MKUTANO WA KUMI NA MOJA Kikao Cha Tano – Tarehe 9 Aprili, 20
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________ MKUTANO WA KUMI NA MOJA Kikao cha Tano – Tarehe 9 Aprili, 2018 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. (Makofi) (Hapa Wabunge walipiga makofi kumshangilia Spika kwa kurejea Bungeni) SPIKA: Ahsanteni sana Waheshimiwa Wabunge. Katibu tuendelee. NDG. STEPHEN KAGAIGAI – KATIBU WA BUNGE: HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, kwa kweli, niivunje tu Kanuni yako na mimi niseme tunafurahi kukuona. Karibu sana Bungeni. (Makofi) Taarifa za Matoleo ya Magazeti pamoja na Nyongeza zake zilizochapishwa tangu Kikoa cha Mwisho cha Mkutano wa Bunge uliopita kama ifuatavyo:- 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) (i) Toleo Na. 05 la tarehe 02 Februari, 2018; (ii) Toleo Na. 06 la tarehe 09 Februari, 2018 (iii) Toleo Maalum Na. 03 la tarehe 13 Februari, 2018; (iv) Toleo Na. 07 la tarehe 16 Februari, 2018; (v) Toleo Na. 08 la tarehe 23 Februari, 2018; (vi) Toleo Na. 09 la tarehe 02 Machi, 2018; (vii) Toleo Na. 10 la tarehe 09 Machi, 2018; (viii) Toleo Na. 11 la tarehe 16 Machi, 2018; na (ix) Toleo Na. 12 la tarehe 23 Machi, 2018. Mheshimiwa Spika, aidha, naomba kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba nakala za magazeti haya zimeshasambazwa na zimetolewa pia kwa mfumo wa nakala tete. Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi, tunakushukuru sana. Katibu. NDG. STEPHEN KAGAIGAI – KATIBU WA BUNGE: MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Tunaanza na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum. Na. 34 Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa – Mkoa wa Simiyu MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:- Mkoa wa Simiyu ambao ni mkoa mpya hauna Hospitali ya Rufaa, hivyo wagonjwa wanalazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 140 kufuata huduma hiyo katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Shinyanga na Mwanza; mwaka 2015/2016 Mkoa wa Simiyu ulipokea fedha kidogo ya kuanzisha jengo la OPD. 2 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) (a) Je, Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa? (b) Je, ni lini Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo? NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kukukaribisha tena katika Bunge letu tukufu. Tumefurahi sana kukuona. (Makofi) Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, awali ya yote, Wizara inapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kwa kutambua jitihada ambazo Serikali imefanya katika kuendeleza mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, ukiwa ni mmoja wa mikoa mipya ulioanzishwa mwaka 2012. Kutokana na uhitaji wa huduma za afya ngazi ya rufaa katika ngazi ya mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu iliandaa na kupeleka andiko Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa kwa kuzingatia mahitaji ya kitabibu kwa ajili ya kuingizwa kwenye bajeti. Mheshimiwa Spika, niongeze hapa tu kwamba, pamoja na andiko hili hospitali hii sasa kwa agizo la Mheshimiwa Rais, zimeletwa tena katika Wizara ya Afya. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa fedha na hadi sasa jumla ya shilingi 2,087,268,672 zimeshatolewa. Kati ya fedha hizo, shilingi 299,896,185 zilitumika kununua ardhi yenye ukubwa wa ekari 121. Shilingi milioni 595,650,815 zilitumika katika ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na utawala katika awamu ya 3 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) kwanza na shilingi 1,191,721,672 zilitumika kuendeleza ujenzi wa jengo la OPD katika awamu ya pili. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga fedha zaidi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za tiba katika Hospitali za Rufaa za mikoa ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Simiyu. Hii inaenda sambamba vilevile na kupatiwa ahadi ya fedha ya shilingi bilioni 10 ambayo zilitolewa na Mheshimiwa Rais alipotembelea Mkoa wa Simiyu tarehe 11 Januari, 2017. SPIKA: Mheshimiwa Leah Komanya, swali la nyongeza. MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, Mheshimiwa Rais alipotembelea Mkoa wa Simiyu mapema Januari, 2017 baada ya kuona maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa, kwanza hakuridhishwa na bajeti iliyotengwa ya shilingi bilioni 38 ya kujenga Hospitali ya Mkoa. Hivyo, akasema hospitali hiyo ijengwe kwa shilingi bilioni 10 na kwamba akatoa ahadi zitolewe shilingi bilioni 10 ili mwaka 2019 aje kuzindua hospitali hiyo. Mpaka sasa ni jengo la OPD tu ndilo lililokamilika na 2017 mpaka leo hakuna fedha yoyote iliyoletwa na Serikali. SPIKA: Mheshimiwa Leah, swali sasa. MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, naomba commitment ya Serikali kuhusiana na ahadi ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Spika, swali langu dogo la pili; tunayo Hospitali Teule ya Somanda, hospitali hiyo ina changamoto. Madaktari wanaohitajika ni 22, waliopo ni wanane, lakini hao wanane hawana examination room, hamna Mganga wa Usingizi wala hakuna casuality room. