1 Bunge La Tanzania
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ______________ MAJADILIANO YA BUNGE ______________ MKUTANO WA KUMI NA MBILI Kikao cha Nane – Tarehe 20 Juni, 2008 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Samuel J. Sitta) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU Na. 67 Ujenzi wa Barabara ya Bunambiyu Hadi Mhunze Kupitia Idukilo MHE. FRED MPENDAZOE TUNGU aliuliza:- Kwa kuwa, katika mwaka wa fedha 2007/2008 Serikali ilitoa shilingi milioni 270 kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya kutoka Bunambiyu hadi Mhunze kupitia Idukilo; na kwa kuwa, ujenzi huo ulikadiriwa kugharimu shilingi milioni 840/=. Je, Serikali haioni ni busara kutoa kiasi cha fedha kilichobaki (Shilingi milioni 570) mapema ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni muhimu sana? NAIBU WAZIRI TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fred Mpendazoe, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu inahudumia sehemu ya barabara kutoka Bunambiyu kupitia Idukilo na kuishia kijiji cha Ngundangali, Sehemu ya kutoka Ngundangali hadi Mhunze yenye urefu wa Km.8 inahudumiwa na Wakala wa barabara yaani TANROADS. 1 Katika mwaka 2006/2007 Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu iliwasilisha maombi ya shilingi milioni 840 kwa ajili ya kujenga Km.52 za barabara kwa kiwango cha changarawe kutoka Bunambiyu hadi Ngundangali kupitia Idukilo. Kutokana na ufinyu wa Bajeti Serikali kupitia Program ya Usafiri katika Halmashauri (Local Government Transport Program) ilitoa kiasi cha shilingi milioni 270 kwa ajili ya matengenezo ya sehemu korofi katika Km.23 za barabara hiyo yenye urefu wa Km.52 kuanzia kijiji cha Bunambiyu hadi kijiji cha Ngundangali kufanya kazi hii. Katika mwaka huu wa fedha mwaka 2007/2008 kazi zinazofanyika ni:- (i) Kuchonga barabara hiyo; (ii) Kujenga makalvati; (iii) Kuweka changarawe na mifereji ya maji; na (iv) Kazi kwa ujumla inatarajiwa kukamilika mwezi Julai 2008. Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo yenye urefu wa Km.52 na ndio maana ilitoa fedha ili barabara hiyo ianze kupatiwa matengenezo ya sehemu korofi. Mheshimiwa Spika, hata hivyo maombi ya fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara kutoka katika Halmashauri ikiwamo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ni mengi ikilinganishwa na uwezo wa kifedha wa Serikali. Serikali katika Bajeti ya mwaka 2008/2009 ya Program ya Usafiri katika Halmashauri (Local Government Transport Program), fedha zilizopangwa kupelekwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu iwapo Bajeti hiyo itapitishwa ni shilingi milioni 200, fedha hizi ni kwa ajili ya matengenezo ya sehemu korofi (Spot Improvement). Hivyo basi Halmashauri inashauriwa kuweka barabara hiyo katika vipaumbele vya Halmashauri ya Wilaya na kutumia fedha hizo kwa ajili ya matengenezo ya sehemu korofi (Spot Improvement) kwenye kipande hicho cha barabara kilichobaki chenye urefu wa Km.29 ili barabara hiyo iweze kupitika. MHE. FRED M. TUNGU: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kwa dhati kabisa nishukuru Serikali kwa kutoa hizo shilingi milioni 270 mwaka jana, ilitoa katika mazingira magumu sana na ninaomba nishukuru kwa niaba ya Wananchi wa Wilaya ya Kishapu. Mheshimiwa Spika, lakini naomba vile vile nishukuru kwa ajili ya hizi shilingi milioni 200 ambazo zipo katika Bajeti na ninaamini kwamba Serikali na Bunge litapitisha Bajeti ili hizo fedha ziende na zikatengeneze hizo Km.29 ambazo zimebaki. Mheshimiwa Spika, lakini nina swali moja dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa sehemu ya barabara ambayo imetengenezwa kutokana na fedha hizi milioni 270 ambazo zimetolewa inalalamikiwa na wananchi hasa kutokana na makalvati ambayo yamewekwa hayaridhishi na utengenezaji wa mifereji ya maji vile vile hauridhishi. 2 Je, Serikali itawahakikishia Wananchi wa Wilaya ya Kishapu hasa mahali barabara inapopita kwamba wakandarasi wanaojenga barabara hiyo hawatalipwa fedha zao za mwisho mpaka pale watakaporekebisha mapungufu yaliyojitokeza? NAIBU WAZIRI TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu kwanza kabisa naomba nichukue fursa hii kupokea shukrani za Mbunge wa Kishapu na kusema ahsante kwa ku-appreciate mchango ambao umetolewa na Serikali na ninawashukuru pia kwa niaba ya Waziri Mkuu kwamba anafurahi kuona kwamba kiasi hicho cha pesa ambacho nimekitamka hapa kimetengwa. (Makofi) Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo ningeomba nijibu swali lake hili analolizungumzia kwamba ile shughuli ambayo inaendelea pale kwa sasa hivi inaonekana kwamba haifanyiki kwa kiwango ambacho kinatakiwa na anashauri hapa kwamba tuzuie inaitwa retention money ili malipo yasifanyike mpaka tuwe na uhakika kwamba kazi hiyo imefanyika kwa kiwango kinachotakiwa. Mimi ninadhani Mheshimiwa Mbunge Fred Mpendazoe anatusaidia sana hapa, pesa za Serikali zinazoenda katika Halmashauri zetu lazima zitumike kwa utaratibu unaotakiwa na kwa kiwango na kwa ubora ambao unatakiwa. Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninamwomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kuhakikisha kwamba yeye na Baraza la Madiwani wanaenda pale na kusimamia barabara ile na kwamba inatengenezwa kwa kiwango hicho kinachotakiwa na kwa vile ametutahadharisha hapa ninaomba nitamke kwa niaba ya Serikali kwamba tutamshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu ikiwezekana tutume kikosi kutoka Wizarani hapa, kiende mpaka Kishapu kiende kikaangalie barabara hiyo kwa sababu haya ni baadhi ya matatizo ambayo tunayapata katika barabara zetu zote kwamba hazifanyiki kwa kiwango kinachotakiwa. Kwa hiyo, ninawaomba na Wabunge wenzangu wote na Halmashauri zote zihakikishe kwamba tunapokuwa tumetenga hela kwa ajili ya ujenzi wa barabara, barabara hizo zinatengezwa kwa kiwango kinachotakiwa. (Makofi) Na. 68 Mpango wa Kuimarisha Njia za Usafiri kwa Nchi za Afrika Mashariki MHE. MOHAMMED H. J. MNYAA (K.n.y. MHE. ABUBAKAR KHAMIS BAKARY) aliuliza:- Kwa kuwa moja kati ya malengo makubwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuimarisha njia za usafiri kwa Wanachama. Je, hatua hiyo imefikia wapi na ni maeneo yapi katika nchi zipi yatanufaika na mpango huo? NAIBU WAZIRI WA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakary Khamis Bakary, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) kama ifuatavyo. 3 Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa moja kati ya malengo makubwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuimarisha njia za usafiri kwa Nchi Wanachama. Kwa sasa Nchi Wanachama zinatekeleza miradi mbalimbali iliyopewa kipaumbele na kuainishwa katika Mkakati wa Tatu wa Maendeleo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Mwaka 2006-2010. Katika Mkakati huo Mkataba wa kuimarisha njia za usafiri na uchukuzi umebainishwa. Lengo kuu la Mkataba huo ni kuunganisha Nchi Wanachama kwa kuimarisha njia za usafiri na uchukuzi ili kukuza biashara baina ya Nchi Wanachama. Mheshimiwa Spika, Hatua iliyofikiwa katika sekta ya usafiri ni kama ifuatavyo:- (a) Kazi ya uhandisi na michoro kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Arusha – Namanga – Athi river imekamilika ambapo taratibu za awali za ujenzi wa mradi huo zinaendelea vizuri, na “African Development Bank (ADB)” na “Japanese Bank for International Co-operation (JBIC)” zinafadhili mradi huo. (b) Mheshimiwa Spika, Kuhusu mradi wa barabara ya Malindi – Mombasa – Horohoro – Tanga – Sadani – Bagamoyo kazi ya upembuzi yakinifu inaendelea na lengo kuu la mradi huu ni kuwa na barabara inayounganisha bandari ya Dar es Salaam na Mombasa. Aidha, “Millenium Challenge Co-operation (MCC)” imetenga fedha kwa ajili ya barabara ya Tanga – Horohoro. (c) Mheshimiwa Spika, mradi wa usalama wa usafiri wa anga ambao unahusu kanuni za usafiri wa anga katika Nchi Wanachama unaendelea vizuri na tayari Itifaki ya kuanzisha chombo kitakachosimamia usalama wa usafiri wa anga imekwishasainiwa mwezi Aprili mwaka 2007. Menejimenti ya chombo hicho imeshateuliwa na kuanza kazi ambapo Makao Makuu ya Taasisi hii yanategemewa kuwa Entebbe, Uganda. Aidha, mradi wa kuendeleza Karume Airport Pemba umekubaliwa kuwa mmoja wa miradi itakayofadhiliwa na ADB. (d) Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Maendeleo ya Reli ya Afrika Mashariki (The EAC Railway Development Master Plan), umebainisha maeneo katika Nchi Wanachama kwa nia ya kuunganisha nchi hizo kwa maendeleo ya usafiri wa reli. Hivi sasa ripoti ya wataalam waelekezi imo katika hatua za mwisho na hivi karibuni inategemewa kuwasilishwa kwa Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki kwa maoni ili utekelezaji uanze. (e) Mheshimiwa Spika, kwa upande wa usafiri wa majini hatua mbalimbali zinachukuliwa ikiwemo kufanya utafiti kwa ajili ya kuelewa kina cha maji na njia za kuweza kupita meli katika Ziwa Victoria. Aidha, hatua za kutafuta fedha kwa ajili ya vifaa vya kuongozea meli na ukarabati wa Bandari ya Kisumu – Kenya, Mwanza – Tanzania na Port Bell – Uganda zinaendelea vizuri, pamoja na jitihada hizo, jumuiya inaendelea na taratibu za kuunganisha Ziwa Tanganyika katika mpango huo. Mheshimiwa Spika, miradi ya Zanzibar itakayoombewa ufadhili chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tayari imeshafikishwa kwenye Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na taarifa ya miradi hiyo imeshawasilishwa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa hatua zaidi. Aidha, Nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Afrika 4 Mashariki yaani Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi zitanufaika na mpango huu wa miradi kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki. MHE. MOHAMMED H. J. MNYAA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa swali la nyongeza. Kwa kuwa, njia zote alizozitaja za kuimarisha