20 MAY 2019.Pmd
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA KUMI NA TANO Kikao cha Thelathini na Moja – Tarehe 20 Mei, 2019 (Bunge Lilianza saa Tatu Asubuhi) DUA Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea na Mkutano wetu wa 15, leo kikao cha 31. Katibu! NDG. RAMADHAN ISSA ABDALLAH – KATIBU MEZANI: TAARIFA YA SPIKA SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, nasikitika kuwatangazia kifo cha mwanasiasa mkongwe na kiongozi aliyepata kuhudumia kwa muda mrefu hasa kule kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Ally Juma Shamhuna. Waheshimiwa Wabunge, katika uhai wake, marehemu Ally Juma Shamhuma amepata kushika nyadhifa mbalimbali zikiwemo hizi zifuatazo; amepata kuwa Mkurugenzi wa Mifugo, amewahi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, amewahi kuwa Katibu Mkuu, Export Processing Zone Zanzibar, amewahi kuwa Waziri wa Mipango, amekuwa Waziri wa Nchi, Afisi ya Waziri Kiongozi, aliwahi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo na wakati huo huo akiwa ni 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Naibu Waziri Kiongozi, katika uhai wake amekuwa Waziri wa Ardhi, Maji na Nishati na alipata kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali. Aidha, Marehemu Mheshimiwa Shamhuna kwa muda mrefu alikuwa ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi kutokea Zanzibar na baadhi yenu humu Wabunge mtamkumbuka marehemu Mheshimiwa Shamhuna kama Mbunge wa Bunge la Katiba na alikuwa Mjumbe wa Kamati namba 8 kwenye Bunge la Katiba, Kamati ambayo nilikuwa Mwenyekiti wake. Kwa niaba yenu Waheshimiwa Wabunge, tunatoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Tunatoa pole kwa Wazanzibari wote na Watanzania wote kwa ujumla kufuatia kifo hicho na tunamuomba Mwenyezi Mungu aihifadhi roho yake mahali pema peponi, amina.
[Show full text]