20 DESEMBA, 2013 MREMA 1.Pmd
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _______________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA KUMI NA NNE Kikao cha Kumi na Nne – Tarehe 20 Desemba, 2013 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Mussa A. Zungu) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati Zifuatazo Ziliwasilisha Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. SAADA M. SALUM): Taarifa ya Mwaka ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Mwaka 2011/2012 [The Annual Report of Tanzania Revenue Authority (TRA) for the Year 2011/2012]. 1 Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) [NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. SAADA M. SALUM)] Taarifa ya Mwaka na Hesabu Zilizokaguliwa za Fungu 45 – Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2012 [The Annual Report and Audited Financial Statement of Vote 45 – National Audit Office for the Financial Year ended 30th June, 2012]. MHE. ABDULKARIM E. H. SHAH – MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA ARDHI, MALIASILI NA MAZINGIRA: Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Kuhusu Utekelezaji wa Shughuli zake kwa Mwaka, 2013. MHE. REBECCA M. MNGODO (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KILIMO, MIFUGO NA MAJI): Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Utekelezaji wa Shughuli zake kwa Mwaka, 2013. MASWALI NA MAJIBU Na. 159 Kutumia Maji ya Chemchem Jimboni Tabora Kaskazini MHE. ISMAIL A. RAGE (K.n.y. MHE. SHAFFIN A. SUMAR) aliuliza:- Katika Kata za Magiri, Ishilimulwa na maeneo mengine ya Jimbo la Tabora Kaskazini, kunapatikana maji ya chemchem:- Je, kwa nini Serikali isiyatambue maeneo hayo na kupima hayo maji kama yanafaa kwa matumizi ya binadamu na kisha kuboresha huduma hiyo? 2 Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shaffin Ahmedali Sumar, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, kama ifuatayo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Magiri na kijiji cha Ishihimulwa katika Kata ya Bukumbi, kuna chemchem tatu (3) zilizo hai, kati ya hizo mbili ziko katika Kata ya Magiri na moja katika kijiji cha Ishihimulwa Kata ya Bukumbi katika Jimbo la Tabora Kaskazini. Aidha, Jimbo zima la Tabora Kaskazini lina jumla ya chemchemi kumi na tatu (13). Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa fedha 2010/2011 Halmashauri ya Wilaya ya Uyui ilitenga na kuidhinishwa shilingi 4,000,000,000/= ambazo zilitumika kufanya utafiti na kupima ubora wa maji katika chemchem ya kijiji cha Isikizya na kubaini kuwa maji haya yanafaa kwa matumizi ya Binadamu. Chanzo hiki cha maji kimeboreshwa na kinatoa huduma katika Ofisi za Makao Makuu ya Wilaya ya Uyui na kwa wananchi wa maeneo ya jirani. Mradi huu uligharimu jumla ya shilingi 200,000,000/= kwa mwaka wa fedha 2011/2012 zinazohusisha uboreshaji wa chemchem sita (6) pamoja na ujenzi wa miundombinu mingine ya maji. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2011/2012 kiasi cha shilingi 9,000,000/= kutoka Bajeti ya matumizi ya kawaida ya Halmashauri zilitengwa na kutumika kupima ubora wa maji pamoja na wingi wa maji (Yield) yake katika chemchem 12 pamoja na vyanzo vingine vya maji katika Jimbo la Tabora Kaskazini na kubaini pia kuwa maji haya yanafaa kwa matumizi ya binadamu. 3 Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) [NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (TAMISEMI)] Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa maeneo hayo katika kutoa huduma ya maji katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013, ilitenga na kuidhinisha shilingi 100,000,000/= ambazo zilitumika kuimarisha chemchemi ya Isikizya, Ndono, Lende na Goweko ambapo jumla ya wakazi 1,500 wananufaika na huduma ya maji kutoka katika miradi hii. MHE. ISMAIL A. RAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Je, anaweza kulifahamisha Bunge hili Tukufu na wananchi wa Tabora ule mradi kabambe wa kutoa maji kutoka Lake Victoria mkakati wake umefikia wapi? WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kufanya upembuzi, usanifu wa mradi huo wa kutoa maji kutoka bomba la Lake Victoria mpaka Shinyanga na kupitia Nzega hadi Tabora inaendelea. Hatua ya kwanza ya kutathmini kama inawezekana kufanya hivyo imekamilika na gharama za kutekeleza mradi huo zinajulikana sasa na Serikali inahangaikia kupata fedha ili mradi huo utangazwe na uanzwe kujengwa. Na. 160 Ushiriki wa Vijana Kwenye “Big Brother Africa” MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:- (a) Je, Serikali inahusikaje katika ushiriki wa Vijana wa Tanzania kwenye mashindano ya “Big Brother Africa”? (b) Je, kuna faida gani kwa Taifa kutokana na ushiriki wa vijana kwenye