MKUTANO WA NANE Kikao Cha Ishirini Na Mbili
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE YA TANZANIA __________ MKUTANO WA NANE ______________ Kikao cha Ishirini na Mbili – Tarehe 12 Julai, 2007 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Samuel J. Sitta) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU Na. 194 Madiwani Viti Maalum MHE. ESTHER K. NYAWAZWA aliuliza:- Kwa kuwa, Udiwani wa Viti Maalum ni njia ya kupitia katika Uchaguzi ili kuongeza idadi ya Madiwani wanawake katika Halmashauri au Wilaya na kwa kuwa, mikopo mingi itolewayo na Halmashauri za Wilaya huelekezwa zaidi kwa vikundi vya wanawake; na kwa kuwa katika Halmashauri/Wilaya ya Sengerema Madiwani wa Viti Maalum hutolewa katika Kamati ya Mikopo na kuna nafasi za kugombea miongoni mwa Madiwani wenzao hukatazwa mfano Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri/Wilaya au Naibu Meya wa Jiji, Mwenyekiti Kamati ya Maadili na kadhalika. (a) Je, ni kigezo gani hutumika katika kuwatoa Madiwani Viti Maalum katika Kamati ya kutoa mikopo? (b) Je, ni Sheria ipi inayomtoa Diwani wa Viti Maalum, asigombee nafasi zilizotajwa hapo juu na kwa nini na kama sheria hiyo ipo Serikali haioni kuwa haiwatendei haki Madiwani hao na kwamba inavunja Katiba? (c) Kama sheria hiyo ipo, Serikali haioni kuwa imepitwa na wakati na hivyo iletwe Bungeni irekebishwe? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA LA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nyawazwa, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:- 1 (a) Mheshimiwa Spika, uratibu uliotumika kuunda Kamati ya mikopo ya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ni kwa kufuata mwongozo wa uendeshaji Mfuko uliotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, katika Halmashauri zote nchini. Ujumbe wa Kamati ya kutoa mikopo haugombewi bali umewekwa bayana kulingana na mwongozo uliotolewa na Serikali. Kamati ya mikopo katika Halmashauri inaundwa kwa mujibu wa mwongozo nilioutaja hapo juu kwa mujibu wa mwongozo huo kamati ya mikopo ngazi ya Halmashauri inaundwa na wajumbe wafuatao:- (i) Mkurugenzi wa Halmashauri – Mwenyekiti; (ii) Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri – Katibu; (iii) Afisa Maendeleo ya Jamii (jinsia); (iv) Afisa Mipango wa Halmashauri naye ni mjumbe; (v) Wabunge wote waliomo ndani ya Halmashauri husika ni wajumbe; (vi) Wawakilishi wawili wanawake wa vikundi vya uzalishaji mali nao ni wajumbe pamoja; na (vii) Kamati inaweza kumwalika mtaalam yeyote kwa kadri ivyoona. (b) Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 36 (2) cha sheria Na. 7 ya mwaka 1982 ya Serikali za Mitaa (Mamlaka ya Wilaya) na kifungu cha 20 (3) cha sheria Na. 8 ya mwaka 1982 ya Serikali ya Mitaa (Mamlaka ya Miji), Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Meya na Naibu Meya wa Halmashauri husika ni lazima awe Diwani wa kuchaguliwa na wananchi. Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Halmashauri, anachaguliwa kutoka miongoni mwa Madiwani wanaounda Kamati hiyo. Kwa kuzingatia sheria nilizozitaja hapo juu, ni dhahiri kwamba Serikali haivunji Katiba bali inadumisha dhana ya utawala bora. (c) Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwahusisha Madiwani wa Viti Maalum katika Kamati mbalimbali zikiwemo Kamati za Mikopo. Baada ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, kwa kulitambua hilo, Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kupitia kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika tarehe 5/4/2006 kiliwachagua Madiwani wawili wa Viti Maalum kuingia katika Kamati ya Mikopo. Hata hivyo, kulingana na mwongozo wa uendeshaji wa mfuko ulitolewa na Wizara kuna wawakilisha wawili wanawake wa vikundi vya uzalishaji mali. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa haina mpango wowote wa kurekebisha sheria nilizozitaja kwa sababu ni mwaka jana tu baadhi ya vipengele vimerekebishwa kupitia Bunge lako Tukufu. The Local Government Law Miscellaneous Amendment Act Na. 13 ya mwaka 2006. 2 MHE. ESTHER K. NYAWAZWA: Mheshimiwa Spika, nafurahi sana kupata maelezo mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa swali langu la msingi. Lakini ukizingatia kwamba tunapozungumza wakiwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya, Madiwani, wanakuwa ni Madiwani wote. Je, sasa inafikiaje tunapoanza kugawana madaraka tunaanza kubagua Viti Maalum, naomba hapo miongozo haiwezi kurekebishwa? (Makofi) NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA LA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni mwaka jana tu mwezi Desemba, sheria hii ya Serikali za Mitaa ililetwa hapa Bungeni na vipengele mbalimbali vimerekebishwa. Kama Mheshimiwa Mbunge angeona kuna ulazima mimi nafikiri kwa kipindi hicho angetoa hilo angalizo na sisi tungeliangalia. Lakini kwa sasa kurudiarudia, mwaka jana tumefanya amendment na mwaka huu tuanze tena kufanya amendment mimi nafikiri kwa Bunge lako Tukufu itakuwa ni usumbufu. Naomba tuvute subira na wakati ukifika tunaweza tukaliangalia jambo hili kwa undani zaidi. (Makofi) MHE. ZAYNAB M. VULU: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tuko katika hatua maalum ya kutaka kuingia kwenye fifty fifty na kwa kuwa sheria zinatungwa na sisi Wabunge tukiwa humu ndani. