Majadiliano Ya Bunge ______
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA __________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA PILI Kikao cha Sita - Tarehe 14 Februari, 2006 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Samuel J. Sitta) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA MASOKO: Taarifa ya Mwaka na Hesabu za Shirika la Viwango Tanzania kwa mwaka ulioishia Tarehe 30 Juni, 2003 (The Annual Report and Accounts of the Tanzania Bureau of Standards (TBS) for the Year ended 30th June, 2003). NAIBU WAZIRI WA MIUNDOMBINU (MHE. DR. MAUA A. DAFTARI): Taarifa ya Mwaka na Hesabu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwa Mwaka ulioishia tarehe 30 Juni, 2005 (The Annual Report and Accounts of the Tanzania Communications Regulatory Authority for the Year ended 30th June, 2005). MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kabla sijamwita muuliza swali wa kwanza kwa siku ya leo, naomba niwatakie heri wale wote ambao wanaitambua siku ya wapendanao. Kipekee nawatakia heri wale wote ambao wanapenda lakini hawapendwi na wale wote ambao hali ya mapenzi imelegalega. (Kicheko/Makofi) Na. 59 Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:- 1 Kwa kuwa Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani kipo katika Jimbo la Ubungo, na kwa kuwa Kituo hicho kinatoza aina mbalimbali za ushuru:- Je, wakazi wa Jimbo la Ubungo wanafaidika vipi na mapato yanayopatikana kutoka katika Kituo hicho? NAIBU WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima J. Mdee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani kipo katika Jimbo la Ubungo. Kituo hicho kilianza Desemba, 1999 na kilikabidhiwa kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam mwaka 2000. Aidha, kazi za Kituo hiki ni kutoza ushuru mbalimbali hususan ushuru wa kulaza mabasi, kutumia kituo, wasindikizaji, kodi ya pango, kodi ya mabango, kodi ya vioski na kadhalika. (Makofi) Mheshimiwa Spika, kutokana na kodi zinazotozwa, wakazi wa Ubungo wanaendelea kufaidika na mapato ya kituo hicho katika nyanja mbalimbali kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, kwa upannde wa usafi, Jiji la Dar es Salaam linatoa huduma za usafi kwa Manispaa zote tatu likiwamo Jimbo la Ubungo na Halmashauri ya Jiji inatoa mitambo na magari kuhudumia maeneo ya Tandale Sokoni, kizimba kilichopo barabara ya Sam Nujoma na Mburahati kwa Jongo. Mheshimiwa Spika, elimu, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imesaidia kugharamia ujenzi wa Maabara ya Shule ya Sekondari Kiluvya na imenunua madawati kwa ajili sekondari hiyo. Mbeshimiwa Spika, kwa upande wa biashara na uchumi, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imechangia na kuboresha kituo cha uchongaji wa vinyago kilichoko Mwenge ambapo kimelipa umeme jumla ya shilingi milioni 3.5. (Makofi) Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ajira, kama tunavyoelewa kwamba Kituo cha Mabasi cha Ubungo kinafunguliwa saa 10.30 alfajiri na kinafungwa saa 4.00 usiku. Kutokana na kuwepo kwake ndani ya Jimbo la Ubungo, kituo hicho kimetoa ajira kwa wakazi zaidi ya 1,000 na zaidi ya nusu ya waajiriwa hao ni wakazi wa Jimbo la Ubungo. Pia eneo hilo kwa sasa hivi lina thamani kubwa sana kwa sababu hoteli za kisasa zimejengwa kama vile Landmark, Royal Kibadamo na Ubungo Plaza. (Makofi) 2 Mheshimiwa Spika, kwa upande wa miundombinu, Halmashauri ya Jiji imejenga daraja la Kiluvya ili kuwarahisishia wakazi wa Kiluvya kwenda maeneo mengine bila kupata adha yoyote. (Makofi) MHE. JAMES P. MUSALIKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Kituo hiki kinasaidia na kinahudumia wasafiri wote wa nchi nzima, lakini kwa kuwa pia kuna wapigadebe ambao Serikali imesema wasiwepo na wanakera na wanasababisha wizi. Je, Serikali inatamka nini kuhusu kuwepo kwa wapigadebe ambao wanasabaisha matatizo kwa wasafiri kutoka Mikoa ya Bara? NAIBU WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, tatizo la wapigadebe linafahamika katika vituo vyote vya mabasi katika nchi nzima. Serikali inaweka utaratibu kwa hao wapigadebe ili wafahamike ni watu gani ambao wanaweza kufanya kazi hiyo ya usindikizaji. Kwa hiyo, zinatafutwa sheria ili kuwalinda hao wapigadebe kuhakikisha kwamba hao wasafiri hawapati adha kutokana na wapigadebe hao. (Makofi) Na. 60 Udhibiti wa Takataka MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:- Kwa kuwa maeneo mengi ya Mjini yamekithiri kwa uchafu unaotupwa na wananchi wenyewe, mfano mifuko ya plastiki maarufu kama rambo:- (a) Je, Serikali ina mkakati au mpango gani wa kudhibiti takataka hizo hasa zile za mifuko ya plastiki? (b) Je, Serikali itafanya nini kuhakikisha kila mwananchi anaweka eneo lake safi? (c) Je, Serikali itafanya nini kuhakikisha kuwa madampo yanayojaa uchafu yanasafishwa kwa wakati ili kuondoa kero ya harufu mbaya inayotokana na uoza wa taka wa muda mrefu? WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MAZINGIRA alijibu: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan A. J. Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:- (a) Hatua ya kwanza iliyochukuliwa na Serikali kudhibiti tatizo la mifuko ya plastiki ni kuweka ushuru kwenye mifuko hiyo kwa madhumuni ya kupunguza utumiaji wake. 3 Hatua ya pili ni kuwezesha uingizaji, utengenezaji na matumizi ya mifuko mbadala. Matarajio ni kwamba watumiaji wakuu na wananchi kwa ujumla wataanza kuona gharama kutumia mifuko ya plastiki na hivyo kutumia vifaa mbadala. Mheshimiwa Spika, hatua zingine zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ni pamoja na kuhamasisha viwanda vinavyozalisha bidhaa za plastiki vijihusishe zaidi na kurejeleza taka za aina hiyo, kuhamasisha Asasi na vikundi mbalimbali visivyo vya Kiserikali katika kurejeleza bidhaa zitokanazo na plastiki ili kutengeneza vifaa mbalimbali kama vile madawati ya shule, meza na mabomba ya maji na yale ya kupitisha nyaya za umeme, kuhimiza mifumo madhubuti katika Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji ya kukusanya, kutenganisha na kurejeleza taka ikiwa ni pamoja na kuweka vyombo maalum vya kukusanyia taka za plastiki na kuanzisha vituo na maghala ya kukusanyia taka za mifuko ya plastiki na nyinginezo za plastiki zikisubiri kurejelezwa. (Makofi) Mheshimiwa Spika, hatua ya kuweka ushuru wa asilimia 15 kwenye mifuko ya plastiki inayoingizwa nchini imepunguza kiasi uingizaji wa aina hii ya palastiki kwa asilimia 50. (b) Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, sheria Na. 20 ya mwaka 2004 katika kifungu cha 122 inataka kila mmiliki au mkazi wa eneo lolote kuweka mazingira yake safi na kwa wakati wote. Akishindwa kufanya hivyo anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria. Mtu yeyote atakayetupa takataka hovyo hovyo au kushindwa kusafisha mazingira yake au kuweka eneo lake katika hali ya usafi, chini ya kifungu 190 cha sheria hiyo atatozwa faini isiyozidi shilingi milioni moja. (c) Sheria ya Serikali za Mitaa Na.7 na Sheria ya Serikali za Mitaa Na.8 zote za mwaka 1982 zinazipa Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji jukumu la kukusanya na kuondoa takataka katika maeneo ya umma, maeneo yanayomilikiwa na watu binafsi, taasisi, viwanda na biashara. Mheshimiwa Spika, wajibu wa kwanza wa kutunza mazingira ni wa mwananchi anayeishi katika mazingira hayo. Serikali kwa upande wake kupitia Serikali za Mitaa itaendelea na juhudi za kuboresha ukusanyaji wa taka ngumu na taka za maji maji. Aidha, Serikali itaendelea na jukumu la kukuza weledi na kujenga hamasa ili jamii ya Kitanzania ikabiliane na tatizo la takataka zinazotupwa hovyo zenye athari kwa mazingira, mandhari na afya kwa binadamu na mifugo. Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi ya kumjibu Mheshimiwa Susan A. J. Lyimo Mbunge wa Viti Maalum, kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa na wananchi na wengine kuteuliwa na Mheshimiwa Rais. Nawashukuru kwa dhati kabisa wananchi wa Rungwe Mashariki kwa kunichagua tena bila kupingwa kuwa Mbunge wao. Imani hiyo ni kubwa na ni deni kwangu linaloweza kulipwa kwa utumishi kwao na kwa Watanzania wote. (Makofi) 4 MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Lakini nina swali moja dogo la nyongeza. Pamoja na kwamba Waziri amesema kwamba mifuko ya plastiki imewekewa ushuru ili kupunguza matumizi, lakini bado amesema ni asilimia 50 tu katika punguzo hilo. Je, haoni kwamba kuna umuhimu wa Wizara yake kuleta Muswada Bungeni ambao utahakikisha kwamba mifuko ya plastiki inazuiliwa? WAZIRI NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, tunaangalia hatua mbalimbali nyingizo za kuchukua kama Serikali ili kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la mifuko ya plastiki. Pamoja na hiyo tutaangalia uwezekano wa kuzuia uingizaji wa aina ya plastiki mbalimbali. Lakini hili lazima tulifanyie kazi kwa sababu linaweza kuathiri biashara. Tuangalie makubaliano na nchi nyingine. Lakini tutachukua hatua ambazo haihitaji kuzitangaza hapa kwa sababu tuna mamlaka ya kufuta uingizaji. (Makofi) MHE. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante na namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri. Lakini naomba niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:- Kuhusiana na takataka, kwa sasa hivi kwanza tunapongeza juhudi za Serikali kwa kuwahusisha watu binafsi na vikundi vya watu kufanya biashara ya kubeba taka. Lakini kutokana na hali ya usalama barabarani na magari ambayo yanatumika kwa uwezo wao mdogo. Je, Mheshimiwa Waziri asingeona ni wakati mzuri wa kupata hata kama grants kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara hao ili waweze kupata magari mazuri ya kuwawezesha kubeba takataka