Tarehe 16 Aprili, 2011
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA TATU Kikao cha Tisa – Tarehe 16 Aprili, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua MISWADA YA SHERIA YA SERIKALI Muswada wa Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama wa Mwaka 2011 (The Judiciary Administration Bill, 2011) (Majadiliano Yanaendelea) SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, jana tulianza na Muswada huu na hivi leo tutaendelea na majadiliano hadi saa 4.30 asubuhi, halafu tutawaita wanaotoa ufafanuzi waweze kufanya kazi, baada ya hapo tutaingia kwenye Kamati ya Bunge Zima mpaka saa 6.00 mchana halafu itafuata hoja ya kuahirisha kikao. Kwa hiyo, leo ninaanza kumwita Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Freeman Mbowe, atakayefuata nitaangalia baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani; huwezi kuleta wadogowadogo tena watakuwa wanamsema sivyo. Mheshimiwa Freeman Mbowe. (Kicheko) MHE. FREEMAN A. MBOWE (KIONGOZI WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI): Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kwanza kabisa ya mimi binafsi kutoa mchango katika Muswada huu wa Dispensation of Justice, ambao ni muhimu sana katika nchi yetu. Kwanza, ninaomba niweke bayana kabisa kwamba, sisi kama Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kimsingi, tunaunga mkono hoja hii bila tatizo lolote. Yapo mambo kadhaa ya msingi ambayo tutajielekeza kwayo, kwa lengo zuri tu la kuboresha. Ninaomba Waheshimiwa Wabunge wote waelewe kwamba, wajibu wa Mahakama, unakamilisha mtiririko wote wa utoaji haki katika Taifa letu na investiment kama Taifa kwenye mfumo mzima wa utoaji haki ni priority ya Taifa. Mheshimiwa Spika, lakini leo nitajielekeza zaidi kwenye takwimu ili pengine kuweza kulipa Bunge na kulipa Taifa uelewa wa hali halisi ilivyo ndani ya Mahakama zetu.
[Show full text]