na Miradi ya Maji ya mserereko 102. Miradi mingine ni ya kusukuma kwa mashine 5, chemichem 545 na Miradi ya kuvuna maji ya mvua 202. Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Kandaga ipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza ikiwa na Vijiji vitatu vya Kandaga, Mlela na Kalenge. Asilimia 55 ya wakazi wapatao 23,696 Kata hii wanapata Huduma ya Maji. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha huduma ya maji hatua zifuatazo zimechukuliwa. Kwanza, Halmashauri ya Wilaya inatekeleza Mradi wa Maji kwa shilingi milioni 394.5 kwa mwaka 2013/2014 katika Kijiji cha Kandaga ambao umetekelezwa asilimia 65 na unatarajia kukamilika mwaka huu wa fedha. Kwa Mwaka 2013/2014 Halmashauri imetenga shilingi milioni 150 kupitia ruzuku ya Maendeleo (LGCDG) ili kufufua Mradi wa Maji wa kusukumwa na mashine. Kijiji cha Kalenge kinapata Huduma ya Maji kupitia Mradi wa Mtiririko uliojengwa kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA) kwa gharama ya shilingi milioni 251.8 Mradi huu una vituo 22 vinavyofanya kazi. Kijiji cha Mlela kinapata Huduma ya Maji kupitia Visima vifupi 3 vilivyojengwa kupitia fedha za ruzuku ya Maendeleo (LGCDG) kwa gharama ya shilingi milioni 14.8 na pia chemichemi 3 zilizohifadhiwa wa gharama ya shilingi milioni 6.5. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuboresha huduma ya maji katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kigoma kadiri rasilimali fedha zinavyopatikana. (Makofi) MWENYEKITI: Mheshimiwa Machali! MHE. MOSES J. MACHALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri maswali madogo ya nyongeza. Kwa kuwa katika roman 2 Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba imetengwa shilingi milioni 150 kupitia ruzuku ya (LGCGD) ili kufufua Mradi wa Maji wa kusukuma kwa mashine. Nilikuwa naomba commitment ya Serikali. Je, Serikali ipo tayari kuweza kuisukuma Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza kuonyesha kwamba fedha hizi zinapelekwa kwa ajili ya kuweza kuanza kazi hii? 2 Nakala ya Mtandao (Online Document) Kwa kuwa suala la kutenga fedha ni suala moja na utekelezaji wa fedha hizi kuhakikisha kwamba Mradi huu unatekelezeka ni suala jingine. Ni lini fedha hizi zitaanza kutumika na hatimaye mradi huu uweze kuwasaidia wananchi hawa? Swali la pili, kwa kuwa suala la Serikali kuwa inatenga fedha halafu matokeo yake fedha hizi hatuoni zikitumika. Kuna experience katika Mradi wa Maji wa Elijuu katika Jimbo la Kasulu Mjini. Mwaka 2011/2012 Serikali ilitenga shilingi milioni 85 lakini hadi leo hakuna kazi yoyote inefanyika. Naomba kauli ya Serikali kwamba ni kwanini Serikali imetenga fedha halafu Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu inashindwa kuweza kutumia fedha zile mpaka leo na wananchi wale hawana maji na ulikuwa ni Mradi wa kwa ajili ya ukarabati. MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri majibu. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ELIMU): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza anahitaji commitment ya Serikali ambayo itahakikisha kwamba tunapeleka fedha zile milioni 150 kwa ajili ya Mradi ule ambao tunautekeleza kupitia ruzuku ya maendeleo. Nimhakikishie kwamba mipango yetu ya maji kwenye ngazi za Vijiji ni endelevu na mipango hii iliyopo TAMISEMI fedha yote iliyokuwa inatakiwa kupelekwa kwa ajili ya Mradi wa Maji tunaifikisha na kwa kuwa Mradi huu uko kwenye Mwaka wa Fedha 2013/2014 ambao unaishia Juni hii mwishoni tuna uhakika na hiyo ndyo commitment ya Serikali. Tutapeleka fedha zote ili Mradi uweze kukamilika wananchi waweze kupata maji. Swali la nyongeza la pili linahusu Kasulu. Kama ambavyo nimesema kwenye jibu la Swali la kwanza la nyongeza kwamba commitment ya Serikali ni kuhakikisha Miradi yote iliyopangwa kwenye