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuirekebisha hiyo sheria hata kama tutakuwa tunarudiarudia lakini kurudia huko ni kwa ajili ya kujenga? (Makofi) NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA LA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA : Mheshimiwa Spika, kwa sasa hilo suala liko kwenye mchakato. Mimi nafikiri tungengojea huo mchakato ukiisha uingie Bungeni ndiyo tutarekebisha hili suala. Lakini naomba Waheshimiwa Wabunge, katika mchakato huu washiriki kikamilifu ili sheria hii ipite haraka. Hata mimi mwenyewe nitafurahi iwapo asilimia hamsini kwa hamsini itapita. (Makofi) Na. 195 Ruzuku ya Maendeleo MHE. SIRAJU JUMA KABOYONGA aliuliza:- Kwa kuwa katika miaka ya fedha ya 2004/2005 na 2005/2006 Manispaa ya Tabora haikupata fedha za ruzuku ya Maendeleo kwa kushindwa kukidhi baadhi ya masharti ya ruzuku hiyo, kama vile kutokuwa na Mkurugenzi wa Mji na kwa sababu hiyo wananchi wakakosa fedha hizo ambazo wanazihitaji sana:- (a) Je, kwa nini Serikali iinyima Manispaa ya Tabora fedha za Maendeleo kwa kushindwa kutimiza sharti ambalo liko nje ya uwezo wa Manispaa na Wananchi wa Tabora? 3 (b) Kwa kufanya hivyo. Je, Serikali haioni kwamba haikuwatendea haki wananchi wa Manispaa hiyo? (c) Je, kwa nini Serikali isiwe na utaratibu wa kuwafidia Manispaa inaposhindwa kutimiza masharti ya vigezo vya ruzuku ya Maendeleo kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake kama kutokuwa na watendaji ambao wanateuliwa na mamlaka nyingine kama vile Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu au Waziri wa Serikali za Mitaa? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA LA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Siraju Juma Kaboyonga, Mbunge wa Tabora Mjini, lenye sehemu (a) (b) na (c) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora haikupata ruzuku ya fedha za maendeleo (Local Government Capital Development Grants) kwa mwaka 2004/2005 na 2005/2006 kwa sababu ya ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 88 uliobainika kutokea. Hiki ndicho kigezo kikubwa kilichosababisha hiyo Halmashauri kukosa fedha hizo. Pia wakati upimaji unafanyika, Mkurugenzi wa Manispaa, mweka Hazina na baadhi ya Watumishi wa Idara ya Fedha, walikuwa wamesimamishwa kazi kutokana na ubadhirifu huo. (b) Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivyo, Serikali ilikuwa inaweka mazingira mazuri ili wananchi wa Tabora wanufaike na matumizi mazuri ya fedha za maendeleo. Kwa mazingira ya ubadhirifu isingekuwa kwa maslahi ya umma kupeleka fedha nyingi mahali hapo kwani uwezekano wa fedha hizo kutowafikia wananchi ungekuwa mkubwa. Kwa sasa Serikali imepeleka watendaji wapya katika Halmashauri hiyo. Katika upimaji wa mwaka 2006/07 Halmashauri hii ilifuzu vigezo vinavyotakiwa ikiwa ni pamoja na kupata hati safi ya Ukaguzi toka kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali katika kipindi cha mwaka 2005/06. (c) Mheshimiwa Spika, hakuna utaratibu wa kufidia Halmashauri yoyote inaposhindwa kutimiza masharti ya vigezo vya ruzuku ya maendeleo kutokana na utendaji mbovu. Kuhusu kutoteua watendaji wapya mapema katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Serikali isingeweza kuteua watendaji wengine hadi kesi zilizokuwa zinawakabili wale watuhumiwa zimalizike mahakamani. Suala hilo ni kwa mujibu wa sheria na Kanuni za utumishi wa umma zilizopo kwa sasa. Hata hivyo, kigezo cha kukosa watumishi muhimu siyo kigezo pekee kilifanya kusababisha Halmashauri kukosa ruzuku ya Maendeleo. Vipo vigezo vingine vinavyoweza kukosesha Halmashauri fedha za ruzuku, vigezo hivyo ni pamoja na:- - Hesabu za mwisho za mwaka wa fedha uliopita zilizoandaliwa kwa mujibu wa sheria za fedha Serikali za Mitaa, ziwe zimewasilishwa kwa ukaguzi wakati uliowekwa. 4 - Halmashauri iwe haikupokea Hati chafu ya ukaguzi kwa hesabu za mwisho zilizokaguliwa. - Pasiwepo na ubadhirifu katika usimamizi wa fedha uliotolewa taarifa ama na wakaguzi wa ndani au wa nje kwa miezi 12 iliyopita na kuthibitishwa. Mheshimiwa Spika, Halmashauri zote zinazokosa fedha za ruzuku ya Maendeleo hupewa fedha za kujengewa uwezo (Capacity Building) ili kuwajengea uwezo baadaye ziweze kupata na kutumia fedha za ruzuku ya Maendeleo ipasavyo. MHE. SIRAJU JUMA KABOYONGA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wakati mfumo mzima wa kutoa ruzuku (Capital Development Grand) ulipoanzishwa ni dhahiri zilikuwepo Manispaa au District Councils ambazo zilikuwa na vitabu vichafu na inachukua muda takriban zaidi ya mwaka mmoja mpaka miwili kurekebisha vitabu. Sasa utaratibu wa kutoa ruzuku hii ni sawa sawa na mbio ambazo zinatakiwa zianzie pamoja lakini mbio zile zinafanya wengine wawe mbele wengine wawe nyuma halafu mnatakiwa mfike mwisho kwa pamoja. Haiwezekani. SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, nenda kwenye