Majadiliano Ya Bunge ______
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA KUMI NA SITA Kikao cha Tano - Tarehe 15 Juni, 2004 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Pius Msekwa) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU Na. 40 Uwekezaji kwa Utaratibu wa BOT MHE. DR. LAWRENCE M. GAMA aliuliza:- Kwa kuwa kwa muda mrefu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikizungumzia utaratibu wa uwekezaji hususan katika sekta ya miundombinu kwa utaratibu wa Build, Operate and Transfer ili kurahisisha maendeleo. Je, Serikali inaweza kuwavutia wawekezaji wowote chini ya utaratibu huo? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UBINAFSISHAJI alijibu:- Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dr. Lawrence Gama, Mbunge wa Songea Mjini, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, katika kikao cha Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kilichomaliza shughuli zake tarehe 23 Aprili, 2004, nilimjibu Mheshimiwa Philip Magani, Mbunge wa Ruangwa, ambaye alipenda kufahamu jinsi ya kuwavutia wawekezaji kwa njia ya Build, Operate and Transfer (BOT). Mheshimiwa Spika, katika kurejea jibu langu la msingi ni kuwa, utaratibu wa Build, Operate and Tranfer ni mbinu ambayo Serikali imeamua kuitumia kwa kutoa vivutio maalum ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje, kuwekeza katika miundombinu ili kuipa Serikali unafuu katika gharama za uwekezaji. Chini ya utaratibu huu wawekezaji binafsi huruhusiwa kujenga, kuendesha na hatimaye kukabidhi kwa 1 Serikali, miundombinu waliyojenga baada ya muda wa makubaliano kumalizika kwa kuingia mikataba na Serikali. Mheshimiwa Spika, mkataba wa namna hii humruhusu mwekezaji binafsi kutoza ushuru kwa watumiaji wote wa miundombinu aliyojenga kwa kuzingatia makubaliano ambayo yako kwenye mkataba na Serikali.
[Show full text]