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha hospitali hiyo teule ya mkoa ili wananchi wa Mkoa wa Simiyu wasihangaike kwenda Mkoani Mwanza? 4 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa maswali mawili ya Mheshimiwa Leah Komanya; na nimpongeze kwa kufuatilia afya na maendeleo ya wananchi wa Simiyu. Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu kwamba, Mheshimiwa Rais mwishoni mwa mwaka 2017 alikabidhi hospitali zote za rufaa za mikoa ambazo zilikuwa zinasimamiwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuja katika Wizara ya Afya. Na sisi ndani ya Wizara ya Afya tumeshajipanga kuhakikisha kwamba hospitali hizi tunazihudumia na kuzisimamia kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti kama nilivyosema katika jibu langu la awali. Mheshimiwa Spika, niendelee kusema tu kwamba ahadi ya Mheshimiwa Rais ni commitment, nasi ndani ya Wizara tutaendelea kuisimamia kuhakikisha kwamba fedha hizo zinapatikana kwa malengo ambayo yamekusudiwa, baada ya kufanya tathmini ya kina kuangalia mahitaji halisi ya Hospitali hii ya Simiyu. Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, swali lake la pili lilikuwa ni kuhusiana na watumishi. Katika mwaka wa fedha uliopita, Serikali iliajiri watumishi 3,152 ambao tuliwagawa katika mikoa mbalimbali. Tunatambua bado tuna changamoto kubwa sana ya watumishi na tunatarajia kwamba Serikali itatoa kibali hivi karibuni na Mkoa wa Simiyu utazingatiwa katika mahitaji yake. SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, swali hili limechukua muda mwingi. Naomba tuendelee na swali la Mheshimiwa Abdallah Ali Mtolea, Mbunge wa Temeke kwa Wizara hiyo hiyo ya Afya. MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kabla ya kuuliza naomba nifanye marekebisho machache kwenye hii Order Paper maana yake imeandikwa kwamba namuuliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, 5 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) TAMISEMI lakini swali nalielekeza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto. Baada ya marekebisho hayo naomba swali hili la Wanatemeke sasa lipate majibu ya Serikali. Na. 35 Serikali Kuihudumia Hospitali ya Temeke MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:- Serikali iliipandisha hadhi Hospitali ya Temeke kuwa Hospitali ya Mkoa ambayo sasa inastahili kuhudumiwa na Wizara badala ya Halmashauri ili huduma inayotolewa hapo ifanane na hadhi ya Hospitali ya Mkoa. Je, ni lini Serikali itaanza kuihudumia hospitali hiyo kwa kiwango kinachostahili ili kuipunguzia mzigo Halmashauri? NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, ni kweli, Serikali iliipandisha hadhi Serikali ya Temeke kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Hospitali hiyo ni moja ya hospitali tatu katika Mkoa wa Dar es Salaam zilizopandishwa hadhi kuwa Hospitali za Rufaa za Mkoa ikiwa ni pamoja na Hospitali za Mwananyamala na Ilala. Lengo ni kuhakikisha kuwa huduma za afya za kibingwa zinawafikia wananchi na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Mheshimiwa Spika, katika mwendelezo wa kuboresha huduma za kibingwa kwa wananchi, tarehe 25 Novemba, 2017 Hospitali ya Temeke ni miongoni mwa hospitali 23 za 6 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Rufaa za Mikoa ambazo zilikabidhiwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka TAMISEMI wakati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizindua Hospitali ya Mafunzo ya Mloganzila. Wizara yangu imekabidhiwa hospitali hizi kutoka TAMISEMI tarehe 15 Machi, 2018. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha hospitali hii inatoa huduma kulingana na hadhi iliyopewa, Serikali imeweka vipaumbele vya kuboresha utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na:- (i) Vipaumbele vya kuongeza madaktari bingwa wanane katika fani za magonjwa ya akinamama, upasuaji, mifupa, mama na watoto na magonjwa ya ndani. Hospitali ya Temeke kwa sasa ina wataalam hao. (ii) Kuhakikisha upatokanaji wa dawa na vifaatiba. (iii) Kuhakikisha mipango ya hospitali inawekwa wakiasaidiana na Wizara katika kukarabati vyumba vya upasuaji, maabara na vyumba vya wagonjwa. Mheshimiwa Spika,