MAJADILIANO YA BUNGE ___MKUTANO WA NNE Kikao Cha
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ______________ MAJADILIANO YA BUNGE _____________ MKUTANO WA NNE Kikao cha Tisa – Tarehe 21 Juni, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. PEREIRA AME SILIMA):- Taarifa za Majumuisho ya Mpango Mkakati wa Kujibu Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu za Wizara, Idara na Serikali na Mikoa kwa Mwaka wa Fedha 2009/2010. Taarifa ya Mwaka na Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa mwaka 2009/2010 (The Annual Report and Audited Accounts of Tanzania Revenue Authority for The Year 2009/2010. MASWALI NA MAJIBU Na. 86 Posho za Madiwani MHE. ZARINA SHAMTE MADABIDA aliuliza:- Diwani ni Kiongozi muhimu sana wa kusimamia utekelezaji wa mipango yote ya Kata, na kumsaidia Mbunge kumudu majukumu yake. Lakini pamoja na majukumu 1 mengine ya kusimamia maendeleo ya wananchi katika maeneo yao, wanapata posho ya shilingi 120,000/= ambayo ni kidogo sana ikilinganishwa na majukumu makubwa waliyonayo:- Je, Serikali haioni sasa umuhimu wa kuongeza viwango vya posho za Madiwani kulingana na kupanda kwa gharama za maisha? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zarina Shamte Madabida, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa Waheshimiwa Madiwani ndio wasimamizi wakubwa wa utekelezaji wa Mipango ya maendeleo ngazi ya Kata. Aidha, ni kweli kuwa majukumu ya Madiwani yameongezeka hasa baada ya kuanzishwa dhana ya upelekaji madaraka kwa wananchi yaani (D by D). Kwa kuzingatia hilo Serikali imekuwa ikiboresha maslahi ya Madiwani ikiwemo posho na stahili mbalimbali kwa lengo la kuwarahisishia utekelezaji wa majukumu yao. Katika mwaka wa fedha 2007/2008, Serikali ilitekeleza ahadi yake ya kuongeza posho za Madiwani kama ifuatavyo:- (i) Posho ya mwezi shilingi 120,000/= ambapo shilingi 60,000/= ni ruzuku ya Serikali Kuu; (ii) Posho ya kikao shilingi 40,000; na (iii) Posho ya madaraka kwa wenyeviti/meya viwango ni kati ya shilingi 100,000 na 350,000/=. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa utekelezaji wa Mpango wa kupeleka Madaraka kwa Wananchi yaani (D by D) umesababisha rasilimali nyingi kupelekwa katika ngazi ya mamlaka za Serikali za Mitaa na hivyo kuhitaji usimamizi wa karibu chini ya Waheshimiwa Madiwani. Aidha, wakati najibu sehemu (a) ya swali la Mheshimiwa Deo Filikunjombe, Mbunge wa Ludewa, kuhusu maslahi ya Madiwani katika Kikao cha Nane (8) cha Bunge hili nilieleza kwamba azma ya Serikali ni kuendelea kuboresha posho za Waheshimiwa Madiwani kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu. Hivyo, naomba Waheshimiwa Madiwani watambue kuwa Serikali hii ni sikivu na itaendelea kutekeleza azma hiyo kama ilivyokusudiwa. MHE. ZARINA SHAMTE MADABIDA: Ahsante sana Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini atakubaliana na mimi kwamba ni miaka sasa mitatu tokea kima hicho kipandishwe. Lakini vile vile 2 tumeshuhudia katika kipindi hiki ndiyo kumekuwa na mfumko mkubwa sana wa kupanda kwa vitu vingi sana. Je, Serikali haioni kwamba sasa hivi imefika kweli kipindi wakati ambapo hizi posho ziongezwe hasa ukitilia maanani kwamba hawapati mshahara? Je, Serikali haiwezi sasa basi kama haiwezi kupandisha posho hizi sasa hivi kuwaruhusu Madiwani wapate asilimia japo ndogo katika makusanyo yao kutoka kwenye Manispaa zao ili posho zipande? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA(TAMISEMI): Mheshimiwa Spika, haya yanayosemwa hapa, tuliyazungumza Dar es Salaam na katika Kamati yetu ile ya Katiba, Sheria na Utawala. Mheshimiwa Waziri wa Nchi, alisema kwamba ni nini ambacho tunakusudia kufanya kwa maana ya kuboresha hizi posho za Madiwani zinazozungumzwa hapa. Wakati huo huo tulipokuja hapa Wabunge mbalimbali wamezungumza hapa ndani kwa uchungu mkubwa sana kuhusu posho hizi za Madiwani na wakati huo huo hata jana nimewasikiliza Waheshimiwa Wabunge wakizungumza hapa. Wamezungumza kwa uzito mkubwa kuhusu posho za Madiwani. Sisi wenyewe kama Wizara tumekwenda katika Mikoa yote tuliyokwenda na Halmashauri zote kila mmoja amekuwa namna ya kuboresha posho za Madiwani. Hakuna mtu yoyote Mheshimiwa Spika ambaye ana ubishi na hilo. Hata wewe mwenyewe huwezi kubisha katika jambo hili linalozungumzwa hapa. Tulipokwenda tukasema sasa tunataka kufanya kazi hii na naomba Waheshimiwa Wabunge watuamini tunaposema kwamba Serikali hii ni sikivu, ni Serikali ambayo inasikiliza kuhusu matatizo ya Madiwani. Nataka watuamini kwamba ni kweli kabisa tunavyosema hivyo, ndivyo anavyoamini Mheshimiwa Rais wetu, ndivyo anavyoamini Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi na sisi wote kama Wizara. Nataka nikuambie leo hapa Mheshimiwa Spika, jambo hili tunalijadili, idadi yetu ya Madiwani imeongezeka. Sitaki nitumie takwimu hapa, kwa sababu nitaonekana kwamba natetea. Lakini niseme tu kwamba wakati tulipoanza kufanya kazi hii yako mambo mengi ambayo katika Sheria zetu yanaonekana kwamba yanakinzana na jambo linalozungumzwa. Kwa mfano, suala la posho, iko Sheria inayozungumza kuhusu hilo. Kwa mfano, suala la kuwapa mishahara, iko Sheria inasema hivyo. Kwa mfano suala la kuwapa exemption Madiwani, iko Sheria. Mheshimiwa Waziri Mkuu, niseme hapa, ametuagiza kama Wizara kwamba tusimame tuangalie namna ambavyo tutamshauri ili hayo yote ambayo yanaonekana kwamba yanazuia posho hizi ziweze kutoka kama zinavyosemwa hapa yaweze kufanyiwa kazi. 3 Mheshimiwa Spika, kanuni ya kusonga ugali ni kuacha maji yachemke. Mimi naomba tu mtuamini kwamba maji yakishachemka kazi hiyo itafanyika na watuamini kwamba tutafanya hivyo. (Makofi) MHE. DEO H. FILIKUNJOMBE: Asante Mheshimiwa Spika kunipa fursa hii niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri anakubali kabisa kwamba Madiwani ni watu muhimu sana kwenye kufuatilia maendeleo majimboni kwetu na kwa kuwa wakati tunapofanya kampeni tunasema mafiga matatu, figa la kwanza linahudumiwa vizuri, figa la pili linahudumiwa vizuri, figa la tatu tunalitekeleza ambao ni Madiwani, sasa Mheshimiwa Waziri anatoa tamko gani au kauli gani kwamba tubadili Sheria zetu za fedha na Sheria za Halmashauri ili kwamba ikishindikana kuwaboreshea maslahi yao basi Madiwani nao waweze kukopa vyombo vya usafiri kama vile wanavyokopa Mawaziri, kama vile wanavyokopa Wabunge? Ahsante sana. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Spika, hii theory ya mafiga matatu ni sahihi kabisa. Hapa sisi tunaamini katika utawala na uongozi wa pamoja. Nataka niseme tu hapa, anazungumza juu ya Sheria mambo ya exemption. Mambo ya exemption yana Sheria yake, watumishi wa Serikali, Wabunge kama inavyoelezwa, wenye mishahara, na vitu vingine. Madiwani wanapata posho, ukisema kwamba unawa-exempt unasema kwamba unawapa mimi, waende na wao wakanunue nao magari, unajiuliza unawakata nini, unawakata posho na nini. Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nikasema kwamba mtupe nafasi sasa tuhuishe haya mambo yatakapokuja hapa tukiyaleta hapa tukija wote sisi hapa tukazungumza mambo haya, hakuna hela ya Serikali inayotumika bila kupata kibali cha Serikali kwa maana ya Bunge hapa na sisi tuombe itakapokuwa imetokea hivyo baada ya kumshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu sisi tutatekeleza yote yale ambayo nyinyi mtakuwa mmeelekeza hapa. Kwa hiyo naomba mtuamini kwamba tutafanya kazi hiyo na mtaona ambacho kitafanyika. Na. 87 Ujenzi wa Barabaraza Zinazounganisha Kanda mbili za Nkasi Kusini MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:- Jimbo la Nkasi Kusini lililogawanyika katika kanda mbili ambazo zinajitegemea katika masuala yote ya kijamii na kiuchumi lina tatizo kubwa la mawasiliano ya barabara zinazounganisha kanda hizo. Wakati wa uchaguzi mkuu 2010 Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya kuboresha barabara hizo za Kitosi-Wempembe, Nkana-Kala na Namanyere- Ninde. 4 (a) Je, ni lini Serikali itaanza mchakato wa kutengeneza barabara hizo tatu kama utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais? (b) Kwa kuwa barabara hizi ni mzigo usiobebeka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi. Je, Serikali iko tayari kuzichukua na kuzihudumia barabara hizo kupitia wakala wake (TANROADS)? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbunge wa Nkasi Kusini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya kuboresha barabara zilizotajwa na Mheshimiwa Mbunge, kwa kuzingatia agizo la Mheshimiwa Rais, Halmashauri katika Bajeti ya mwaka 2010/2011 kupitia fedha za Mfuko wa Barabara ilifanya ukarabati wa barabara kama ifuatavyo:- 1. Barabara ya Kitosi – Wampembe yenye urefu wa kilometa 68 imefanyiwa matengenezo ya sehemu korofi yaani (spot improvement) kwa shilingi milioni 8 urefu wa kilometa 6; 2. Barabara ya Nkana – Kala yenye urefu wa kilometa 67 imefanyiwa matengenezo ya muda maalum yaani (periodic maintenance) urefu wa kilometa 1 kwa shilingi milioni 15; na 3. Barabara ya Namanyere – Ninde yenye urefu wa kilometa 60 imefanyiwa matengenezo ya sehemu korofi yaani (spot improvement) kwa gharama ya shilingi milioni 7 umbali wa kilometa 5 na kujenga makalvati mistari 9 kwa gharama ya shilingi milioni 14.5. Mheshimiwa Spika, kupitia mpango wa usafiri wa Serikali za Mitaa (LGTP), barabara ya Nkana – Nkala itafanyiwa ukarabati wa daraja lenye urefu wa mita 3 kwa