Online Document)
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ______________ MAJADILIANO YA BUNGE _____________ MKUTANO WA NNE Kikao cha Hamsini na Moja - Tarehe 19 Agosti, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatayo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA MAJI: Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Taarifa ya Mwaka na Hesabu zilizokaguliwa za Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha, 2009/2010 (The Annual Report and Audited Accounts of the Local Authorities Pensions Fund for Financial Year 2009/2010). NAIBU WAZIRI WA MAJI: Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. NAIBU WAZIRI WA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Hotuba ya Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MHE.BETTY E. MACHANGU (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA): Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka 2010/2011 Pamoja na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani juu ya Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MASWALI NA MAJIBU Na. 450 Uhitaji wa Hospitali ya Wilaya ya Tabora Mjini MHE. SAID J. NKUMBA (K.n.y. MHE. MUNDE T. ABDALLAH) aiuliza:- 1 Wilaya ya Tabora Mijini ni miongoni mwa Wilaya zisizo na Hospitali ya Wilaya na kutokana na hali hiyo, husababisha msongamano mkubwa kwenye hospitali ya Mkoa wa Tabora ambayo inahudumia wagonjwa wa Wilaya zote sita (6) za Mkoa huo:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga hospitali ya Wilaya Tabora Mijini kufuatia maombi ambayo yameshapelekwa Serikalini? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munde Tambwe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Manispaa ya Tabora haina Hospitali ya Wilaya. Kwa kuzingtaia ukweli huu, Halmashauri imetenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo katika eneo la Ipuli lenye ukubwa wa mita za mraba 16,000. Aidha, ramani za majengo ya Hospitali hiyo zimepatikana. Kwa mwaka wa fedha 2010/2011, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ilitenga jumla ya shilingi milioni 100 fedha za ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa (CDG) ili kuanza ujenzi wa Hospitali hiyo. Mheshimiwa Spika, katika Bajeti ya mwaka 2011/2012 zimetengwa shilingi milioni 100 kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani (Own Source) kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na wodi ya wazazi (Maternity Ward). Aidha, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora iliwasilisha maombi maalum ya jumla ya shilingi milioni 600 katika Bajeti ya mwaka 2011/2012 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. MHE. SAID J. NKUMBA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. (a)Kwa kuwa kumekuwa na msongamano mkubwa sana katika hospitali ya Kitete, Tabora na Hospitali hii ni Hospitali sasa ya Rufaa na kwa kuwa Manispaa ya Tabora ilitenga shilingi milioni 100 kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri hapa. Je, Serikali Kuu ina mchango gani katika kusaidia Manispaa ya Tabora ili ujenzi huo ambao umeanza pale Ipuli uweze kwenda kwa haraka? (b)Kwa kuwa Sikonge vile vile tumeanzisha mkakati wa kuhakikisha kwamba tuwe na Hospitali ya Serikali ya Wilaya pale kuna KItuo cha Afya cha Mazinge ambacho Mheshimiwa Naibu Waziri alikwisha kuja kukitembelea. Je, mikakati ambayo inaweza ikafanyika pale Tabora inaweza ikafanyika vilevile Sikonge ili na sisi tuweze kufaidika na ujenzi wa Hopsitali hii ya Wilaya? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saidi Nkumba, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, anachosema Mheshimiwa Saidi Nkumba ni sahihi. Hospitali ile ya Tabora pale ya Kiteto inayotumiwa na Manispaa ya Tabora na ndiyo hiyo hiyo inayotumiwa pia na Wilaya ya Uyui ambayo sisi Kihalmashauri tunaiita Halmashauri ya Wilaya ya Tabora. Pameshonana pale ni kweli kama anavyosema. Sasa hela zilizopelekwa pale kwa ajili ya kuanzisha hii Hospitali mpya tunayozungumza katika eneo la Ikuli, wametenga milioni 100 na halafu katika own source wametenga milioni nyingine 100 hapa. 2 Sasa anazungumza habari ya Serikali Kuu kwamba inaingiaje pale. Kwa takwimu nilizopata, mimi nimezungumza na Mkurugenzi Mtendaji Fannuel Senge, ameniambia waliomba shilingi milioni 600, lakini kwa sababu ya ufinyu wa Bajeti imeonekana kwamba hela hizi hazikuweza kupatikana, tumeahidi kama Wizara tutasaidia kwa ajili ya kufuatilia jambo hili ili tuweze kuona kwamba hela hizi zinapatikana kwa ajili ya Ilupi. Hii ya pili anayoizungumza hapa, wao Sikonge wana DDH hii Designated District Hospital ambayo ndiyo