6 MEI, 2013 MREMA 1.Pmd
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
6 MEI, 2013 BUNGE LA TANZANIA ________________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________________ MKUTANO WA KUMI NA MOJA Kikao cha Kumi na Tisa – Tarehe 6 Mei, 2013 (Mkutano Ulianza Saa 3.00 Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge tukae. Waheshimiwa, mtakuwa mmepata Supplementary Order Paper, halafu na ile paper ya kwanza Supplementary hiki ni Kikao cha 19, wameandika 18 ni Kikao cha 19. Kwa hiyo, mtakuwa na Supplementary Order Paper. Katibu tuendelee? HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati Zifuatayo Ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014. 1 6 MEI, 2013 MHE. AUGUSTINO M. MASELE (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA): Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013 Pamoja na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014. MHE. GRACE S. KIWELU (K.n.y. MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI WA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI): Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014. MASWALI NA MAJIBU Na. 145 Wajibu wa Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji MHE. MARIAM R. KASEMBE (K.n.y. MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA) aliuliza:- Msingi mkubwa wa Maendeleo ya Jamii huanzia kwenye ngazi ya Mitaa na Vijiji ambapo hutegemea ubunifu na utendaji wa Viongozi wa ngazi husika. Je, Serikali, inawezaje kuwahakikishia wananchi kwamba, Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji wanajua wajibu wao? 2 6 MEI, 2013 NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, nakubaliana kwamba, msingi wa maendeleo ya jamii unaanzia katika ngazi za chini za Serikali za Mitaa. Wasimamizi wa maendeleo katika ngazi hiyo ni Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa. Aidha ni kweli, kwamba, ili Viongozi hawa waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ni lazima wapatiwe mafunzo ya kuwajengea uwezo. Mheshimiwa Spika, Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa wana wajibu wa kusimamia Ulinzi na Usalama katika maeneo yao, kuwakilisha wananchi wao katika Vikao vya Kamati za Maendeleo za Kata na ya Wilaya na kuitisha na kuongoza Mikutano ya Vijiji na Mitaa, kushirikiana na Maafisa Watendaji katika kuhakikisha mapato yanakusanywa na kudhibitiwa. (Makofi) Aidha kuwahamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za kijamii na maendeleo, kutunza register ya wakazi wote wa Vijiji na takwimu nyingine za maendeleo ya Vijiji, ikiwa ni pamoja na kumbukumbu za vizazi na vifo. Kusimamia masuala ya kisiasa katika maeneo yao na kutekeleza kazi nyingine watakazopangiwa na Halmashauri za Wilaya. Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa zinazoikabili Serikali, hasa katika kutekeleza Sera ya Ugatuaji wa Madaraka kwa wananchi ni ushiriki mdogo wa jamii katika shughuli za kijamii na maendeleo. Mahudhurio hafifu ya wananchi katika vikao vya maamuzi na ukusanyaji na usimamizi dhaifu wa mapato. Aidha, katika ngazi ya Vijiji na Mitaa kumekuwa na tatizo la utunzaji wa vitabu vya mahesabu, uandaaji wa Taarifa za Mapato na Matumizi na Taarifa ya Utekelezaji wa majukumu ya Kijiji na Mtaa. 3 6 MEI, 2013 Pia masuala ya utawala bora, hasa uwazi na uwajibikaji, uadilifu ni miongoni mwa maeneo yanayolalamikiwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hizi ni wazi kwamba, upo umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwajengea uwezo Wenyeviti na Watendaji wengine wa Vijiji na Mitaa. Serikali, imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kuwa Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa wanajengewa uwezo, ili kujua majukumu yao. Mara baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2009, kila Halmashauri ilitoa mafunzo kwa Viongozi hao kuhusu majukumu yao. Aidha, Serikali, imekuwa ikipeleka 40% ya fedha za kujenga uwezo katika Vijiji na Mitaa, ambapo 50% ya fedha hizo hutumika kwa ajili ya kujenga uwezo wa Wenyeviti na Watendaji wa Vijiji na Mitaa. Pamoja na jitihada hizi za Serikali, baadhi ya Halmashauri kupitia mapato ya ndani, zimekuwa zikitenga fedha kwa ajili, ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa Vijiji na wale wa Mitaa. Mheshimiwa Spika, Serikali, itaendelea kuwajengea uwezo Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa, kadiri hali ya kifedha itakavyokuwa inaruhusu. (Makofi) MHE. MARIAM R. KASEMBE: Mheshimiwa Spika, aHsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwa kuwa, katika majibu ya msingi Mheshimiwa Waziri, amesema kwamba, imekuwa ikipeleka 40% katika Halmashauri zetu kwa ajili, ya mafunzo ya Viongozi wetu wa Vijiji. Je, Wizara imekuwa ikifuatiliaje kuhakikisha kwamba, 40% hii inayokwenda ni kweli, Wenyeviti wa Vijiji pamoja na Wenyeviti wa Vitongoji wamekuwa wakipatiwa mafunzo hayo? Kwa sababu, nina uhakika katika Halmashauri nyingine, mafunzo haya Wenyeviti huwa hawapewi. 