Majadiliano Ya Bunge ______
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ______________ MKUTANO WA TATU Kikao cha Hamsini - Tarehe 24 Juni, 2016 (Bunge lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Dkt. Tulia Ackson) Alisoma Dua NAIBU SPIKA: Tukae. Katibu! NDG. CHARLES MLOKA – KATIBU MEZANI: Maswali. MASWALI NA MAJIBU Na. 424 Kuigawa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. HAMIDU H. BOBALI) aliuliza:- Jimbo la Mchinga na Mtama linaunda Halmashauri ya Wilaya ya Lindi na ukubwa wa Halmashauri hii ni kikwazo cha kuwafikia wananchi kwa urahisi katika kuwapelekea huduma za jamii. Je, kwa nini Serikali isiigawe Halmashauri hii ili kuwa na Halmashauri mbili yaani Mchinga na Mtama? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:- 1 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishwaji wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa unazingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 145 na Ibara 146 na Sheria ya Serikali za Mitaa, Mamlaka ya Wilaya, Sura Namba 287 kifungu cha 5 ambazo kwa pamoja zinampa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kuwa na Madaraka ya kuanzisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa nchini. Mheshimiwa Naibu Spika, kusudio la kugawanya Halmashauri ni lazima likidhi vigezo vinavyowekwa kwa kuzingatia taratibu zilizopo ikiwa ni pamoja na kujadiliwa kwenye vikao vya kisheria, ikiwemo Mkutano Mkuu wa Vijiji, Kamati za Maendeleo za Kata, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC), Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na baadae huwasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
[Show full text]