mashindano hayo? 4 Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) NAIBU WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haihusiki moja kwa moja na ushiriki wa vijana katika mashindano ya mchezo wa “Big Brother Africa” bali inatambua uwepo wa mashindano ya “Big Brother Africa” yanayoendeshwa na Kampuni ya “Multichoice” ya Afrika ya Kusini yenye tawi lake hapa nchini. Kama walivyo vijana wengine wanaoshiriki Mashindano haya kutoka nchi mbalimbali za Afrika, vijana kutoka Tanzania hujaza fomu za ushiriki kupitia kwenye mitandao kama vijana wengine kwa utashi wao binafsi. Mchakato wote wa ushiriki wa vijana wanaoomba hufanywa na Multichoice Africa. (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wanaoshiriki mbali na kuzitangaza nchi wanazotoka, hutangaza vivutio vilivyo katika nchi zao ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vya utalii na maliasili. Hivyo Vijana wa Tanzania wanaoshiriki Mashindano haya; wameitangaza Tanzania na maliasili zake katika ramani ya Dunia. Kwa wale waliofanikiwa kuingia katika hatua za ushindi wamepata zawadi za fedha taslimu ambazo zimewasaidia kuboresha maisha yao. Aidha Mashindano hayo huwezesha vijana kufahamiana, kuvumiliana, kujifunza na kujenga urafiki miongoni mwao licha ya kuwa na tamaduni zinazotofautiana. 5 Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuuliza maswali mawili mengine ya nyongeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu lake Mheshimiwa Waziri amesema Serikali haihusiki moja kwa moja, lakini anaonesha ni namna gani Serikali inavyohusika. Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Serikali ya Uganda imepitisha sheria inayokataza vipindi, uandishi na mavazi yenye kuchochea ngono na tayari Rais Museveni amesaini. Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini Serikali ya Tanzania inawaachia vijana hawa kushiriki mashindano ambayo yanaonekana au mwonekano wake mkubwa ni kushadidia vitendo vya ngono na ufuska? Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Hivi Mheshimiwa anasema kwamba washiriki wale wanatangaza vivutio vya utalii, ilihali Watanzania wote ni mashahidi kwamba vitendo vinavyoonekana pale ni vya kuchochea ngono, ukahaba na ufuska. Je, Serikali inatumia vigezo gani pale inapotumia Jeshi la Polisi kuwakamata dada poa na kaka shughuli ilihali ikiwaachia vijana wa Tanzania wakipeperusha bendera ya Watanzania kwenye mashindano ambayo maadili yake makubwa ni kushadidia ngono, ufuska na ufisadi? NAIBU WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, maelezo yangu ya awali yameonyesha ni namna gani ambavyo Serikali haihusiki. Lakini Serikali inatambua vijana wale wanaoshiriki kwa maana vijana hawa hujaza fomu zile kupitia katika mitandao na mashindano haya yanasimamiwa na Multichoice Africa ambao wana tawi lao hapa Tanzania. 6 Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) [NAIBU WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO] Nimeeleza zile faida za msingi ambazo Mtanzania yoyote anayechaguliwa afike pale awe anajua Kiingereza awe na umri usiopungua miaka 18 lakini kueleza wenzake vivutio vya utalii vilivyopo hapa. Pamoja na kasoro zote zinazoonekana wapo Watanzania karibu 3 nao walitolewa kwa sababu ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge nakubaliana naye. Tunaweza tukapima faida na hasara lakini chang amoto zinazojitokeza, Serikali itazifanyia kazi na itatoa taarifa juu ya kuendelea kwa vijana wetu kushiriki ama la. (Makofi) Pili, nakubaliana naye kwamba wapo washiriki wa nchi mbalimbali wameweza kufedhehesha nchi zao kwa kushiriki ngono katika mashindano haya. Naomba tu kutumia nafasi hii kusema kwamba kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi tumeyapokea tunayafanyia kazi na tutatoa tamko. (Makofi) Na. 161 Kuboresha Hospitali ya Muhimbili MHE. RICHARD M. NDASSA (K.n.y. MHE. RITA L. MLAKI aliuliza:- Hospitali ya Muhimbili ndio hospitali kubwa ya Rufaa Dar es Salaam na nchi nzima na wagonjwa wengi mpaka wanakosa mahali pa kulala na kulazwa chini:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha hospitali hiyo ili angalau ipatikane nafasi ya kulala wagonjwa na vitanda? (b) Je, ni uwiano gani wa Daktari kwa kuona wagonjwa kwa siku ili kuhakikisha kuwa kuna Madaktari wa kutosha? (c) Je, Serikali inatenga fedha kiasi gani kwa mwaka kwa ajili ya kuhudumia hospitali hiyo kwa matumizi mbalimbali kama dawa, chakula na magari? 7 Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rita Louise Mlaki, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango wa kujenga jengo la kutolea huduma kwa wagonjwa wanaotaka huduma binafsi ambalo litakuwa na vitanda 200. Jengo hili litaongeza upatikanaji wa nafasi za kulaza wagonjwa wengine.