Majadiliano Ya Bunge ______
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ________ MAJADILIANO YA BUNGE __________ MKUTANO WA KUMI NA SITA Kikao cha Thelathini na Saba - Tarehe 30 Julai, 2004 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Pius Msekwa) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA USHIRIKA NA MASOKO: Hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Ushirika na Masoko kwa Mwaka wa Fedha 2004/2005. MHE. DR. AARON D. CHIDUO (k.n.y. MHE. WILLIAM H. SHELLUKINDO - MWENYEKITI WA KAMATI YA UWEKEZAJI NA BIASHARA): Taarifa ya Kamati ya Uwekezaji na Biashara Kuhusu Utekelezaji wa Wizara ya Ushirika na Masoko kwa Mwaka wa Fedha Uliopita, Pamoja na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2004/2005. MASWALI NA MAJIBU Na.345 Viwanda/Mashirika Yaliyobinafsishwa MHE. BERNARD K. MEMBE aliuliza:- Kwa kuwa Serikali imeweka mikakati maalum ya kuwasaidia Wananchi katika kumiliki mashirika yanayobinafsishwa ikiwa ni pamoja na kuuza baadhi ya mashirika kwa Watanzania kwa kutumia thamani ya vitabu badala ya thamani halisi kwenye soko; na kwa kuwa, moja ya matatizo yaliyopo ni kwa baadhi ya watu waliouziwa mashirika 1 hayo hawajaanza ukarabati na uzalishaji katika mashirika/viwanda hivyo na kusababisha ukosefu wa ajira kwa vijana wetu:- (a) Je, ni mashirika na viwanda vingapi ambavyo havijaanza uzalishaji hadi sasa? (b) Je, sasa Serikali ipo tayari kupokea lawama kwa kuwaendeleza hao wanaolegalega katika kufufua viwanda/mashirika yaliyobinafsishwa? NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ABDISALAAM ISSA KHATIBU)(k.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UBINAFSISHAJI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bernard Membe, Mbunge wa Mtama, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mashirika na viwanda vipatavyo 13 havijaanza uzalishaji tangu vibinafsishwe. Baadhi ya mashirika/viwanda hivyo ni Morogoro Tanneries, Moshi Tanneries, Mwanza Tanneries, Tanzania Bag Corporation (Moshi), Moshi Hotel, TAFICO (Dar ed Salaam), baadhi ya mashamba ya mkonge yaliyobinafsishwa kwa Katani Ltd., Kiwanda cha Chai Dabaga, Iringa, Mkata Saw Mills Ltd., UFI, Pugu Kaolin Mines Ltd., Morogoro Polyester Textile Mills Limited na Mikumi Wildlife Lodge. (b) Mheshimiwa Spika, sababu mbalimbali zimefanya mashirika na viwanda husika kushindwa/kuchelewa kuanza kufanya kazi. Baadhi ya sababu hizo ni viwanda kuwa katika hali mbaya sana na hivyo kuhitaji mitaji mikubwa. Vilevile teknolojia katika mashirika/viwanda vingi imepitwa na wakati. Hali hii huwalazimisha wawekezaji kutafuta teknolojia ya kisasa ambayo gharama yake ni kubwa na pia inahitaji kufundisha wataalam wa kuitumia kwa ufanisi na tija. Baadhi ya sera zetu kuwa kikwazo kwa wawekezaji. Mfano hapa ni viwanda vya ngozi ambavyo vilishindwa kuanza kazi kwa sababu sera zilizokuwepo miaka michache iliyopita, zilikuwa zikiwavutia zaidi wauzaji ngozi ghafi katika masoko ya nje ya nchi badala ya kuzisindika hapa nchini. Kwa bahati nzuri, Serikali imeshughulikia tatizo hili kwa kutoza kodi (Export Tax) kwenye ngozi ghafi zinazouzwa nje ya nchi. Baadhi ya wawekezaji kushindwa kupata mikopo ya Mabenki kutokana na riba kubwa na kukosekana kwa dhamana za mikopo na kadhalika. Pia