MKUTANO WA KUMI NA SABA Kikao Cha Tano
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA _______ MAJADILIANO YA BUNGE __________ MKUTANO WA KUMI NA SABA Kikao cha Tano - Tarehe 11 Novemba, 2019 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba tukae. Tunaendelea na Mkutano wetu wa Kumi na Saba na leo ni kikao cha tano. Katibu. NDG. MOSSY LUKUVI – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Tunaanza na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, swali linaulizwa na Mheshimiwa Mary Pius Chatanda Mbunge wa Korongwe Mjini. Na. 56 Ukarabati wa Shule Korogwe MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:- Serikali imefanya kazikubwa sana ya ukarabati wa Shule ya Sekondari Korogwe lakini haikuunganisha nyumba za Walimu zilizopo Shuleni hapo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzikarabati nyumba hizo? 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) SPIKA: Majibu ya swali hilo, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Jafo tafadhali. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari Korogwe ni miongoni mwa shule 45 zilizokarabatiwa katika awamu ya kwanza ya ukarabati wa shule kongwe nchini. Ukarabati wa shule kongwe awamu ya kwanza ulihusisha vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, mabweni, maabara, ofisi za walimu, majengo ya utawala, mabwalo ya chakula na majiko, mifumo ya maji safi na taka na mifumo ya umeme. Mheshimiwa Spika, ukarabati wa shule kongwe awamu ya kwanza haukuhusisha nyumba za walimu kutokana na sababu za kibajeti.
[Show full text]