Majadiliano Ya Bunge ______
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA NANE Kikao cha Kumi na Nne – Tarehe 2 Julai, 2007 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mhe. Spika (Mhe. Samuel J. Sitta) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI. Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA): Hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) kwa Mwaka wa Fedha 2007/2008. MWENYEKITI WA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA UTAWALA: Taarifa ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu Utekelezaji wa Ofisi ya Rais (Ikulu na Menejimenti ya Utumishi wa Umma) kwa Mwaka wa Fedha 2006/2007 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2007/2008. SPIKA: Nakushangaa Mwenyekiti George Malima Lubeleje, umenunanuna na hali jana Waziri Mkuu alikuwa katika Jimbo lako. (Kicheko/Makofi) MSEMAJI WA KAMBI YA UPINZANI OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA (MHE. SHOKA KHAMIS JUMA): Maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Utekelezaji wa Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) kwa mwaka wa Fedha uliopita, pamoja na Maoni ya Upinzani kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka 2007/2008 1 MASWALI NA MAJIBU Na. 116 Majengo Yaliyokuwa ya Wapigania Uhuru Kongwa MHE. HAFIDH ALI TAHIR aliuliza: - Kwa kuwa Tanzania imesifika na inaendelea kusifika kwa kusimamia Amani na kujitolea mhanga katika kupigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika; na kwa kuwa eneo la Kongwa, Mkoani Dodoma ni sehemu iliyotumika kuwahifadhi wapigania uhuru toka Msumbiji, Namibia na Afrika Kusini na yapo majengo yaliyotumiwa na wapigania uhuru hao:- (a) Je, Serikali imeyatunzaje majengo hayo ili yawe kielelezo kwa vizazi vya nchi hizo na Tanzania kwa ujumla? (b) Je, wananchi wa eneo hilo la Kongwa wamefaidika vipi na uhifadhi wa wapigania uhuru hao baada ya nchi zao kujitawala? (c) Je, viongozi wangapi waliowahi kuhifadhiwa katika eneo la Kongwa au waliofuata baada yao wamewahi kulitembelea eneo hilo? SPIKA: Waheshimiwa Wabunge wengine mtakaouliza maswali hamtatoa salamu za aina hiyo kwa sababu mchakato huo bado unaendelea na kwa kila jimbo. (Makofi) NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, MAAFA NA KAMPENI DHIDI YA UKIMWI alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir, Mbunge wa Dimani, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba katika eneo la Kongwa mkoani Dodoma yapo majengo ambayo yaliwahi kutumiwa na wapigania uhuru kutoka nchi za Kusini mwa Afrika hadi mwaka 1974. Baada ya hapo majengo hayo yameendelea kuhifadhiwa na Wizara au Taasisi mbalimbali za Serikali zilizokabidhiwa katika nyakati tofauti. Kwa hivi sasa majengo hayo kupitia maombi ya wananchi wa Kongwa yanatumika kama sehemu ya Shule ya Sekondari ya kutwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Maumbile (structures) ya majengo, makaburi yao na mahandaki likiwemo alilotumia Hayati Comrade Samora Machel yamebaki kama yalivyojengwa na kwa hakika ni vielelezo vinavyotumika kwa vizazi vya nchi hizo. Hivi karibuni, yaani tarehe 21 Juni, 2007, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa alipokea ugeni wa Serikali ya Msumbiji kutoka Televisheni ya Taifa ambao ulitembelea eneo hilo la kihistoria na kupiga picha. 