Vijiji vyetu inatekelezwa. Kama fedha hiyo itakuwa inatoka kwenye ngazi ya Wizara kuwapelekea Halmashauri bado jibu langu ni lilelile kwamba tutahakikisha tunapeleka fedha kwenye ngazi za Halmashauri ili Halmashauri ipeleke fedha kwenye ngazi za Vijiji kutekeleza Miradi hii ya Maji ili wananchi waweze kupata Maji safi na Salama. MWENYEKITI: Mheshimiwa David Silinde! MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Suala la Maji ni suala ambalo limekuwa likiulizwa na kila Mbunge. Maswali mengi ambayo yamekuwa yakielezwa ni ahadi ambazo Rais amekuwa akitoa moja kwa moja. Mimi nakumbuka mwaka 2010 Mheshimiwa Mwandosya ndiye uliyemwokoa Rais pale Tunduma kwa sababu watu walikasirika juu ya suala la Maji. Sasa napenda Serikali utapatie majibu, Rais anapotoa ahadi ya Maji ni muda gani inapaswa ikamilike? NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi anazozitoa Mheshimiwa Rais ni kwamba zitatekelezwa na kwamba kama ilikuwa 2010 basi ni ahadi ya miaka mitano tutaitekeleza na ni agizo. Kwa hiyo, si kweli kwamba tunaweza tukazipuuza kutekeleza ahadi za Mheshimiwa Rais. Lakini pia nimhakikishie tu rafiki yangu Mheshimiwa David Silinde, kwamba hebu soma soma ile Randama tumepeleka hela kidogo pale Tunduma. 3 Nakala ya Mtandao (Online Document) MWENYEKITI: Mheshimiwa Machangu! MJUMBE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti,… MWENYEKITI: Mheshimiwa Machangu, subiri kidogo kuna mkubwa wako kasimama hapa. Mheshimiwa Machangu kaa na akishajibu yeye imekwisha biashara hiyo. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, ASIYE NA WIZARA MAALUM (PROF. MARK J. MWANDOSYA) Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu Swali la nyongeza pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri ya Mheshimiwa David Silinde, kama ifuatavyo:- Kwanza niseme kwamba mimi siwezi kumwokoa Rais bali Rais ataniokoa mimi. Kwa hilo niliweke wazi kwamba hilo umezidisha umeweka chumvi. Jana tulifika mahali pazuri chini ya uongozi wako kwamba hata utekelezaji wa ahadi zote za Serikali itakuwa rahisi pale tukapoanzisha Mfuko wa Maji na tumeagizwa baada ya kukubaliana hapa kwamba tutaandaa Sheria mahsusi ya Mfuko huo ingawaje kwa sasa Mfuko huo umejificha ficha katika Sheria nyingine lakini sasa utakuwa mahsusi kwa ajili ya maji na utakuwa predictable na fedha zitapatikana. Kwa hiyo, tutaleta hapa Bungeni wakati unaofaa ili hata ahadi zote hizi tuwe na uhakika kabisa kwamba zitatekelezwa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi) Na. 173 Fidia ya Wafanyabiashara wa Maduka ya Nnanila. MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Wananchi wa Mnanila Manyovu ambao ni wafanyabiashara walijenga maduka mia moja na ishirini (120) kwa maelekezo ya Halmashauri ya Wilaya na baadaye TANROADS wakaja wakabomoa maduka hayo ya wafanyabiashara wamebaki wanahangaika bila msaada. Je, Kwanini Halmashauri isiwalipe fidia ya shilingi milioni tisini na sita (96,000,000) wafanyabiashara hao? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ELIMU) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabalila kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa eneo la Mtanila lilitengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kabla ya kugawanywa na kuanzisha Halmashauri nyingine ya Buhigwe kwa ajili ya ujenzi wa soko ambapo jumla ya wafanyabiashara 120 walijenga maduka katika eneo hilo. Aidha, mwaka 2004 TANROADS ilitoa notice ikiwataka Wananchi wote kubomoa nyumba na vibanda vyao vilivyopo ndani ya hifadhi ya barabara ili kupisha ujenzi wa barabara iliyokuwa ikijengwa kutoka Kigoma Manyovu (kilomita 60) kwa kiwango cha lami. Awali katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu inaandaa mchoro wa mipango Miji wenye namba 52/13/259 eneo hilo halikuwa limependekezwa