MKUTANO WA TATU Kikao Cha Hamsini Na Nane
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA __________ MAJADILIANO YA BUNGE __________ MKUTANO WA TATU Kikao cha Hamsini na Nane – Tarehe 24 Juni, 2021 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Dkt. Tulia Ackson) Alisoma Dua NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Katibu. NDG. MOSSY LUKUVI – KATIBU MEZANI: HATI ZA KUWASILISHA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Mwaka 2019/2020. NAIBU SPIKA: Ahsante sana, Katibu. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) NDG. MOSSY LUKUVI – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU NAIBU SPIKA: Maswali, tutaanza na Ofisi ya Rais TAMISEMI. Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda sasa aulize swali lake. Na. 485 Utoaji wa Namba Vijiji vya Jimbo la Ndanda MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itasaidia na kufanikisha kutoa Namba kwa Vijiji vya Chipunda, Mkalinda na Sululu ya Leo vyenye wakazi zaidi ya elfu kumi katika Jimbo la Ndanda? NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Mheshimiwa David Silinde, majibu. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vya Chipunda na Sululu ni vijiji halali ambavyo vimeendelea pia kutambulika kupitia Matangazo ya Serikali Namba 536 Mamlaka za Miji na 537 Mamlaka za Wilaya ya tarehe 19/07/2019.
[Show full text]