Bunge La Tanzania ______
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE _____________ MKUTANO WA NNE Kikao cha Kumi na Saba – Tarehe 6 Julai, 2006 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Samuel J. Sitta) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kabla hatujaingia katika kipindi cha Maswali Majibu, ninalo tangazo moja tu. Naomba muwatambue wageni wa Mheshimiwa Richard Nyaulawa, Mbunge wa Mbeya Vijijini ambao ni Madiwani 23 na Maafisa wa Wilaya watano kutoka Mbeya Vijijini. Wapo sehemu hii ya kulia pale, naomba wasimame Waheshimiwa Madiwani. Ohoo hawajafika. Basi tunatambua kwamba labda bado wako njiani. Ahsante. (Makofi) MASWALI NA MAJIBU Na. 157 Barabara ya Mkendo/Shabani MHE. VEDASTUSI M. MANYINYI aliuliza:- Kwa kuwa barabara ya Mukendo/Shabani ni kioo cha Manispaa ya Musoma, na kwa kuwa barabara hiyo ni ya muda mrefu na lami yake imeharibika sana; na kwa kuwa, mwaka jana Serikali iliahidi kuikarabati barabara hiyo kuanzia Januari, mwaka 2006:- Je, ukarabati wa barabara hiyo utaaanza lini na kukamilika baada ya muda gani? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedastusi Mathayo, Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini kama ifuatavyo:- 1 Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ilikwishaagiza Miji yote iliyopandishwa hadhi kuwa Manispaa kuandaa makisio kati ya urefu wa kilomita 3 hadi 4 za barabara kwa ajili ya kuandaa mpango wa ukarabati. Halmashauri ya Manispaa ya Musoma ni kati ya Manispaa zilizokwishawasiliana makisio hayo. Aidha, katika mpango uliowasilishwa Halmashauri imepanga kukarabati barabara za Mkendo, Shabani, Sokoni, Kusaga na Indira Ganthi kwa kiwango cha lami zenye jumla ya urefu wa kilomita 4.8 kati ya barabara zake zote zenye urefu wa kilomita 14.
[Show full text]