MKUTANO WA TATU Kikao Cha Hamsini Na Sita
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA TATU Kikao cha Hamsini na Sita – Tarehe 22 Juni, 2021 (Bunge Lilianza saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba tukae. Waheshimiwa tunaendelea na Mkutano wetu wa Tatu, leo ni Kikao cha Hamsini na Sita na kabla hatujaendelea nitumie nafasi hii kuwashukuru sana wasaidizi wangu wote wakiongozwa na Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa David Kihenzile, Mheshimiwa Zungu na Mheshimiwa Najma kwa kazi nzuri ambayo wameifanya wiki nzima kutuendeshea mjadala wetu wa bajeti. (Makofi) Sasa leo hapa ndio siku ya maamuzi ambayo kila Mbunge anapaswa kuwa humu ndani, kwa Mbunge ambaye Spika hana taarifa yake na hatapiga kura hapa leo hilo la kwake yeye. (Makofi) Katibu. NDG. NENELWA MWIHAMBI – KATIBU WA BUNGE: MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Maswali na tunaanza na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Na. 465 Ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri Katika Mji wa Laela MHE. DEUS C. SANGU aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Halmashauri ya Sumbawanga katika Mji wa Laela baada ya agizo la Serikali la kuhamisha Makao Makuu? SPIKA: Majibu ya swali hilo muhimu la watu wa Kwela, Mheshimiwa Naibu Waziri - TAMISEMI, Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange tafadhali. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ni miongoni mwa Halmashauri 30 zilizohamia kwenye maeneo mapya ya utawala mwaka 2019.
[Show full text]