1 BUNGE LA TANZANIA MKUTANO WA PILI Kikao Cha Sita
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA MKUTANO WA PILI Kikao cha Sita – Tarehe 15 Februari, 2011 (Kikao Kilianza Saa 3.00 Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati ifuatayo iliwasilishwa Mezani:- NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Taarifa ya Mwaka na Hesabu zilizokaguliwa za Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwa Mwaka ulioishia tarehe 30 Juni, 2010. (The Annual Report and Accounts of TCRA Consumer Consultative Council, TRCA – CCC for the year ended 30th June, 2010). MASWALI NA MAJIBU Na. 67 Madai ya Walimu Wastaafu – Singida MHE. MWIGULU LAMECK MCHEMA MADELU (K.n.y. MHE. DIANA MKUMBO CHILOLO) aliuliza:- Walimu wanane (8) wastaafu wa Manispaa ya Singida waliokuwa wameajiriwa kwa mkataba bado hawajalipwa madai ya mishahara ya miezi kumi na sita (16) licha ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kulifuatilia suala hili kwa karibu:- Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya suala hilo? NAIBU WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI (K.n.y. WAZIRI MKUU) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Diana Mkumbo Chilolo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- 1 Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna walimu wastaafu nane waodai malimbikizo yao ya mishahara. Mheshimiwa Spika, kilichojitokeza hapa ni utaratibu wa mikataba kutoeleweka vizuri. Hivyo wahusika kukosea kosea mikataba na kurudishwa ili kujaza upya na hivyo kuchelewesha zoezi la ulipaji wa mishahara hiyo. Mheshimiwa Spika, kwa utaratibu wa sasa mwajiri ambaye ni Halmashauri huomba kibali cha kuajiri walimu wastaafu kwa mkataba toka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Baada ya kibali kutolewa Halmashauri husika huingia Mkataba na walimu watakuwa wameridhika na sifa za uwezo wao wa kufundisha mishahara yao na kufundisha katika shule za msingi na Sekondari. Walimu hawa na mikataba yao watalipwa mishahara yao kwa viwango vyao walivyofikia kabla ya kustaafu kwao katika orodha ya malipo (payroll ya Serikali Hazina. Aidha, malipo ya walimu hawa yameandaliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kinachosubiriwa sasa ni kibali cha Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili walipwe madai yao. MHE. DIANA MKUMBO CHILOLO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri swali hili nimeshauliza ndani ya Bunge hili mara nne leo ni mara ya tano. Kwa kuwa inasikitisha sana Serikali imekuwa ikiniahidi ndani ya Bunge hili kwamba malipo ya walimu hawa ni halali na yanaandaliwa mara zote. Mara ya nne nikajibiwa mwaka jana mwezi wa nne kwamba malipo yao yatalipwa kabla ya Bunge la Bajeti Julai mwaka jana 2010. Leo hii tena naambiwa kibali cha utumishi kinasubiriwa. SPIKA: Jitahidi maswali ya nyongeza yawe mafupi. MHE. DIANA MKUMBO CHILOLO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara hii iko chini ya Waziri Mkuu naweza nikapewa kauli ya Serikali kuhusu madai haya kwa kuwa walimu hawa wana hali mbaya sana? (Makofi) Kwa kuwa inaonyesha wazi watendaji, ndani ya Wizara ya Elimu ukiacha TAMISEMI ambayo imegatuliwa sasa hivi wanadharau kauli za Mawaziri wanazotoa hapa Bungeni. Je, inasema nini kuhusu watendaji hawa wanaokwamisha utekelezaji wa Serikali ya CCM na kunifanya mimi mwakilishi wa walimu hawa kuonekana sina maana? (Makofi) NAIBU WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba swali hili limeulizwa hapa kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge, lakini napenda nimhakikishie kwamba kwa kipindi hiki cha ugatuaji wa madaraka kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo kwenda TAMISEMI tukiwa tunashughulikiwa walimu wa elimu ya msingi na sekondari sasa jambo hili tutalifuatilia na mimi sasa kwa kuwa ndio mhusika na ndio mwenye dhamana ya elimu ya msingi na sekondari ndani ya 2 TAMISEMI nitahakikisha nafuatilia jambo hili mpaka linapata mafanikio. Sitakubali tena hili lije kuulizwa tena hapa mwezi Aprili . (Makofi) Na. 68 Hitaji la Umeme Katika Vijiji vya Jimbo la Mbeya Vijijini MHE. MCH. LUCKSON NDAGA MWANJALE aliuliza:- Umeme unapitia katika vijiji vya Haporoto, Idimi Kata ya Ihangu na Kijiji na Lwanjilo, Ifupa kata ya Ilungu, Iyawaya Kata ya Inyala, Songwi Juu Kata ya Ijombe kuelekea Wilaya nyingine lakini hakuna transfoma kwenye maeneo hayo:- Je, ni lini Serikali itafunga transfoma katika Kata hizo ili wananchi hao waweze kupata huduma ya umeme? NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:- Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mch. Luckson Ndaga Mwanjale, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:- Ni kweli vijiji alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge ni kati ya vijiji 112 vilivyomo kwenye jimbo la Mbeya Vijijini ambavyo bado havijapata huduma ya umeme japo vinapitiwa na njia za msongo wa kilovolti 33 na 11. Zoezi la kutathimini gharama za ufungaji wa transfoma na ujenzi wa njia za umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 ili kuvipatia umeme vijiji alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge linatarajiwa kuanza mwezi Februari, 2011 na litakamilika mwezi Machi, 2011. Maombi ya fedha kwa ajili ya mradi huo yanatarajiwa kuwasilishwa kwa wakala wa Nishati Vijijini (REA) punde baada ya tathimini hiyo kukamilika. Mheshimiwa Spika, aidha, zoezi la kuainisha vijiji vyote nchini vinavyopitiwa na njia za umeme msongo wa kilovoti 33 ama 11 na ambavyo havina umeme vikiwemo vijiji alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge, limekamilika na kukabidhiwa kwa wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa hatua zaidi. MHE. MCH. LUCKSON NDAGA MWANJALE: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kazi hiyo itakamilika mwezi Machi. Je, Waziri atanihakikishia kwamba gharama hizi zitaingizwa katika Bajeti ya mwaka huu na kwamba mwaka huu umeme uanze kufungwa pale? Ahsante sana. (Makofi) NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, mradi wa sasa hivi katika hii miradi iliyokuwepo pale kwake ni kutoka Izombwe kwenda Santilia, Santilia kwenda Hongoro ambao ndio mradi ambao uko kwenye utekelezaji sasa hivi. Nilichosema ni kwamba baada ya mradi huu kukamilika ambao umeshafanyiwa tathimini mkandarasi ameshafika, vifaa vingine vinakuja, nguzo zilizokuwepo pale kama miaka minane (8) zimesimama tu zimeshaharibika. Kwa hiyo, zinakuja nguzo mpya zinaanza 3 kuwekwa kuanzia mwezi wa nne. Lakini tukimaliza kazi hii ndio tunaanza kusambaza sasa kutokana na mradi huu, ni mradi mkubwa kwenda kwenye vijiji alivyovitaja. Kazi ya kufanya tathimini ya vijijini hivyo ndio tunatarajia iingie ikamilike baina ya mwezi wa pili na wa tatu Machi, 2011 na kwa maana hiyo, tunatarajia tutavitumbukiza katika Bajeti ya Wizara na ya REA ili tuone kama tutapata utekelezaji mwaka ujao. MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bado tuko kwenye maeneo ya Mbeya ningependa kujua ni limi umeme utapelekwa kwenye Kata za Iziwa, Itagano, Itende, Mwansekwa na Tembela zote za Mbeya Mjini ambalo ni Jiji kwa kuwa baadhi ya Kata kama Isiwa tayari wananchi walishafanya wiring kwenye nyumba zao miaka mingi? Ahsante sana. (Makofi) NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, tumepokea Kata hizo alizozitaja Mheshimiwa Mbunge, lakini naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbilinyi kwamba Wilaya ya Mbeya Mjini inatarajia kupata mradi wa usambazaji umeme kupitia MCC na ambao wakandarasi wameshafika wameshafanya tathimini. Kwa hiyo, tunatarajia kwamba maeneo mengi kwa sababu ndio sera ya MCC hayo ambayo yatafikiwa na mradi wa MCC baada ya hapo yale mengine tutafanya sisi wenyewe. Kwa hiyo, naomba tufanye subira ili tukamilishe mradi huu wa awamu ya MCC ya usambazaji katika maeneo mbalimbali Mkoa wake uko katika Mikoa Sita itakayofikiwa na mradi huo halafu tufanye tathimini ya hayo maeneo mengine ambayo yatakuwa hayajafikiwa na mradi huo. Na. 69 Benki Kutoza Riba Kubwa MHE. ABBAS ZUBERI MTEMVU aliuliza:- Benki za CRDB, NMB na NBC zilizoko ndani ya Ofisi za Bunge Dodoma, zimekuwa zikitoa mikopo ya riba ya 15% wakati kuna asilimia moja inakatwa kwa ajili ya bima:- (a) Je, ni kwa nini riba hiyo ni kubwa sana na wakati mkopaji ana dhamana ya mshahara wake na pia ana bima ya asilimia moja? (b) Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka wa kuzungumza na benki hizo ili zishushe riba zake? NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. PEREIRA AME SILIMA) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ruhusa yako, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abbas Zuberi Mtemvu, Mbunge wa Temeke, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- 4 (a) Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba, kufuatia mageuzi ya sekta ya kifedha nchini kuanzia mwaka 1991, Serikali ilisitisha upangaji wa riba zinazotozwa na mabenki na kuruhusu riba hizo kuwekwa kwa nguvu ya soko, mahitaji na ugavi. Lengo la hatua hii likiwa ni kuweka riba zinazoendana na hali halisi ya soko kwa kuzingatia pamoja na mambo mengine, sifa alizonazo mkopaji. Ningependa kumfahamisha Mheshimiwa Abbas Mtemvu kwamba japokuwa dhamana ya mishahara na bima ni vigezo muhimu vinavyotumiwa na mabenki katika kupanga viwango vya riba, hivyo siyo vigezo pekee na havitoshelezi. Kwa mantiki hiyo basi mabenki yamekuwa yakitoa sababu mbalimbali za kutoza riba kubwa kwa baadhi ya wakopaji. Kwa mfano, sababu ya kwanza ni sifa alizonazo mkopaji, urahisi wa upatikanaji wa taarifa juu ya sifa za wakopaji, ikiwa ni pamoja na vyombo vinavyoweza kuhakiki usahihi wa taarifa hizo. Sababu nyingine zinazotolewa na mabenki ni ukosefu wa dhamana zinazokubalika na kuuzika kwa urahisi. (b) Mheshimiwa Spika, katika kuboresha huduma za sekta ya kifedha, ikiwa ni pamoja na kupunguza riba kwa ujumla na sio kwa wafanyakazi pekee, Serikali inatekeleza awamu ya pili ya mageuzi katika sekta ya fedha (The Second Generation Financial Sector Reforms). Chini ya mpango