Majadiliano Ya Bunge Mkutano Wa Kumi Na Nne
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _________________ MAJADILIANO YA BUNGE _______________ MKUTANO WA KUMI NA NNE Kikao cha Tisa – Tarehe 6 Februari, 2009 (Mkutano Ulianza Saa 3.00 Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU Na. 107 Mikakati ya Kupambana na Uharibifu wa Mazingira MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:- Kwa kuwa, mwaka 2006 Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ilitangaza mambo muhimu ya kuzingatia katika mikakati ya kupambana na uharibifu wa mazingira hapa nchini:- (a) Je, ni miti kiasi gani imepandwa kwa kila mkoa na kwa maeneo yapi? (b)Je, matumizi ya mkaa yamepunguzwa kwa kiasi gani hapa nchini kuanzia mwaka 2006 – 2008? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MAZINGIRA alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Sakaya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikipokea taarifa za upandaji miti kutoka mikoa yote Tanzania Bara, kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa. Taarifa zilizowasilishwa toka kila mkoa, zinatoa mchanganuo wa miti iliyopandwa katika kila wilaya. Katika kipindi cha mwaka 2006/2007, jumla ya miti 95,411,580 ilipandwa na kutunzwa ambayo ni sawa na 73.6% ya lengo la miti 1 129,597,818. Idadi hii ni ya miti ilipandwa katika mikoa yote 21 na katika Wilaya zake zote. Mchanganuo huu ni mrefu, hivyo nitampatia Mheshimiwa Mbunge, kama kiambatanisho. Labda tu kwa faida ya wananchi, Mkoa unaoongoza kwa upandaji miti ni Iringa ikiwa na jumla ya miti 17,486,732; ikifuatiwa na Mkoa wa Tanga ikiwa na jumla ya miti 6,873,579 na Mara ikiwa na jumla ya miti 5,443,842.
[Show full text]