Tarehe 16 Aprili, 2018
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA KUMI NA MOJA Kikao cha Kumi – Tarehe 16 Aprili, 2018 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Dkt. Tulia Ackson) Alisoma Dua NAIBU SPIKA: Wabunge tukae, Katibu. NDG. RAMADHANI ISSA ABDALLAH – KATIBU MEZANI: HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa mwaka wa fedha 2018/2019. NAIBU SPIKA: Ahsante, Katibu. NDG. RAMADHANI ISSA ABDALLAH – KATIBU MEZANI: 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) MASWALI NA MAJIBU Na. 77 Kituo cha Afya na Zahanati Zilizojengwa na Mbunge MHE. HUSSEIN N. AMAR aliuliza:- Kwa juhudi zake Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale ameanzisha ujenzi wa baadhi ya majengo ya zahanati kubwa na za kisasa katika Vijiji vya Nyamikonze na Inyenze. (a) Je, Serikali ipo tayari kusaidia kukamilisha ujenzi huo? (b) Je, Serikali ipo tayari kuifungua zahanati iliyojengwa na Mbunge katika Kijiji cha Mwamakilinga ambayo imekamilika tangu Novemba, 2014? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri ya Nyang’hwale kupitia mapato ya ndani ilitenga shilingi milioni 45 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati ya Kijiji cha Nyamikonze, lakini ukamilishaji haukufanyika kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Nyang’hwale kuwa kidogo. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Nyang’hwale kupitia mapato ya ndani imetenga shilingi milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Nyamikonze. Mpaka sasa zahanati haijaanza kufanya kazi na wananchi wa kijiji hicho wanapata huduma za afya katika zahanati ya Mwingiro iliyo karibu na kijiji hicho. 2 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) (b) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Nyang’hwale katika mwaka wa fedha 2017/2018 imetenga shilingi milioni 90 kutokana na mapato ya ndani kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati katika Kijiji cha Inyenze iliyofikia hatua ya kuezekwa. Fedha hizo bado hazijapatikana kutokana na makusanyo kuwa kidogo. Mara fedha hizo zitakapopatikana utekelezaji utafanyika kama mpango unavyoelekeza. Zahanati ya Mwamakilinga iliyojengwa na Mbunge wa Jimbo hilo, ilifunguliwa na Mheshimiwa Engineer Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Geita tarehe 29 Januari, 2018 na mpaka sasa inafanya kazi. (c) Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale alianzisha ujenzi wa majengo matatu katika Kituo cha Afya Kharumwa ambayo yote yalikuwa hatua ya lenta. Majengo hayo ni wodi ya watoto, wadi ya wazazi ambayo ndani ina chumba cha upasuaji wa dharura kwa wajawazito na jengo la kuhifadhia maiti (mortuary). Shirika la AMREF linaendelea na ukamilishaji wa jengo la wodi ya wazazi ambayo ndani ina chumba cha upasuaji wa dharura kwa wajawazito. Ujenzi huo unategemea kukamilika ifikapo tarehe 15, Mei, 2018 kwa gharama ya shilingi milioni 164. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua jitihada kubwa zilizofanywa na Mbunge wa Nyang’hwale, mwishoni mwa mwezi Desemba, 2017 Serikali ilitoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya Kituo cha Afya Kharumwa. Halmashauri imetenga shilingi milioni 70 kwa ajili ya ukamilishaji wa wodi ya watoto na shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Kharumwa. Ujenzi huo unaaendelea na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Mei, 2018. Kiasi cha shilingi milioni 280 kilichobaki kitatumika katika ujenzi wa chumba cha upasuaji (theatre), maabara ya kisasa, nyumba ya mtumishi na wodi ya upasuaji (surgical ward) kwa wanawake na wanaume. NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, swali la nyongeza. 3 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza, lakini naomba nitumie nafasi hii kuwapa pole wananchi wangu wa Jimbo la Nyang’hwale kwa mauaji ya kikatili ambayo yamefanyika wiki iliyopita, akina mama wanne wamenyongwa kwa kutumia kanga zao na wawili wakiwa wajawazito na mauaji hayo yanaendelea kwa Wilaya za jirani. Mheshimiwa Naibu Spika, swali dogo la nyongeza ni kama ifuatavyo; je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha kuisaidia Halmashauri ya Nyang’hwale ili kukamilisha ujenzi wa zahanati iliyopo Iyenze na Mwamakiliga? Serikali ina mpango gani kuisaidia Halmashauri? Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naishukuru AMREF kwa kukamilisha majengo matatu yaliyopo pale Kituo cha Afya Kharumwa. Serikali ina mpango gani baada ya kukamilishwa majengo hayo kuendeleza kwa kutusaidia kuongeza vifaatiba pamoja na wauguzi? (Makofi) NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, majibu. NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kwa dhati kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada zake za kuhakikisha wananchi wanapata huduma iliyo bora ya afya. Yeye hakika ni mfano bora wa kuigwa kwa Waheshimiwa Wabunge wengine. (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza, anauliza Serikali kusaidia Halmashauri kumalizia zahanati, ni nia ya dhati kabisa ya Serikali kuhakikisha kwamba tunasaidia, lakini kinachogomba ni uwezo. Kwa hiyo, kadri bajeti itakavyokuwa imeboreka, hakika hatuwezi tukawaacha wananchi ambao Mheshimiwa Mbunge ameonesha jitihada tukaacha kumalizia. 4 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili baada ya kazi nzuri iliyofanywa na AMREF, suala la zima la kupeleka vifaa pamoja na wataalam, ili kazi iliyotarajiwa iweze kuwa nzuri, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba vituo vya afya na zahanati zetu zote zinafanya kazi. Muda siyo mrefu, wakati tunahitimisha, Mheshimiwa Waziri wa Utawala atakuja kusema neno kuhusiana na suala zima la kuajiri watumishi wa Serikali. (Makofi) NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mahmoud Mgimwa, swali la nyongeza. MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Mtikila kilijenga zahanati ambayo ilikamilika mwaka 2015, lakini mpaka leo haijafunguliwa kwa sababu ya tatizo la vifaa na wataalam. Namuomba Naibu Waziri aniambie, ni lini watafungua zahanati hii ili kutokudhoofisha nguvu za wananchi? NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, TAMISEMI, majibu. NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tulipokea katika michango ya Mheshimiwa Bobali na nikayarudia katika moja ya maswali ambayo nilikuwa najibu hapa, kwamba ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba zahanati ambazo zimekamilika huduma itatolewa. Mheshimiwa Naibu Spika, nimetangulia kusema muda siyo mrefu kwamba ni siku ya leo ambapo Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Utawala atakuja kuhitimisha na atasema neno kuhusiana na suala zima la kupatikana wahudumu wa afya na waganga, maana na sisi tunategemea kupata kibali cha ajira kutoka kwake. 5 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Cecil Mwambe, swali la nyongeza. MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira yaliyopo Jimbo la Nyang’hwale yanafanana kabisa na mazingira yaliyopo kwenye Jimbo la Ndanda na hasa kwenye Kata ya Chiwata ambapo kuna Shule ya Sekondari ya Chidya. Wananchi wa Chidya waliamua wenyewe kutumia nguvu zao kujenga jengo pale kwa ajili ya kuweza kupata zahanati. Kwa bahati mbaya kabisa, maelekezo niliyokuwa nawaambia, watakapokuwa wamefanikiwa kukamilisha boma, wawe wameendelea juu wameweka mpaka bati, Serikali itakuja kumalizia kuwaletea vifaa pamoja na kufungua. Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri ya kututaka tusubiri, lakini napenda watu wale wasikie, Chidya ni sehemu ya mkakati wa hiyo mikakati yenu ya Wizara kukamilisha maboma hayo na lini hiyo kazi itafanyika? (Makofi) NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI majibu. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali na pia ni azma ya CCM; ukisoma katika Ilani ya CCM ukurasa wa 81 Ibara ya 50 tumetaja kabisa kwamba kila sehemu ambayo ipo kijiji tutahakikisha kwamba inajengwa zahanati, kila Kata itakuwepo na Kituo cha Afya na kila Wilaya itakuwa na Hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, ni azma thabiti na ndiyo maana imeandikwa. Naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge avute subira. Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba wananchi wake kama ilivyo Nyang’hwale wamejitolea, lakini sina uhakika kama naye 6 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mbunge amefanya kazi nzuri kama Mbunge wa Nyang’hwale. Na yeye tumtake ashirikiane na Serikali, kwani wanaotibiwa ni wananchi wetu. Kwa hiyo, ni vizuri wote tukashiriki katika suala zima la kuhakikisha kwamba afya inakuwa bora. (Makofi) NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mussa Ntimizi, swali la fupi. MHE. MUSSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nipongeze kazi nzuri ya kuboresha mazingira ya kutolea afya katika maeneo yetu kwa nchi nzima. Kutokana na shida kubwa ya afya iliyopo katika maeneo yetu tuliyokuwa nayo, Serikali ije na mpango