4 MEI, 2013 MREMA 1.Pmd
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
4 MEI, 2013 BUNGE LA TANZANIA _____________ MAJADILIANO YA BUNGE _______________ MKUTANO WA KUMI NA MOJA Kikao cha Kumi na Nane - Tarehe 4 Mei, 2013 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge tukae. Waheshimiwa Wabunge Mkutano wa 11 unaendelea, kikao hiki ni cha 18. HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:- Randama za Makadirio ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014. 1 4 MEI, 2013 MHE. OMAR R. NUNDU (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA): Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013 na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014. MHE. CHRISTOWAJA G. MTINDA (K.n.y. MHE. MCH. ISRAEL Y. NATSE - MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI WA WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:- Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014. HOJA ZA SERIKALI Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2013/2014 Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2013/2014. Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwasilisha hotuba yangu ya Bajeti kwa mwaka 2013/2014 mbele ya Bunge lako Tukufu. 2 4 MEI, 2013 Pili, nawashukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu na Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais kwa kuendelea kuniamini kuiongoza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Namshukuru pia Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mizengo Pinda kwa maelekezo anayonipatia katika kutekeleza majukumu ya Wizara yangu. Nawathibitishia Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi kwa ujumla kwamba nitaendelea kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa ufanisi, uadilifu na uaminifu mkubwa. Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Anna Margareth Abdallah (Mb.) na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Mohammed Seif Khatib (Mb.) kwa kuchaguliwa kuiongoza Kamati hiyo. Hali kadhalika, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote walioteuliwa kuwa Wajumbe wa Kamati hiyo. Ninawaomba Wajumbe hao wapokee shukurani zangu kwa maoni waliyotupatia wakati wa kuchambua mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka 2013/2014. Maoni na mapendekezo yao yametusaidia sana katika kuiandaa hotuba hii. Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo tarehe 28 Machi, 2013 Mbunge mwenzetu Salim Hemed Khamis, Mbunge wa Jimbo la Chambani alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Ninaungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole kwako Mheshimiwa Naibu Spika, familia, ndugu na marafiki kwa msiba huo. Namuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Peponi, Amina. Mheshimiwa Naibu Spika, Dira na dhima ya Wizara ya Ulinzi na JKT. Dira ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni kuwa Taasisi iliyotukuka ya kudumisha amani na usalama nchini. Kwa kuzingatia kwamba ulinzi wa Taifa ndilo jukumu la kwanza kwa Serikali, dhima ya Wizara hii ni kuilinda mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya 3 4 MEI, 2013 maadui kutoka nje au ndani ya nchi na kuhakikisha kuwa uhuru na maslahi ya Taifa letu (national interests) yanakuwa salama wakati wote. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Wizara yangu inaendelea kutekeleza jukumu hili kwa ufanisi. Kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya mwaka 1966 Sura 192 na Sheria ya JKT ya mwaka 1963 Sura 193, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imekabidhiwa jukumu la kusimamia Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa katika kutekeleza majukumu yake. Vile vile Wizara yangu ina wajibu wa kuvipatia vyombo hivi mahitaji yake ya kimsingi ili kuviwezesha kutekeleza majukumu hayo. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya mwaka 1966, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ina majukumu saba. Kwanza, Wizara ina jukumu la kulinda mipaka ya nchi yetu. Pili, Wizara ya Ulinzi inasaidiana na Mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga ili kuwapatia wananchi waliofikwa na majanga misaada ya kibinadamu. Tatu, Wizara inashiriki katika shughuli za Ulinzi wa Amani katika nchi zenye migogoro duniani. Nne, Wizara hii inaandaa umma wa Watanzania kushiriki katika shughuli za Ulinzi wa Taifa. Tano, Wizara inawajengea vijana wa Kitanzania moyo wa uzalendo na mshikamano wa kitaifa ili kuwaandaa kikamilifu katika kutekeleza shughuli za kujitegemea. Sita, Wizara ya Ulinzi inafanya utafiti ili kuendeleza teknolojia kuhusu matumizi ya kijeshi na kiraia. Saba, Wizara hii inaimarisha ushirikiano na nchi nyingine duniani katika masuala ya Kijeshi. 4 4 MEI, 2013 Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza majukumu niliyoyataja hapo awali, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imejiwekea malengo makuu manane kwa mwaka 2013/2014. Kwanza, kuandikisha Wanajeshi wapya kwa ajili ya Ulinzi wa Taifa. Pili, kuwaendeleza kielimu maafisa na askari wa JWTZ na JKT. Tatu, kununua na kulipatia Jeshi zana bora kwa ajili ya Ulinzi wa Taifa. Nne, kutunza na kuhifadhi vizuri zana za kijeshi na kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi na makazi kwa Wanajeshi. Tano, kuimarisha mahusiano mema na nchi nyingine duniani katika masuala ya kijeshi. Sita, kutoa mafunzo ya ulinzi wa mgambo kwa Watanzania ili kuimarisha Jeshi la Akiba. Saba, kuwapatia vijana wa Kitanzania mafunzo ya kuwajengea nidhamu, ukakamavu na moyo wa uzalendo. Nane, kuyajengea mashirika ya Mzinga, Nyumbu na SUMAJKT mazingira bora ya kukuza teknolojia ili yaweze kujitegemea na kupunguza utegemezi kwa ruzuku ya Serikali. Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka 2012/2013, tulipokea maoni, ushauri na maelekezo kutoka kwa iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa maoni, ushauri na maelekezo yaliyotolewa yamefanyiwa kazi na majibu yake yameainishwa. Hali kadhalika, hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa mjadala huo pia zimezingatiwa katika mpango na bajeti ya mwaka 2013/2014 ninayowasilisha leo hapa Bungeni. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa jukumu kubwa la Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni kulinda uhuru na usalama wa nchi yetu naomba nieleze hali ya usalama wa mipaka yetu na nchi nyingine ilivyokuwa katika mwaka 2012/2013. Hali ya usalama wa mipaka yetu na nchi jirani, nchi kavu na baharini ni shwari kwa ujumla. Hata hivyo katika baadhi ya mipaka yetu na nchi za Uganda, Kenya na Zambia kuna tatizo la muda mrefu la kung’olewa kwa alama za mipakani yaani “beacons”. Wizara yangu kwa kushirikiana 5 4 MEI, 2013 na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa zinaendelea kulifanyia kazi suala hili ili kuzirudisha alama hizo kwenye eneo la mpaka. Mheshimiwa Naibu Spika, Mpaka katika Bahari ya Hindi. Hali ya Usalama katika eneo la mpaka wa Bahari ya Hindi lenye urefu wa kilomita 1,424 ambako nchi yetu inapakana na Kenya, Visiwa vya Ushelisheli, Komoro na Msumbiji inaendelea kuwa shwari. Hivi sasa matukio ya uharamia yaliyokuwa yakitokea miaka mitatu iliyopita yamepungua kwa kiasi kikubwa. Katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2012 hadi sasa hakujatokea tukio lolote la uharamia katika eneo hili. Mafanikio haya yanatokana na doria zinazofanywa na Jeshi la Wananchi kupitia Kamandi yake ya Wanamaji pamoja na ulinzi unaofanywa na majeshi ya Ulaya, Asia na Marekani katika eneo la Ghuba ya Aden. Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya Usalama katika mpaka huu wenye urefu wa kilometa 1,190 ambako Tanzania inapakana na Kenya na Uganda inaendelea kuwa shwari. Hata hivyo kumejitokeza tatizo la wahamiaji haramu kutoka Ethiopia na Somalia wanaoingia nchini kwa kupitia kwenye mpaka wetu na nchi jirani. Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi zimekuwa zikiwasaka wahamiaji haramu pamoja na kuwatafuta Mawakala wa biashara hiyo ili kuwachukulia hatua za kisheria. Mheshimiwa Naibu Spika, Mpaka wa Kaskazini. Hali ya Usalama katika mpaka huu wenye urefu wa kilomita 1,220 ambako Tanzania inapakana na Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni shwari. Jeshi la Wananchi wa Tanzania linaendelea kudumisha ulinzi katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika. Ili kuimarisha ulinzi wa eneo hilo Jeshi la Wananchi wa Tanzania linatarajia kupata boti 2 za kisasa mwishoni mwa mwaka huu ambazo zitatumika kufanyia doria katika Ziwa Tanganyika. 6 4 MEI, 2013 Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpaka wa Kusini Tanzania inapakana na Msumbiji, Malawi na Zambia. Hali ya usalama katika mpaka wetu wa kusini wenye urefu wa kilomita 759 zikiwemo kilomita 36 za maji kwenye Ziwa Nyasa ni shwari. Kuhusu mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa kati ya Malawi na Tanzania mazungumzo bado yanaendelea. Mazungumzo haya yanaratibiwa na Wizara yetu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto mbalimbali nilizozieleza hapo awali, napenda kuwahakikishia wananchi wote wa Tanzania kwa ujumla kwamba ulinzi wa mipaka yetu ni imara. Jeshi letu liko makini na linaendelea kuchukua tahadhari kwa kuimarisha vikosi vyake ili kudumisha ulinzi na usalama wa nchi yetu.