2 Mheshimiwa Spika, wananchi wa eneo la Kongwa wanafaidika kwa kuyatumia majengo hayo kuwapatia vijana wao elimu ya sekondari hadi kidato cha nne. Aidha, mipango ya baadaye ya bodi ya shule hiyo ni kuifanya iweze kutoa elimu ya sekondari hadi kidato cha sita. Mheshimiwa Spika, viongozi waliowahi kuhifadhiwa katika kambi ya Kongwa ni pamoja na aliyekuwa Rais wa Namibia Mheshimiwa Sam Nujoma, Rais wa kwanza wa Msumbiji, Hayati Samora Machel na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa SWAPO nchini Namibia, Mheshimiwa Hifikepunye Pohamba. Viongozi waliotembelea kambi hiyo kwa madhumuni mbalimbali ni wengi wakiwemo mabalozi na wafanyakazi wengi wa nchi husika hapa nchini. Viongozi waandamizi wa majeshi na watendaji mbalimbali wa Serikali katika nchi hizo. Aidha, kati ya viongozi waliohifadhiwa hapo na baadaye kuweza kutembelea kambi hiyo ni Mheshimiwa Sam Nujoma, aliyekuwa Rais wa Namibia ambaye alifika tarehe 3 Julai, 2000 na Mheshimiwa Hifikepunye Pohamba aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa SWAPO ambaye alitembelea hapo tarehe 5 Julai, 2003. Mheshimiwa Hifikepunye Pohamba kwa sasa ndiye Rais wa nchi ya Namibia. MHE. HAFIDH ALI TAHIR: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake kutokana na suala hili lakini alichokuwa akizungumza Mheshimiwa Waziri ni kwamba majengo hayo hivi sasa yanatumika kama shule. Lakini pamoja na hayo, mbali ya kuwepo shule, je, Serikali haioni kwamba bado kuna umuhimu wa kuendelea kuzihifadhi sehemu hizo za Kongwa na kuzifanya kuwa kivutio kimojawapo cha watalii na kumbukumbu za kihistoria hasa njia za chini kwa chini zilizokuwa zinatumiwa na Mheshimiwa Machel na sehemu nyingine kuliko kuziweka kama zilivyo hivi sasa? Lakini la pili kwa kuwa sioni faida, je, wananchi wa Kongwa wamefaidika vipi kwa kuwekewa majengo yale kuwa shule? Je, hao waliokowako hapo wamewasaidia vipi wananchi wa Kongwa katika kuendeleza shughuli zao za kijamii katika sehemu ile? NAIBU WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU MAAFA NA KAMPENI DHIDI YA UKIMWI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishasema katika jibu la msingi kwamba maumbile kwa maana ya majengo, hasa hasa yale ya makaburi na mahandaki yamebaki kama yalivyo kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo vya nchi hizo kupita na kuangalia historia yao ya nyuma. Siamini kama Mheshimiwa Hafidh Ali lile analosema kwamba kuwepo kwa shule pale sio jambo la faida, naamini hasemi kwa dhamira; naamini kuwepo kwa shule ni suala la msingi na tusingeweza kutumia yale majengo kwa kitu kingine chochote. (Makofi) Na. 117 Kuigawa Tarafa ya Mpwapwa MHE. GEORGE MALIMA LUBELEJE aliuliza:- 3 Kwa kuwa Tarafa ya Mpwapwa iliyopo wilayani Mpwapwa ni kubwa sana ina kata tisa (9) na jumla ya watu 140,000:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuigawa Tarafa hiyo ili kupata Tarafa tatu za Mpwapwa yenyewe (Kata za Mpwapwa mjini, Vinghawe na Chunyu); Tarafa ya Mima (iwe na Kata za Mima, Berege na Mkanana) na Tarafa ya Matomondo (itakayokuwa na Kata za Matomondo, Kimagai na Godogode)? (b) Je, Serikali itakubaliana nami kwamba kuigawa Tarafa ya Mpwapwa kufanya Tarafa tatu (3) za kiutawala kutasaidia sana kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi wa maeneo hayo kuliko ilivyo sasa? