Nakala Ya Mtandao (Online Document) 1 BUNGE LA TANZANIA
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA __________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________ MKUTANO WA ISHIRINI Kikao cha Kwanza – Tarehe 12 Mei, 2015 (Kikao Kilianza Saa Tatu Asubuhi) WIMBO WA TAIFA D U A Spika (Mhe Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZA ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwaslishwa Mezani na:- WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (SERA, URATIBU NA BUNGE): Randama za Makadirio ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016. Hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016. MWENYEKITI WA KAMATI KATIBA SHERIA NA UTAWALA: Taarifa ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015 pamoja na maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016. MHE. SAID MUSSA ZUBEIR (k.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA UCHUMI, VIWANDA NA BIASHARA): Taarifa ya Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015 pamoja na maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016. MHE. ASHA MOHAMED OMARI (k.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Taarifa ya Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2015/2015 pamoja na Matumizi ya Ofisi hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016. MHE. OMARY A. BADWEL (k.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA MASUALA YA UKIMWI): 1 Nakala ya Mtandao (Online Document) Taarifa ya Kamati ya Masuala ya Ukimwi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015 pamoja na maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016. MHE. DAVID E. SILINDE (k.n.y. MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KWA OFISI YA WAZIRI MKUU): Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016. MHE. DAVID E. SILINDE (k.n.y. MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KWA OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI NA UWEZESHAJI): Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016. MHE. DAVID E. SILINDE - MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KWA OFISI YA WAZIRI MKUU (TAMISEMI): Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016. SPIKA: Ahsante. Tunaendelea. MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kama kawaida maswali tunaanza na Ofisi ya Waziri Mkuu na na swali la kwanza linaulizwa na Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, kwa niaba yake Mheshimiwa Grace Kiwelu! Na. 1 Ukosefu wa Huduma ya Mionzi (X-Ray) na Gari la Wagonjwa MHE. GRACE S. KIWELU (k.n.y. MHE. FREEMAN A. MBOWE) aliuliza:- Hospitali ya Wilaya ya Hai iliyoko katika Mji wa Bomang‘ombe inakadiriwa kuhudumia wananchi karibu 100,000 lakini inakabiliwa na ukosefu mkubwa wa vifaa ikiwemo huduma ya mionzi pamoja na gari la kubebea wagonjwa:- Je, ni lini Serikali itanunua vifaa hivi ili kuongeza huduma kwa wananchi hawa hasa ikizingatiwa kuwa hospitali hii ipo pembezoni mwa barabara kuu ya Moshi – Arusha yenye magari mengi na hivyo kukumbwa na ajali za mara kwa mara? SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri wa jirani na Hai! (Kicheko) NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, Mbunge wa Hai kama ifuatavyo:- 2 Nakala ya Mtandao (Online Document) Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kulikuwa na tatizo la ukosefu wa huduma ya mionzi ya X-Ray katika Hospitali ya Wilaya ya Hai, lakini kwa sasa tayari huduma hiyo inapatikana tangu mwezi Agosti, 2014. Kifaa hicho kilipatikana kwa kutumia fursa ya mikopo ya vifaa tiba inayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambacho kinagharamu kiasi cha Shilingi milioni 152. Aidha, huduma hii ya mionzi ilizunduliwa rasmi wakati wa mbio za mwenge na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Ndugu Rachel Kasanda tarehe 22/8/2014. Mheshimiwa Spika, kuhusu gari la wagonjwa, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa ni kweli kumekuwa na tatizo la kukosekana kwa gari hilo. Hospitali ya Wilaya ya Hai ilikuwa na gari moja aina ya Land Cruiser namba DFP 3962 toka mwaka 2007 lililokuwa linatukima kubebea wagonjwa. Mwezi Mei, 2014 lilipata ajali iliyosababisha kutoweza kutumika kwa gari hilo tena. Halmashauri kwa kuona umuhimu wa kuwepo kwa gari la wagonjwa ilitoa gari la Idara ya Mipango, gari namba STJ 9864 ili litumike kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa. Mheshimiwa Spika, kwa sasa Halmashauri ya Wilaya ya Hai inalo gari la wagonjwa Ambulance, aina ya Toyota Hiace lenye namba ya usajili T503 DDL gari hili lilitolewa na Taasisi ya Hai Kilimanjaro Development Initiative (HAKIDI), ikiwa ni sehemu ya jitihada za Mheshimiwa