4 6 MEI, 2013 Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa nini, sasa, kwa kuwa, suala hili la kupewa mafunzo hawa Wenyeviti wa Vijiji ni la msingi sana. Kwa nini sasa Serikali, isiziruhusu Halmashauri kutenga fedha kwenye Bajeti yetu kutokana na makusanyo tunayokusanya, ili mafunzo haya ya Watendaji wa Vijiji, Vitongoji, waweze kuyapata kwa uhakika, kulikoni hali ilivyo hivi sasa? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kasembe, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, utaratibu ambao tumeweka katika Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za MItaa, na kwa sasa tunapozungumza hapa, na nimshukuru sana dada yangu Kasembe, kwa hili analozungumza. Tumeimarisha Sekretarieti zetu. Tunachofanya sisi ni kwamba, tunaye hapa mtu anayesimamia masuala ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika Sekretarieti. Pale kwa Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala na yeye anahusika katika jambo hili, lakini sisi kama centre, kwa maana ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, mmetuona tunakwenda mpaka kule chini Kijijini. Mheshimiwa Spika, na kupitia katika Taarifa za CAG, ambaye huwa anaangalia kama zimetengwa hizi hela zinazozungumzwa hapa 40%, ambayo Mheshimiwa Kasembe anazungumzia, tunakwenda mpaka kule na tumefika mahali tunaanza hata kuchukua hatua kwa wale ambao wameacha kupeleka hii 40% inayozungumzwa hapa. Na 40% inayozungumzwa hapa ni ile ya kujenga uwezo ndio inazungumza hapa. 5 6 MEI, 2013 Mimi nataka nikuthibitishie, mimi mwenyewe hapa, Mheshimiwa Waziri wa Nchi pamoja na Waziri Mkuu na mwenzangu, tumekuwa tunakwenda katika Halmashauri kufuatilia, kuhakikisha kwamba, zinakwenda hizi hela. Sasa nataka nikubaliane na Mheshimiwa kwamba, inawezekana kabisa kwamba, kuna maeneo mengine haziendi. Waheshimiwa Wabunge, tunaomba mtupatie orodha ya Halmashauri ambazo hazipeleki hizi hela kule, halafu sisi tutachukua hatua; hilo la kwanza. Mheshimiwa Spika, la pili. Hili la kupewa mafunzo; jana tulikuwa na Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na wako hapa wanajua, tumetoka Hombolo, tumetoka kwenda kuzungumzia jambo hili. Halmashauri zinatakiwa zitenge hela, zichukue hawa watendaji wetu wa Vijiji na Wenyeviti wa Vijiji, wawapeleke mpaka Hombolo kule, waende wakasome. Mheshimiwa Spika, kwa sababu, ya hali hii inayosemwa, tunachokifanya, tumefanya semina. Baada ya kumaliza Uchaguzi Mkuu, tulijua kwamba, walio wengi pale uwezo wao ni mdogo kwa hiyo, tukapanga semina. Nawaomba Wabunge, kama mnafahamu kwamba, kuna semina ambayo haikufanyika katika ngazi hiyo tunayozungumza hapo, mtusaidie. Mheshimiwa Spika, jana tumetoa maelekezo, tumesema Halmashauri zote ambazo hazijalipia kule Hombolo, tumeomba tupewe orodha yao. Na leo nimeomba saa 7.00 iwe pale Ofisini, ili tushuke na hawa ambao hawapeleki hizo hela kule Hombolo. (Makofi) MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa kunipa nafasi. Nianze ku-declare interest kwamba, mimi nimeshawahi kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa. 6 6 MEI, 2013 Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri, amejaribu kueleza kwa undani na kwa kirefu juu ya hatua za Serikali. Lakini nataka nimwulize Mheshimiwa Waziri kwamba, ni lini kweli kabisa, Serikali, itaamua kwa dhati kabisa kutekeleza majukumu ya kuwawezesha Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa na Vitongoji kwa kuwapa vitendea kazi, posho pamoja na kuhakikisha kuwa, mafunzo haya yanafanyika? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bwanausi. Sio tu kwamba, amekuwa Mwenyekiti wa Mtaa, amekuwa Mstahiki Meya wa Temeke kule kwa hiyo, anajua. Huyu anayezungumza hapa anajua sana haya mambo yanayozungumzwa hapa. Mheshimiwa Spika, mimi nitoe picha kidogo hapa na wala hapa sitaki ku-dismiss kwamba, Wenyeviti wa Vitongoji na Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa, wamefanya kazi kubwa sana katika nchi yetu. Hizi shule tunazozungumza hapa zilizojengwa wao ndio wamejenga, hizi barabara tunazozungumza hapa ndio wanaosimamia; Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, inatambua juhudi zinazofanywa na Wenyeviti wetu wa Vijiji na Vitongoji na tunawapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya. Mheshimiwa Spika, sasa tunaulizwa habari ya posho hapa; ni kweli tumezungumza na juzi tulijibu hapa. Nataka nitoe picha, Vitongoji tulivyonavyo katika Tanzania hapa, tunavyo Vitongoji 60,000 Vijiji