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Kwa niaba ya Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala hapa nchini huzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa. Aidha, vipo vigezo vya kuzingatia, mahsusi kwa uanzishwaji wa Tarafa kama vile: · Idadi ya watu wasiopungua 50,000; · Idadi ya kata zisizopungua 10; · Ukubwa wa eneo lisilopungua kilomita za mraba 500; na · Uwezo wa uongozi na watumishi kuhudumia eneo jipya la kiutawala. Mheshimiwa Spika, Tarafa ya Mpwapwa ina ukubwa wa kilomita za mraba 2,744.7, na jumla ya watu 143,962 katika kata tisa (9) za tarafa hiyo. Tarafa anazopendekeza Mheshimiwa Mbunge za Mpwapwa Mjini zitakuwa na kilomita za mraba 966.2 na jumla ya watu 52,913; Mima itakayokuwa na kilomita za mraba 903.4 na jumla ya watu 52,645, na Matomondo itakayokuwa na kilomita za mraba 874.7 na jumla ya watu 38,404; zitakuwa na kata tatu tu kila tarafa moja. Kwa kuwa tarafa ya sasa ya Mpwapwa yenye kilomita za mraba 2,744.7 na kata 9 ina idadi kubwa ya watu, yaani watu 143,962 ambao ni karibu mara tatu zaidi ya idadi ya chini kivigezo, ni dhahiri kuwa ingestahili kugawanywa. Hata hivyo, ili kuepuka kuigawa zaidi tarafa ya Mpwapwa na hatimaye kuikosesha vigezo vya kupatikana tarafa mpya, kupitia Bunge lako Tukufu, namshauri Mheshimiwa Mbunge kuzingatia wazo la kuigawa katika Tarafa mbili za Mpwapwa mjini na Mima na kuondoa pendekezo la kuanzisha Tarafa ya Matomondo ambayo itakuwa na idadi ya watu 38,404 ambayo ni chini ya kigezo. (b) Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) hapo juu, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuigawa Tarafa ya Mpwapwa kutusaidia sana kuongeza huduma karibu na wananchi. Lakini ili kuendana na vigezo vilivyopangwa ni 4 vizuri kuigawa Tarafa hiyo katika Tarafa mbili badala ya tatu kwa kuanzia. Ni matarajio ya Serikali kwamba Mheshimiwa Mbunge kwa kupitia vikao vya wilaya na mkoa watajadili rasmi mapendekezo ya kuigawa Tarafa na hatimaye kuyawasilisha katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa tathimini zaidi. MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, kwa jibu lake zuri. Je, katika bajeti ya mwaka 2007/2008 ukiacha tarafa ya Matomondo, Serikali itakuwa tayari kuzigawa tarafa mbili za Mpwapwa na Mima? Pili, kwa kuwa Serikali za Mitaa ni Serikali kamili; na kwa kuwa Halmashauri za Wilaya zina madaraka na mamlaka kamili; je, kwa nini zisiachiwe Halmashauri za Wilaya, Miji na Manispaa kugawa vijiji, kata na kadhalika na kuipa taarifa TAMISEMI hasa ikizingatiwa kuwa mchakato wa kugawa vitu hivyo huchukua muda mrefu? Je, Serikali itakuwa tayari kukubali kwamba sasa Serikali za Mitaa ziachiwe kugawa vijiji na kata? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kwa heshima nimjibu Mheshimiwa Lubeleje, maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:- Labda nianze na hili la pili. Kwa sasa ni jambo lisilowezekana kugawa tarafa, kata, na vijiji kwa sababu suala hilo lipo chini ya mamlaka ya kisheria ambayo yamebainisha wazi nani anapaswa kufanya kazi hiyo. Kwa hiyo ugawaji unaweza kufanyika tu hadi hapo sheria zitakapobadilishwa, kwa sasa hilo haliwezekani. Mheshimiwa Spika, Kuhusu suala lake la kwanza, kuhusu zile tarafa mbili, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, kazi ya kwanza ni lazima jambo hili litoke kwenye Halmashauri inayohusika ili kuweza kushirikisha jamii kwa mawazo aliyonayo Mheshimiwa Lubeleje.