Mbunge. MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kifaa hicho kupatikana, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Spika, wiki mbili zilizopita, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Hai alikabidhi magari mawili ya wagonjwa, lakini aligomewa kutokulipa kodi:- Ni kwa nini Serikali ilishindwa kuondoa kodi hii kwasababu magari haya yalikuwa yanakwenda kuhudumia wananchi na siyo ya biashara? Swali la pili, Serikali sasa itakuwa tayari kuhakikisha inahudumia magari hayo ili yasiharibike kwenye matengenezo na mafuta? Mheshimiwa Spika, nakushukuru. NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Siha inatokana na Wilaya ya Hai, kwa hiyo, na- declare interest na hili swali anauliza home boy wangu. Nataka nieleze vizuri hapa ili tuweze kuelewana. Mheshimiwa Spika, haya magari ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Grace Kiwelu, lakini unapotaka kusajili gari hili na unapotaka kupata hiyo nafuu unayozungumzia (exemption) maana yake ni kwamba lile gari ni lazima lionekane kwamba consignee ni Halmashauri ya Wilaya ya Hai na hii jitihada iliyofanyika hapa, hii Taasisi inaitwa HAKIDI ni Taasisi ambayo ina-fall under Mheshimiwa Mbunge mwenyewe. Mheshimiwa Spika, mimi mwenyewe nimetafuta hizi hati za magari, nimekuta kwamba kule wana kivuli, hawana zile hati. Kwa hiyo, walipokwenda sasa, walipotaka kufanya hii habari ya kwamba wapate exemption, hawakuweza kupata exemption. Nikauliza kuhusu Mercedes Benz ambayo ilichukuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Hai, na hii gari nyingine, Toyota Land 3 Nakala ya Mtandao (Online Document) Cruiser ambayo ilianguka, nikauliza kama walipata exemption wakasema walipata exemption. Nikawaambia, kwa nini haya magari mawili ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaleta hapa, hayakupata exemption? Akasema sikiliza! Mheshimiwa Spika, hapa nazungumza na ninamnukuu Kaimu Mkurugenzi Zabdiel Wilson Mosha na ili kuwa na uhakika, nikamwambia thibitisha majibu yako hayo unayonipa! Ninayo barua nathibitisha. Akaniambia nathibitisha kwa maandishi. Akaniambia imekuwa ni vigumu kufanya hivyo kwa sababu bado lina-appear kwamba ni magari ambayo yako katika private ownership. Mheshimiwa Spika, najua kwamba Mheshimiwa Mbunge amefanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba magari haya yanakwenda. Wakitaka sasa wafanye hivi, itabidi wakabidhi hati zote ziende chini ya Halmashauri. Kwa nini? Inaweza kutokea siku moja, mambo hayaendi sawasawa, ukachukua nembo zile ukaondoa, ukaondoa kila kitu, ukarudisha magari yako. Mheshimiwa Spika, lakini ninachosema hapa, ili twende sambamba, hati zile zipatikane na consignee awe ni Halmashauri ya Wilaya ya Hai. Mheshimiwa Spika, kuhusu kuhudumia magari haya kwa sababu magari haya yanahudumia wananchi katika Wilaya ya Hai nitazungumza na Halmashauri ili kuona kwamba magari haya yanahudumiwa kwa utaratibu kwa sababu yanahudumia wananchi, lakini hili la hati tatizo lake limekuwa ni hilo. SPIKA: Mheshimiwa Machangu, swali la nyongeza. MHE. BETTY E. MACHANGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi na Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambayo ni DDH na Mawenzi ni ya Serikali; hospitali hizi hazina scanner. Wagonjwa wa Mkoa wa Kilimanjaro wanakwenda mpaka Arusha Selian Hospital kupata hii huduma. Mheshimiwa Spika, hata kama KCMC ni DDH, ni ya Kanisa, Serikali haioni kwamba wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wanahitaji huduma hii? Hawaoni kwamba ni mateso kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro? SPIKA: Kutoka X-Ray mpaka vitu vingine! Mheshimiwa Naibu Waziri, wewe huhitaji kugonga, unasimama tu. (Kicheko) NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Ahsante. Wakati mwingine unakuwa busy kidogo. SPIKA: Haya Mheshimiwa Naibu Waziri, endelea. NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Mheshimiwa Spika, kwa mradi mkubwa ambao tunao Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Serikali ya Uholanzi ambao utagharimu shilingi bilioni 22 na Tanzania itachangia shilingi bilioni 11, hospitali zote za Mikoa zitapata scanner ambazo tunaita ni Computed Radiography System ambazo zina hadhi za Hospitali za Rufaa za Mikoa. 4 Nakala ya Mtandao (Online Document) Mheshimiwa Spika, Hospitali zote za Kanda nchini ikiwemo KCMC, Bugando na Hospitali ya Mbeya, zitapata CT Scanner baada ya kusaini mikataba na pesa hii kulipwa ambayo ni Computed Radiography System ambazo zitaenezwa katika maeneo yote. Mheshimiwa Spika, lakini pia nitoe taarifa kwa Watanzania wote walio hospitali zote nchini zile ambazo ziko katika mradi huu zipatazo 50 ngazi ya Wilaya, zote zipate X-Ray za kisasa ambazo ni za digital, lakini