MAJADILIANO YA BUNGE ___MKUTANO WA KUMI NA MOJA Kikao Cha Hamsini Na Tatu
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA KUMI NA MOJA Kikao cha Hamsini na Tatu – Tarehe 19 Juni, 2018 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Dkt. Tulia Ackson) Alisoma Dua NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Katibu. NDG. PAMELA PALLANGYO – KATIBU MEZANI: HATI ZA KUWASILISHA MEZANI Hati ifuatayo iliwasilishwa mezani na:- WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO): Taarifa ya mwaka na Hesabu zilizokaguliwa za Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa mwaka wa fedha 2014/2015 (The Annual Report and Audited Accounts of the Roads Fund Board for the Financial Year 2014/2015). NAIBU SPIKA: Katibu. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) NDG. PAMELA PALLANGYO – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU Na. 447 Kupandisha Hadhi Kituo cha Afya Sinza Kuwa Hospitali ya Wilaya MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:- Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alipotembelea Kituo cha Afya cha Palestina kilichopo Kata ya Sinza alitangaza kukipandisha hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya. Hata hivyo, bado Serikali inaendelea kuipatia fedha hospitali hiyo kama Kituo cha Afya. Je, ni lini Serikali itaitambua hospitali hiyo kama Hospitali ya Wilaya kwa kuipa fedha na vitendea kazi vinavyofanana na hadhi yake? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Palestina kimekuwa kinafanya kazi kama Hospitali ya Wilaya kufuatia tamko la Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne la tarehe 11 Disemba, 2012.
[Show full text]