baadhi ya wawekezaji kupeleka malalamiko yao Mahakamani huko tukisubiri maamuzi. Mheshimiwa Spika, Serikali imewasiliana na wahusika wote na kubaini matatizo yanayowakabili. Imedhihirika kwamba, wawekezaji wengi wana sababu za msingi na hivyo Serikali imewapa muda zaidi wa kutekeleza mipango yao kulingana na mikataba ya ubinafsishaji. Kwa wawekezaji ambao imebainika kuwa hawana sababu za msingi, Serikali imechukua hatua za kisheria kwa lengo la kuyachukua (repossess), mashirika/viwanda 2 husika ili waweze kutafutwa wawekezaji wengine watakaoweza kukidhi malengo ya ubinafsishaji. Kwa vile hatua mbalimbali zimechukuliwa ili kutatua tatizo hili, Serikali haipo tayari kupokea au kubebeshwa lawama kuhusu suala hili. Serikali ipo tayari kupokea ushauri na kuufanyia kazi kikamilifu kutoka kwa Mheshimiwa Bernard Membe na Waheshimiwa Wabunge wengine wote, unaolenga katika kuboresha utendaji wa mashirika yaliyobinafsishwa. MHE. BERNARD K. MEMBE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:- (a) Kwa kuwa wawekezaji wote wanafuata business plan na kwenye business plan wanaji-commit kwamba watazalisha, wataleta ajira na wataendeleza ufanisi wa viwanda hivyo na kukiuka hilo maana yake ni kwamba, tayari wamejiondoa katika shughuli hizo na Serikali hasa PSRC, inatakiwa kuchukua hatua za mara moja za kuwafukuza na kuyatoa mashirika/viwanda hivyo kwa Watanzania wenye moyo huo. Kwa nini PSRC haifuatilii kwa makini na kwa haraka pale mikataba inapokiukwa ili mashirika haya yaweze kutolewa kwa Watanzania wenye moyo wa kuyaendeleza? (b) Kwa vile Mheshimiwa Waziri anasema Serikali haistahili lawama lakini ushauri, atakuwa tayari, sasa kwamba katika kipindi cha mwaka huu kabla ya Desemba, mashirika/viwanda vyote vilivyochukuliwa na watu hawa viorodheshwe, viondolewe ili Serikali iwaondoe na kuwapatia watu wengine na isipofanya hivyo ichukue lawama mwisho wa mwaka? NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ABDISALAAM ISSA KHATIBU): Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba, Serikali imeyafuatilia mashirika haya na nimetoa sababu mbalimbali zilizowafanya hao waliobinafsishiwa viwanda hivi kutoviendeleza, hii ni dhahiri kwamba, Serikali imekuwa ikifuatilia. Kama nilivyoorodhesha mashirika hayo 13, ina maana Serikali imefuatilia wapi wamekwama. Mheshimiwa Spika, vile vile kuna sababu ya msingi, kutokana na swali lako la pili kwamba, mashirika hayo tuyarejeshe, kuna sababu kubwa kwamba, Serikali imechukua hatua kupeleka Mahakamani. Kunapokuwa na Court Injunction, Serikali haiwezi kuchukua hatua nyingine tena zaidi ya hivyo, lakini bado inafuatilia. Lakini kama nilivyosema, Serikali ipo tayari kushauriana zaidi na Wabunge juu ya masuala haya sio kwamba ilitulia tu, ilikuwa inachukua hatua zinazohitajika ili kuyarejesha mashirika haya. MHE. ABDULA S. LUTAVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Naomba kuuliza swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa mimi naamini kwamba viwanda hivi vinavyozungumziwa sasa havikuwa vimeanzishwa tu kiholela na vilikuwa na mchango kwa Taifa hili, baada ya 3 mashirika haya kubinafsishwa na kupewa watu binafsi kuyaendesha ni nini imekuwa athari kwa uchumi wa Taifa hili kwa mashirika haya kutoendelea kufanya zile kazi zilizokuwa zimedhamiriwa toka mwanzo wakati huo huo wao walipokuwa wanaji- commit watafanya kazi hiyo sisi tulikubaliana nao kwamba kazi hizi watakuwa wameanza kuziendeleza katika muda gani baada ya wao kuchukua viwanda hivi? NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ABDISALAAM ISSA KHATIBU): Mheshimiwa Spika, bila shaka athari za kiuchumi ni kwamba, Wananchi waliopo karibu na viwanda hivyo au mashirika hayo, wamekosa ajira, vilevile Serikali itakuwa imekosa kodi, mapato, bila shaka haya yanatuathiri. Mheshimiwa Spika, lakini narudia tena kama nilivyojibu kwenye swali la msingi kwamba, hata kama alikuwa na business plan, kwa kuongeza ufanisi, matatizo mbalimbali waliyoyapata katika kuwekeza ili viwanda hivi viweze kujiendesha ndio yaliwazuia wasiendelee. Bila shaka natumai Mheshimiwa Mbunge, amenisikiliza vizuri sana, nimeorodhesha kama mambo matano ambayo yamewarudisha nyuma na mojawapo ni teknolojia. Wakati viwanda hivi vimeundwa vilikuwa na teknolojia ya zamani ambayo sasa hivi vingi vyao haviwezi kutumika lazima wabadilishe teknolojia na hili ni jambo ambalo linazuia wasiendelee mbele kuviendeleza viwanda hivi. Na. 346 Malipo ya STABEX ya Chai 1995/1996 MHE. WILLIAM H. SHELLUKINDO aliuliza:- Kwa kuwa malipo ya STABEX kwa wakulima ni njia nzuri sana ya kuwahamasisha wakulima hapa nchini ili waongeze bidii zaidi katika kuzalisha mazao yenye ubora wa kuweza kuingia katika ushindani wa kidunia; na kwa kuwa Serikali ilikubali kuwalipa wakulima STABEX ya Chai ya mwaka 1995/1996 na baadhi yao wamelipwa mwaka 2002 na baadhi hawajalipwa katika Vijiji vya Sagara, Mayo, Mbokoi, Kwehangala, Kweminyasa na Balangai:- (a) Je, Kampuni ya E.K. Mangesho and Company iliyopewa mkataba wa kusimamia malipo hayo ya STABEX ilipewa mwongozo gani na Serikali kuhusu ulipaji? (b) Je, katika Wilaya ya Lushoto walipaji hao walionana na nani kati ya hawa wafuatao, yaani Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya, Katibu Tarafa wa Tarafa za Bumbuli, Mgwashi na Soni, Maafisa Watendaji wa Kata za Mgwashi, Mayo, Bumbuli, Mponde na Funta? (c) Je, ni nani mwenye uamuzi wa mwisho wa kulipa au kutolipa wakulima wa vijiji nilivyovitaja kati ya Waziri mhusika na kampuni niliyoitaja? NAIBU WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA alijibu:- 4 Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa William H. Shellukindo, Mbunge wa Bumbuli, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:- Kampuni ya E.K. Mangesho ya Dar es Salaam iliajiriwa na Jumuiya ya Ulaya na National Authorizing Officer, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania kama Mkaguzi wa Ndani wa Hesabu za malipo ya STABEX ya chai ya mwaka wa 1995/1996. Utaratibu wa kulipa fidia chini ya STABEX 1996 - Tea, umeelezwa kwa kirefu katika mwongozo ulioandaliwa kwa ajili hiyo. Majukumu ya Mkaguzi wa Ndani wa Hesabu yamefafanuliwa chini ya utaratibu huo. Tayari Mheshimiwa William Shellukindo, amepatiwa nakala ya kumbukumbu hiyo. Chini ya mwongozo ulioandaliwa kwa ajili ya malipo ya STABEX ya chai:- (a) Malipo yangezingatia kiasi cha majani mabichi ambayo wakulima waliwasilisha kwenye viwanda vya kusindika chai au kwenye vituo vya kununulia chai kati ya tarehe 1 Julai, 1995 na tarehe