wanaitumia kama Hospitali ya Wilaya, lakini katika Kituo hiki anachokizungumza kwamba nilifika pale, ni kweli panafaa pale kuwa Hospitali ya Wilaya, hakuna tatizo la kuwa na Designated Hospital na hiyo nyingine. Kwa hiyo, ninachoomba sasa Mheshimiwa Nkumba kwa maana najua ni mfuatiliaji mzuri mambo ya Tumbaku na nini atusaidie sasa kuipeleka katika Halmashauri wazungumze habari hii, wakubaliane kwamba wanata kujenga Hospitali ya Wilaya na kukuza sasa status ya hicho Kituo cha Afya. Sisi kama Wizara tutashirikiana nae kusaidia katika jambo hili. MHE. SUSAN LYIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Tatizo linalozungumzwa la Tabora linafanana sana na la Mkoa wa Kilimanjaro katika hospitali ya Mkoa ya Mawenzi na hili tuliliongea sana wakati wa Bajeti ya Wizara ya Afya. Naibu Waziri anaelewa kwamba Hospitali ya Mawenzi kwa sasa hivi haina theatre na matokeo yake wagonjwa wote hata akiwa na cut wound inabidi apelekwe KCMC, sasa Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kujua ulisema tatizo lile utalishughulikia, lakini mpaka sasa hivi bado. Ni lini sasa theatre ile itaweza kutengenezwa ili wagonjwa waweze kuhudumiwa pale na hasa ikizingatiwa kwamba akina mama wengi wajawazito, watoto wao wengi wamefariki kutokana na hali hiyo? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Susan Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, kwanza naomba ni declare interest, Hospitali ya Mawenzi ni Hospitali ya Mkoa wa Kilimajaro na mimi natoka kutoka Wilaya ya Siha. Kwa hiyo, mimi ni mdau kwa wagonjwa wa Wilaya ya Siha wanaenda kutibiwa pale. Kwa hiyo, naomba ni-declare interest, hilo la kwanza. La pili, ahadi iliyotolewa hapa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu habari ya Mawenzi Hospital sisi wote tuliisikia hapa. Kikao cha Bunge hakijaisha, kikao kinaendelea mpaka sasa hivi tunavyozungumza, nilisema mimi nita-head delegation situmi mtu pale, Mawenzi Hospital nitakwenda mimi mwenyewe, Mheshimiwa Mkuchika ameshaniruhusu na Waziri Mkuu amekubali na Wabunge tutakwenda wote pale tukajue ni nini kilichotokea pale, kwisha. Kwa hiyo, kama kuna watu wanafikiri kwamba hatutakwenda, tutakwenda pale kuhakikisha kwamba ni nini kilichotokea. Mheshimiwa Susan Lyimo, asubiri ataona tutakachofanya. (Makofi) SPIKA: Vitendo ni bora kuliko maneno, haya. (Kicheko) Na. 451 Kero ya Maji Ilula-Kilolo MHE. DIANA M. CHILOLO (K.n.y. MHE. RITTA E. KABATI) aliuliza:- Iko ahadi ya kuwapatia wananchi wa Ilula Wilayani Kilolo wamekuwa na tatizo sugu kwa muda mrefu:- 3 (a) Je ni lini Serikali itamaliza kero hiyo ya maji kwa wananchi wa Ilula, Uhambing’eto na Kipaduka? (b) Je, Seriklai iko tayari kuongozana na Mbunge husika kutembela maeneo hayo ili kujionea hali halizi ilivyo? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAAalijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, ili kutatua kero ya maji Mji wa Ilula, Serikali katika mwaka 2009 kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji iliipatia Mamlaka ya Maji ya mji mdogo wa Ilula shilingi milioni 230 kwa ajili ya kupanua mtandao wa maji, kujenga tanki lenye ujazo wa lita 100, kulaza mabomba yenye urefu wa Km 6 ili kufikisha maji katika Kijiji cha Ikuvala, ujenzi wa vituo 8 vya kuchotea maji, na ununuzi wa mita za maji 250. Aidha, katika mwaka huo, Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji (WSDP) iliidhinisha shilingi milioni 40.5 kwa ajili ya ukarabati wa visima, kununua mitambo miwili ya kusukuma maji na kukarabati matanki ya maji katika Kijiji cha Uhambing’eto. Kupitia Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo wa Wilaya (DADPs) Seriklai ilitoa shilingi milioni 25 kwa ajili ya ukarabati wa Bwawa la kuvunia maji ya mvua linalotumika kwa ajili ya matumizi ya binaadamu na mifugo. Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Kipadula katika mwaka 2008 kilipatiwa shilingi milioni 26.2 fedha za Mfuko wa TASAF kwa ajili ya kuchimba visima viwili virefu vinavyotumia pampu za mikono. Aidha, Kijiji hicho ni miongoni mwa Vijiji 10 vilivyochaguliwa katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Programu ndogo ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ambapo Vijiji vya Ikuka, Kipaduka na Vitono vinahusika. Katika mwaka 2011/2012 zimetengewa shilingi milioni 654 kwa kazi hizo. (b) Mheshimiwa Spika, nipo tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge ili kutatua kero za maji katika maeneo yaliyotajwa. MHE. DIANA M. CHILOLO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza:- (a) Kwa kuwa alikuwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt.