MKUTANO WA KUMI NA MBILI ___Kikao Cha Sita
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _________ MAJADILIANO YA BUNGE __________ MKUTANO WA KUMI NA MBILI __________ Kikao cha Sita - Tarehe 18 Juni, 2003 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Juma J. Akukweti) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU Na. 50 Upungufu wa Watumishi - Hospitali ya Wilaya ya Mbulu MHE. PHILIP S. MARMO aliuliza:- Kwa kuwa siku zilizopita Wizara imekiri upungufu mkubwa wa watumishi katika Hospitali ya Wilaya ya Mbulu katika fani zote kama Madaktari, Wauguzi, Wataalam wa X-ray na Famasia na mfano mmoja ukiwa ni kwamba mashine mpya za chumba cha X- ray hazitumiki kwa sababu ya ukosefu wa wataalam. Je, ni lini Serikali itawaajiri wataalam niliowataja ili kutatua tatizo hilo sugu? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Philip Marmo, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tarehe 18 Julai, 2002 wakati nikijibu swali Na. 873 la Mheshimiwa Mbunge, nilikiri upungufu wa wataalam wa afya katika Hospitali ya Wilaya ya Mbulu. Naomba kumpongeza kwanza Mheshimiwa Philip Marmo, Mbunge wa Mbulu, kwa juhudi zake kubwa sana anazozichukua katika kutatua matatizo yaliyoko katika Hospitali ya Wilaya ya Mbulu ikiwa ni pamoja na upungufu wa watumishi. Halmashauri 1 za Wilaya nyingi hapa nchini bado zina upungufu wa wataalam katika fani mbalimbali. Ofisi ya Rais, pamoja na Idara Kuu ya Utumishi inajitahidi sana kutoa vibali vya ajira, lakini waombaji wa kazi hizo mara nyingi wamekuwa ni wachache. Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Wilaya ya Mbulu ni moja ya Hospitali za Wilaya ambazo zina upungufu wa Madaktari, Wauguzi na wataalam wengine. Hata hivyo hospitali hii ina Madaktari Wasaidizi saba kati yao watatu wamepelekwa masomoni na wanatarajiwa kurudi mwaka kesho 2004. Aidha, hospitali hii inahitaji Wakunga Wasaidizi 35 lakini hadi sasa waliopo ni 18 tu. Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mtaalam wa kutumia X-ray, ni kweli kuwa Hospitali ya Wilaya ya Mbulu inayo X-ray mpya lakini hadi sasa hivi haitumiki kwa kukosa mtaalam. Mwaka 2003, Halmashauri hii ilipatiwa kibali cha kuajiri mtaalam, lakini hakuna aliyeomba. Baada ya utaratibu huu kushindikana, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ilikutana na wahusika katika Wizara ya Afya ili kuwaomba wasaidie katika kumpata mtaalam huyo. Hadi sasa juhudi hizo bado zinaendelea na tunayo matumaini makubwa kuwa mtaalam atapatikana ili huduma inayosubiriwa na wananchi kwa hamu iweze kutolewa. MHE. PHILIP S. MARMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri, amelijibu swali langu vizuri sana lakini nina swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Spika, mimi huwa nikiwa Wilayani angalau mara moja kwa wiki natembelea hospitali hii kupitia kuangalia hali ya wagonjwa, lakini pia kuangalia hali ya hospitali na hali halisi ni kwamba hospitali hii inajaa sana kwa sababu inakuwa kama Hospitali ya Rufaa kwa Vituo vya Afya sita, licha ya hiyo kuna vituo vya nje ya Wilaya, Zahanati zaidi ya 20 na Zahanati tano katika hizo ni za nje ya Wilaya, kwa ajili hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri na Wizara hii kwa ujumla inaonaje namna gani tutatue tatizo hili, kuhamisha baadhi ya watumishi ambapo kuna vituo na zahanati hizi au kutafuta mkakati mpya kabisa ili kutatua tatizo hili la pekee kwa Hospitali ya Wilaya kuwa kama Hospitali ya Wilaya kwa ajili ya uzuri na utendaji kwa wafanyakazi wake? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua ni kweli kabisa kwamba hospitali hii inatumika kama Referral Hospital kwa kiasi fulani na Halmashauri ya Kiteto ambapo vile vile kuna matatizo makubwa siyo ya wataalam tu lakini hata Hospitali yenyewe ya Wilaya. Mheshimiwa Naibu Spika, tunachoweza kusema tu ni kwamba pengine kisiasa haitakuwa jambo jema kujaribu kuwahamisha wataalam tulionao wachache kutoka katika eneo moja kwa kuzingatia hali halisi kwamba kila mahali demand hiyo ipo. Mimi nadhani juhudi tunazozifanya za kujaribu kupata wataalam ili kuweza kukidhi haja ya kila hospitali pengine ndiyo jambo jema ambalo tunaweza tukasema litatusaidia sana. 2 MHE. ISMAIL J. R. IWVATTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu vizuri sana swali na amekiri mwenyewe kwamba pamoja na Serikali kutoa vibali kwa Halmashauri ya Mbulu iweze kuajiri Madaktari imekuwa bado ni vigumu. Je, Serikali haioni kwamba ni kutokana na mishahara midogo ambayo wanapewa Madaktari Wilayani ndiyo sababu inayofanya wasiende huko katika Wilaya kwa sababu Madaktari wengi wanaona bora wafanye kazi katika Miji mikubwa kama Dar es Salaam ama Miji ya Mikoa ili waweze kufungua na Zahanati zao au wakafanye katika ajira za ziada katika hospitali nyingine, katika Wilaya kitu kama hicho hakiwezekani ndiyo maana inakuwa vigumu. Je, Serikali itakuwa tayari kuangalia uwezekano wa kuongeza mishahara ya Madaktari ili waweze kukubali kufanya kazi hata Wilayani? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana ziko sababu nyingi ambazo tunaweza tukazitoa zinazopelekea kuwa na uhaba na ukosefu wa wataalam hawa. Moja ya jambo hilo katika baadhi ya maeneo inawezekana ni sababu anayoitoa Mheshimiwa Ismail Iwvatta, kwamba wanavutiwa zaidi na maeneo ya Miji kwa sababu mbalimbali. Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nilitaka tu kwa kweli kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba sababu kubwa kabisa ni uchache wa wataalam waliopo hivi sasa hapa nchini. Hilo ndilo jambo kubwa na ndiyo tatizo kubwa, sababu nyingine kama zipo ni za ziada. Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niongeze vile vile kwamba kwa kuwa swali lake kusema kweli ni la kisera, siwezi nikazungumzia suala la mishahara kuongezwa kwa Madaktari wangu, Wizara zinazohusika nina hakika zinajua hilo na pengine wanafanya juhudi ili kujaribu kuona ni nini kinaweza kufanyika katika eneo hilo. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongezee majibu ya ziada kwenye majibu ya nyongeza ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI kuwa ni kweli mishahara ni moja ya mambo ambayo yanavutia watumishi wa Serikali kufanya kazi au kuwepo kazini. Lakini si mishahara peke yake ambayo kwa kweli ndiyo inayowafanya wabaki Serikalini. Naomba tuzingatie vile vile suala la mazingira mazuri ya watumishi wa Serikali kufanyia kazi wakiwemo Madakari. Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ningependa vile vile kulielezea Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inatambua kazi nzuri wanayoifanya Madaktari na kwa hiyo pamoja na kuwaongezea watumishi wa Serikali mishahara kila mwaka wakati Serikali inapokuwa na nafasi, Madaktari wamekuwa wakipewa mshahara zaidi kuliko wengine na 3 bado Serikali itajitahidi kuboresha mazingira yao pamoja na kuwaongezea mishahara kila inapowezekana. (Makofi) MHE. JOEL N. BENDERA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia na mimi nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba tatizo kubwa ni uchache wa Madaktari na Wauguzi katika hospitali zetu kama ilivyo katika Hospitali ya Mbulu, Korogwe na hospitali nyingine nyingi, sekta hii ya afya ni muhimu na katika Bajeti ya safari hii huduma za jamii zimeongezwa asilimia ya fedha. Je, Serikali katika kutatua tatizo hilo haioni sasa kwa sababu ya umuhimu wa kupata Madaktari, kufanya programu maalum ya kuongeza wataalam hawa katika nchi hii ili kujaza mapengo ambayo ni mapungufu katika Wilaya na Zahanati zote katika nchi hii kama inavyofanya kwenye Sekta ya Elimu? NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo analizungumza Mheshimiwa Joel Bendera, ndilo ambalo limekwishafanyika au linaendelea kufanyika kila mwaka. Hivi sasa idadi ya Madaktari wanaoingia Muhimbili imeongezeka, tuna vyuo vingine vya Bugando na KCMC na vile vile katika vyuo ambavyo viko chini ya Wizara ya Afya wale Matabibu au tuseme AMOs na Clinical Officers idadi yao pia imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka. Lengo la hatua hizi zote ni kuongeza idadi ya wataalam wanaoweza kutoa huduma katika Wilaya zetu. WAZIRI WA SAYANSI, TEKNOLOJIA NA ELIMU YA JUU: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongeza kwenye majibu mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa taaluma hizo muhimu hasa Madaktari ya kwamba sasa bado uwiano wa wagonjwa na Daktari ni Daktari mmoja kwa wagonjwa 24,000, Serikali imeamua kwamba itawasomesha Madaktari na kuwalipia bila kujali kama ni Chuo cha Umma ama kama ni Chuo cha Serikali. Kwa hiyo, tumetenga fedha katika suala hili. Ahsante. (Makofi) Na. 51 Ushuru wa Maegesho ya Magari Jijini Dar es Salaam MHE. MARGARETH J. BWANA aliuliza:- Kwa kuwa wananchi wa Dar es Salaam wamekuwa wakitozwa shilingi 300/= kama ushuru wa maegesho ya magari kwa kila saa moja:- (a) Je, Serikali haioni kwamba hali hiyo imekuwa kero kwa wakazi wa Jiji na kuwaongezea mzigo wa kodi usio wa lazima? 4 (b) Kama kuna ulazima wa ushuru huo kutolewa; je, tangu utaratibu huo uanze, ni kiasi gani cha fedha kimekusanywa; na Serikali imefaidika vipi na mapato hayo? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margareth Bwana, Mbunge wa Viti Maalum, swali lake lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Naibu Spika, ushuru unaotozwa na Jiji la Dar es Salaam kwa kutoa huduma ya maegesho ya magari ulianzishwa kutokana na hali halisi ya mahitaji ya huduma