Majadiliano Ya Bunge ______
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ______________ MAJADILIANO YA BUNGE _____________ MKUTANO WA SABA Kikao cha Kumi na Moja – Tarehe 23 Aprili, 2012 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU Na. 120 Kutoridhisha kwa Hadhi ya Mkoa wa Dodoma MHE. MOZA A. SAIDY aliuliza:- Pamoja na kuwepo kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), bado hadhi ya Mkoa wa Dodoma zikiwemo barabara hairidhishi:- (a) Je, kuna tatizo gani katika Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA)? (b) Je, ni lini barabara za Mji wa Dodoma za Ipagala, Ilazo, Kisasa, Swaswa, Makulu na kadhalika zitatengenezwa ili ziwe na hadhi inayoendana na dhana ya Makao Makuu? SPIKA: Mheshimiwa Moza utahama hiyo microphone, Waziri Majibu. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moza Abeid Saidy, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- 1 (a) Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma ilianzishwa kwa lengo la kupanga na kuendeleza Mji wa Ddoma ili kuwa na hadhi ya Makao Makuu nchini. Ili kutekeleza kazi hii, mwaka 1976 uliandaliwa mpango kabambe ( Master Plan ) wa Mji Mkuu uliotenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Kwa mfano barabara, mfumo wa maji taka na maji safi, maeneo ya viwanja vya makazi, Huduma za Jamii, Biashara, Taasisi, Viwanda, maeneo ya wazi na kadhalika. Mwaka 2011 Mamlaka ilianza kufanya mapitio ya Mpango Kabambe ili uweze kwenda na wakati. Zoezi hili linatarajiwa kukamilika hivi karibuni. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu haijafanikiwa kutekeleza mpango wake kama ilivyotarajiwa kutokana na tatizo kubwa la upatikanaji wa fedha za kutosha. (b) Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara za Ipagala, Ilazo na Swaswa kwa kiwango cha changarawe umeanza katika mwaka wa fedha 2010/2011 na unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2012/2013. Barabara za eneo la Kisasa zenye urefu wa kilomita 11.856 kama alivyoziulizia Mbunge, zinajengwa hivi sasa kwa kiwango cha lami na barabara za eneo la Makulu zinatarajiwa kuanza kuboreshwa katika mwaka wa fedha wa 2013/2014. Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mradi kabambe kuboresha barabara za Mjini Dodoma. Miradi hii itatekelezwa kwa awamu mbili kwa kisimamiwa na CDA pamoja na Manispaa ya Dodoma. Miradi hii kwa jumla itagharimu jumla ya USD 37.7. Mpaka sasa zaidi ya shilingi bilioni 6.3 zimekwisha kutumika tangu awamu ya kwanza ya utekelezaji wa miradi hii ilipoanza mwezi Agosti mwaka 2011, ambapo barabara za Kisasa na Chang’ombe zenye urefu wa Km.15.65 zinaendelea kujengwa ambapo asilimia 30 ya ujenzi umekamilika. Pia ujenzi wa barabara za Mtendeni Market , Tembo, Tabora, Nkuhungu, Chamwino, Chang’ombe zenye urefu wa Km.11.17 zimekamilika kwa asilimia 23.87. Katika kuboresha Miundombinu ya Maji Serikali hivi sasa inaendelea na mradi wa usambazaji mabomba ya Maji yenye urefu wa km.29 unaendelea katika eneo la Kisasa. Mradi huu unagharimu kiasi cha shilingi 846 milioni na unatarajiwa kukamilika kati ya mwezi Juni na Agosti, 2012. Aidha, ujenzi wa bomba la majitaka la urefu wa Km.6 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.2 unaendelea. 2 MHE. MOZA A. SAIDY: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Waziri yasiyokuwa na matumaini, Kwa kuwa Serikali inatenga pesa ndogo ya kuweza kuendesha sekta hii ya CDA. (a) Je, Serikali sasa hivi inaonaje kukitoa chombo hiki kwa kuwa kimeanza kwa muda mrefu bila mafanikio yeyote na kuwanyanyasa wananchi katika mji huu wa Dodoma na Watanzania kukitoa na kubaki kuwa Manispaa? (b)Kwa kuwa, utekelezaji umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu, Je Serikali kweli ina dhamira ya kuhamishia Makao Makuu ya Nchi Dodoma kwa utekelezaji wake ambao unadai miradi na miundombinu ambayo inatekelezwa mpaka sasa hivi hakuna viwanda hakuna kitu chochote ambacho kinaendelea katika Mji huu wa Dodoma. Je, Serikali inatuambia nini wananchi na Watanzania kwa ujumla kukitoa chombo kinachoitwa CDA ambacho kinawatenga wananchi? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU-SERA, URATIBU NA BUNGE: Mheshimiwa Spika, Nataka kukiri kwamba tangu CDA imeanzishwa mambo mengi sana yamefanyika hapa Mjini na sisi Wabunge wengi ni mashahidi. Katika Mji angalau umepangika vizuri ukilinganisha na Miji mingi ya Tanzania ni Dodoma na hii kazi imefanywa vizuri tangu CDA ilipoanzishwa kutokana na utekelezaji wa Master Plan . Kwa hiyo kusema kwamba hakuna kilichofanyika kabisa na hakuna matumaini hapo sasa kidogo tumetia chumvi. Yapo mambo makubwa yamefanyika hapa. Mheshimiwa Spika, leo nakupa takwimu na ukifika pale Mjini utakuta kazi inaendelea. Kwa miaka miwili tu kuna kazi inafanyika ya dola milioni 37.7 niambie Wilaya gani nyingine Mjini hapa Tanzania hivi sasa ambayo inatekeleza miradi ya barabara tu ya dola milioni 37.7. Sasa jiulize kwanini Dodoma, ni kwa sababu ya madhumuni ya Dodoma ya kuwa Makao Makuu. Kwa hiyo, kazi ya uimarishaji miundombinu na haiwezi kukamilika kwa mara moja. Chombo hiki hakiwezi kutoka mpaka kikamilishe kazi yake. Tuna Master Plan mpaka itakapokamilika ndiyo CDA itatoka, lakini kwa sasa haitatoka. Sasa hivi tunaimarisha marekebisho fulani tunayafanya ili kukipa nguvu zaidi na kujenga mahusiano ya karibu zaidi ya CDA. 3 Mheshimiwa Spika, kwa maswali yote aliyouliza Mbunge nataka kumhakikishia kwamba Serikali itaendelea kutenga pesa kwa kushirikiana na wadau wengine ili kutimiza lengo la CDA ambalo wananchi wa Tanzania waliamua. (Makofi) MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona, mimi napenda kumwuliza Waziri, barabara za majengo katika Mji wa Dodoma ni mbaya sana, lakini pia kuna mtaro ambao unapita katikati ya soko mpaka kwenda Hospitali ya Mkoa ambayo ni mchafu umejaa taka na vinyesi, na unahatarisha maisha ya watu. Je, ni nani anastahili kusafisha mtaro huu kati ya CDA na Mamlaka ya Manispaa ya Mji wa Dodoma? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE: Mheshimiwa Spika, kazi ya CDA huwa ni kujenga miundombinu, ikishakamilika inakabidhi Manispaa, lakini nakuhakikishia nitakwenda kuagiza mamlaka inayohusika maana hapa siyo kutaja nani anayehusika, nafikiri Mbunge anataka kazi hiyo ya kusafisha huo mtaro wa kuondoa hicho kinyesi ifanyike. Kwa hiyo, nitahakikisha kwamba leo hii nitakwenda mamlaka zinazohusika kupitia Mheshimiwa Mwanri yupo hapa amesikia ili kazi hiyo ianze kufanyika leo. (Makofi) Na. 121 Upandishaji Hadhi Barabara Inayounganisha Wilaya MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:- Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi barabara inayounganisha Wilaya za Igunga, Uyui na Singida Vijijini kupitia Vijiji vya Mwanzugi, Itumba, Mhamamoja, Seregei, Susujanda, Mswaki(Mpyagula), Loya hadi Iyumba ili iweze kuhudumiwa na TANROADS na kujengwa kwa kiwango cha lami? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:- 4 Mheshimiwa Spika utaratibu wa kupandisha hadhi barabara za Wilaya kuwa za Mkoa na kuhudumiwa na TANROADS ni mapendekezo hayo kujadiliwa katika vikao vya Halmashauri, Kamati za Ushauri za Wilaya DCC na Bodi ya barabara ya Mkoa, maazimio ya Bodi ya Barabara ya Mkoa huwasilishwa katika Wizara ya Ujenzi ambayo inadhamana ya kupandisha hadhi barabara kuwa ya Mkoa. Mheshimiwa Spika, taarifa zilizopo ni kwamba vikao vya kisheria vinavyotakiwa kupitisha mapendekezo haya havijafanyika. Hivyo mapendekezo hayo yatakapopitishwa rasmi kwenye vikao hivyo yatawasilishwa katika Wizara ya Ujenzi yenye dhamana kwa mujibu wa sheria. Hivyo tunamshauri Mbunge aishauri Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ipitishe wazo hili katika vikao vilivyotajwa hapo juu ili uamuzi uweze kufanyika. MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika nakushukuru sana, na namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri yenye maelekezo mazuri, naomba nimwulize maswali mawili ya nyongeza. (a) Je, Serikali inafahamu kwamba barabara hii inayounganisha Wilaya za Singida Vijijini, Uyui na Igunga ni barabara ambayo inatumika kubeba mazao ya mifugo na mazao ya kilimo kwenda kwenye soko Igunga na kwingineko hadi Dar es Salaam? (b)Serikali itakuwa tayari basi kutekeleza mradi huo wa kupandisha barabara hiyo kuwa ya Mkoa endapo vikao vya DCC pamoja na Bodi ya Barabara itakapopeleka maombi huko Wizarani? (Makofi) NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Spika, mimi nafahamu hivyo kwamba barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi. nafahamu kwamba mazao ya mifugo pamoja na mazao ya kilimo. nafahamu kwamaba binadamu wanapita kule, najua kabisa jambo hili wala sina tatizo kabisa na Mheshimiwa Kafumu kuhusu hili analosema. Mimi ninachoweza kumWahidi hapa kwenye swali la pili la kusema kwamba tutapandisha daraja barabara ile utaratibu ni huo niliousema hapo. Waende katika Road Board ya Mkoa wakubaliane na baadaye sisi na yeye tutashirikiana ili kumshawishi Waziri wa Ujenzi ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kupitisha barabara hii na kuipandisha hadhi ili iweze kuwa katika hali hiyo anayoisema. 5 SPIKA: Ahsante tunaendelea na swali lingine sikumwona mtu aliyesimama kabla, yaani linaloulizwa swali la pili ndiyo msimame akiwa amejibu halafu mnasimama hiyo hapana. Na. 122 Mashamba ya Kilimo Mgongola-Mvomero MHE. ABDULKARIM E. H. SHAH (K.n.y. MHE. ABDULAZIZ ABOOD) aliuliza:- Mashamba ya Kilimo cha Mpunga yaliyoko Mgongolo Wilayani Mvomero, yalimilikiwa na wakulima tangu mwaka 1970. Lakini wakulima wamepokonywa mashamba hayo yamegawiwa kwa wafugaji. Viongozi