9Aprili,2013
9 APRILI, 2013 BUNGE LA TANZANIA ________________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________________ MKUTANO WA KUMI NA MOJA Kikao cha Kwanza - Tarehe 9 Aprili, 2013 WIMBO WA TAIFA (Hapa Waheshimiwa Wabunge Waliimba Wimbo wa Taifa) (Mkutano Ulianza Saa 3.00 Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa msimame tena. Mtakumbuka kwamba wakati wa Vikao vyetu vya Kamati, kwa bahati mbaya sana tulimpoteza mpenzi wetu Mheshimiwa Salim Hemed Khamis. Kwa hiyo, tumkumbuke kwa dakika moja. (Hapa Waheshimiwa Wabunge walisimama kwa Dakika moja kumkumbuka Mheshimiwa Salim Hemed Khamis aliyekuwa Mbunge wa Chambani Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amin. Ahsanteni sana na karibuni tukae. 1 9 APRILI, 2013 Waheshimiwa Wanbunge, katika Mkutano wa Tisa, Bunge lilipitisha Muswada wa Sheria ya Serikali uitwao The Plant Breeders` Rights Bill, 2012, kwa taarifa hii napenda kulialifu Bunge hili Tukufu kwamba, Mswada huo umekwisha pata kibali cha Mheshimiwa Rais na kuwa Sheria ya nchi iitwayo: The Plant Breeders` Rights Act, 2012 Na. 9 ya mwaka 2012. Kwa hiyo, ule sasa ni sheria ya Nchi. HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati ifuatayo iliwasilishwa Mezani na:- WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kuwasilisha mezani Taarifa ya Matoleo yote ya Gazeti la Serikali pamoja na nyongeza zake zilizochapishwa tangu Kikao cha mwisho cha Mkutano wa Bunge uliopita. Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. MASWALI NA MAJIBU Na. 1 Kujenga Barabara ya Old Moshi kwa Lami MHE. GODFREY W. ZAMBI (K.n.y. MHE. DKT. CYRIL A. CHAMI) aliuliza:- Je, Serikali itatekeleza lini ahadi ya kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Old Moshi inayoanzia Kiboriloni kupitia Kikarara, Tsuduni hadi Kidia? 2 9 APRILI, 2013 NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt.
[Show full text]